Saa 10 za kusubiri moshi wa kijani watiania CCM

Dodoma. Zimepita zaidi ya saa 10 tangu waandishi wa habari wakusanyike katika ukumbi wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM), kuitikia wito wa chama hicho, kinachotarajia kutoa matokeo ya mchujo wa watiania wa ubunge, uwakilishi na udiwani.

Anayesubiriwa ni Katibu wa Halmashauri Kuu ya chama hicho, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla ambaye ndiye mamlaka ya kuisemea CCM baada ya mfululizo wa vikao vya mchujo huo.

Ni zaidi ya saa 10, kwa sababu taarifa ya awali ya chama hicho, ilieleza kwamba Makalla angezungumza na wanahabari saa 11:00 jioni katika ukumbi huo, lakini haikufanyika hivyo.

Ilipofika saa 11:00, chama hicho kilitoa taarifa nyingine kuwa mkutano huo wa Makalla na waandishi wa habari ungefanyika saa 3:30 usiku, lakini nao uliota mbawa.

Baada ya taarifa hiyo, hakukutolewa tangazo lingine lolote kueleza ni muda gani mkutano huo utafanyika, huku waandishi wa habari wakiendelea kuvuta subira katika ukumbi huo.

Kinachoteka subira za wanahabari hao, ni unyeti wa taarifa wanazosubiri za majina yaliyopendekezwa na kikao cha Kamati Kuu, kilichoketi Ikulu ya Chamwino, Dodoma kuanzia asubuhi ya Julai 28, 2025.

Kikao hicho kimeketi kufikiri na kupendekeza majina ya watiania zaidi ya 5,000 wa ubunge waliojitokeza kwa ajili ya nafasi hizo.

Kabla ya kikao hicho, kulitangulia kikao cha kamati ya usalama na maadili ya CCM, iliyoanza asubuhi ya Julai 27, 2025 na kutamatika saa 9 usiku Julai 28, 2025.

Ilipofika saa 3:13 usiku, mmoja wa wasaidizi wa Makalla, Abubakari Liongo aliingia ukumbini na kuwaahidi wanahabari kuwa kiongozi huyo angeingia nusu saa baadaye.

“Hongereni kwa uvumilivu, huu sasa ndiyo uandishi wa habari na hapa mtapata story (habari) kubwa sana, naomba msichoke, kiongozi anakuja ndani ya nusu saa kuanzia muda huu,” amesema Liongo, kisha akaondoka.

Ahadi hiyo iliota mbawa, ikafika saa 5:40. Muda huo akatoka ofisa mwingine wa chama hicho, aliyevalia shati ya kijani, naye aliwasihi wanahabari wasiondoke ukumbini hapo kwani Makalla angeingia muda wowote kuanzia saa hiyo.

Hiyo nayo haikutimia, huku baadhi ya waandishi wa habari walionekana kukata tamaa na kuondoka lakini kundi kubwa lilibaki pamoja na maofisa kadhaa wa CCM.

Haikuwa rahisi kwa baadhi ya wanahabari kuuzuia usingizi, walijikuta wakisinzia na hivyo kuzua utani kutoka kwa wale waliobaki macho.

Ilipofika saa 9:00 usiku ofisa mmoja wa CCM aliwatangazia waandishi kuwa kikao kisingefanyika usiku huo, kimeahirishwa hadi saa 4:00 asubuhi leo Julai 29, 2025.

Hata hivyo, hadi wakati taarifa hii inachapishwa saa 5:40 asubuhi kikao kilikuwa hakijafanyika wala majina hayo kutangazwa.