Mwanza. Licha ya kupungua kwa idadi ya matukio ya ukatili dhidi ya watoto mkoani Mwanza, vitendo vya ubakaji bado ni tishio kwa usalama na ustawi wao.
Hali hiyo imelifanya Jeshi la Polisi kushirikiana na wadau wa maendeleo kuimarisha kampeni za ulinzi wa mtoto kupitia elimu na uhamasishaji kwa umma.
Katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Julai mwaka huu, jumla ya matukio 135 ya ubakaji yameripotiwa mkoani hapa, yakiwa ni pungufu ya matukio 20 ukilinganisha na 155 yaliyoripotiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2024.
Katika juhudi hizo, Shirika la SOS Children’s Village limelikabidhi Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza vifaa vya kuelimisha jamii vyenye thamani ya Sh14 milioni, vikiwemo spika 10, vibao 70 vyenye ujumbe mbalimbali, na mabango manne.
Vifaa hivyo vitatumika kwenye shule, masoko, vituo vya mabasi na maeneo ya mikusanyiko ili kuhamasisha jamii kuhusu ulinzi wa mtoto.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo leo Julai 29, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa amesema licha ya matukio ya ubakaji kuendelea kuwa juu, takwimu za matukio ya ukatili wa kijinsia yakiwemo ubakaji, ulawiti, wizi wa mtoto, kutupa mtoto na kuzini mahalimu yamepungua kwa asilimia 11.46 ukilinganisha na mwaka jana.
Amesema kati ya Januari hadi Julai 2025, matukio 147 ya ukatili dhidi ya watoto yameripotiwa yakiwemo 135 ya ubakaji, wizi wa mtoto (2), kutupa mtoto (7) na kuzini mahalimu (3), ukilinganisha na matukio 177 yaliyoripotiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2024, yakiwemo 155 ya ubakaji, wizi wa mtoto (5), kutupa mtoto (12), na kuzini mahalimu (5).
“Haya makosa ya kubaka, kulawiti, wizi wa mtoto, kuzini mahalimu kuna tofauti ya matukio 25 kati ya mwaka huu na mwaka jana, kwa hiyo yamepungua kwa asilimia 11.46.
Kwenye hili Jeshi la Polisi hatuwezi kujipongeza peke yetu, haya ni mafanikio yetu sote wadau wote wamechangia kushuka kwa matukio ya kihalifu,” amesema Mutafungwa.
Amesema matukio hayo yamepungua kutokana na mafanikio ya kampeni ya ‘Mwanza Salama, Mtoto Salama’ iliyozinduliwa Aprili 22, mwaka huu, ambapo kupitia uelimishaji katika jamii, waliwafikia watu 149,777 kwenye shule, vyuo, misikiti, makanisa, mikutano ya hadhara na vyombo vya habari.
“Ile sauti tuliyopaisha kwa ujumbe kwenye jamii ilikuwa kubwa na matokeo tumeanza kuyaona. Mimi ni muumini wa kuelimisha jamii kama njia mojawapo ya kuzuia matukio ya uhalifu,” amesema Mutafungwa.
“Hawa watoto waliozagaa mitaani wanaomba fedha na chakula. Sisi tunaohusika na mambo ya uhalifu tunalitazama hili kwa tafsiri pana, tunaona kwamba kizazi hiki baadaye kinakwenda kuwa sumbufu. Tunawapongeza wanaojitokeza kusaidia jambo hili, wanafanya kazi kubwa,” amesema Mutafungwa.
Naye Kaimu Meneja Miradi wa SOS Children’s Village Mwanza, Elizabeth Swai amesema wanafanya jitihada hizo ili kuhakikisha mtoto anafikia malengo yake akiwa salama.
Amesema kupitia kampeni ya ‘Mwanza Salama, Mtoto Salama’ iliyofanyika Aprili 22 hadi Mei 22 mwaka huu, walitoa elimu ya kupinga ukatili kwa watoto katika kata 21, shule za msingi 10, sekondari saba, vyuo viwili, masoko na vituo vya mabasi mbalimbali.
“Tunaamini kabisa kuwa kupitia vifaa hivi tulivyovitoa, elimu itaendelea kuwa endelevu kwenye jamii na watoto watabaki salama. Tunaamini katika usalama ndiko tunapopata amani ya kitaifa na ya kifamilia, ambayo itamsaidia mtoto afikie malengo yake,” amesema Swai.
Kwa upande wake, Kaimu Ofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Mwanza, Godlove Lulandala amesema kampeni hiyo imeleta mafanikio makubwa kwa kusaidia kuibua matukio mengi ya ukatili dhidi ya watoto, ambayo awali yalikuwa hayajafahamika wala kuripotiwa.
“Baadhi ya matukio hayo yameanza kufanyiwa kazi kisheria, huku mengine yakitatuliwa ndani ya jamii kupitia ushirikiano kati ya wadau na mamlaka husika. Jamii imeanza kutambua maeneo sahihi ya kuripoti vitendo vya ukatili,” amesema Lulandala.