Dar es Salaam. Ili kuimarisha utendaji kazi katika sekta ya umma, Serikali imedhamiria kuanzisha mfumo wa upimaji kwa kutumia mitihani ya lazima kwa maofisa walioteuliwa au kupandishwa vyeo vya uongozi.
Hatua hiyo mpya ni sehemu ya kuhakikisha watu wenye uwezo na uelewa thabiti wa shughuli za utumishi wa umma ndio wanaokabidhiwa majukumu muhimu ya kuendesha taasisi au mashirika ya umma.
Hayo yameelezwa jana, Jumatatu Julai 28, 2025, na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Moses Kusiluka, wakati akifungua mafunzo elekezi ya siku nne kwa wakuu wa taasisi za umma 114 yaliyoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kushirikiana na Taasisi ya Uongozi.
Mafunzo hayo, ambayo yaliyoanza jana, yanatarajiwa kumalizika Julai 31, 2025, huku mada 14 zikitarajiwa kutolewa kwa watumishi hao sambamba na simulizi za viongozi waliofanikiwa.
Dk Kusiluka amesema uamuzi huo unatokana na kuwapo kwa wasiwasi kuwa maofisa wengi wa umma walipopandishwa kwenye nyadhifa mpya wanakosa hata maarifa ya kimsingi kuhusu jinsi taasisi za Serikali zilivyo.
Hali hiyo imesababisha utendaji kazi hafifu bila kujali wasifu alioubeba mhusika.
“Hivi ndivyo inavyofanyika duniani kote. Maendeleo katika nchi yoyote huanza na sekta ya umma yenye nguvu. Tuko mbioni kuanzisha mitihani kwa viongozi baada ya kuteuliwa au kupandishwa vyeo kwa lengo la kuboresha ufanisi na kuhakikisha malengo ya Serikali yanafikiwa,” amesema Dk Kusiluka.
Mbali na mchakato huo, Dk Kusiluka amesema kupitia mafunzo hayo, wakuu wa taasisi watakumbushwa na kuelekezwa ulazima wa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo katika utumishi wa umma, kwani ndiyo namna inayotumika kuendesha taasisi za Serikali.
“Umetoka nje ya Serikali, umekuja na uzoefu wa kuendesha taasisi, lakini ukifika unavurugwa na taratibu kwa sababu huamini kuwa kuna sheria, kanuni na taratibu. Unafanya makosa, ukija kugundua unakuwa mtuhumiwa, hali inayofanya ukose kujiamini,” amesema.
Amesema kukiuka utaratibu ni moja ya kichocheo cha uamuzi mbaya unaoweza kufanya taasisi kupata hasara.
Kubainisha changamoto wanazokutana nazo katika uendeshaji wa taasisi za umma na kubadilishana mbinu za kuzitatua ni moja ya jambo alilolizungumzia, huku akiakisi kile kilichosemwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Juma Mkomi juu ya hamisha hamisha ya watumishi.
“Changamoto zipo na Katibu Mkuu amezungumzia hasa katika suala la kuhamisha watumishi. Kama umeletewa mtu mwenye matatizo, wasiliana na Katibu Mkuu Utumishi. Tusihamishe watu.
“Ukipewa watu uwaangalie kwa mtazamo chanya, wafundishe, watu wanabadilika. Usimkatae mtu bila kumjua au kwa kumsikia,” amesema Dk Kusiluka.
Alitumia nafasi hiyo kuwataka kuzingatia misingi ya utawala bora katika usimamizi na uendeshaji wa taasisi wanazosimamia, kwani kuna tatizo kubwa la utawala bora.
“Mara zote unataka bosi wako akutawale vizuri wizara, taasisi au shirika iwe vizuri, lakini wewe hauko vizuri. Hivyo mtakumbushwa,” amesema.
Mbali na hayo, Dk Kusiluka amesema katika mwaka huu mpya wa fedha angependa kuona taasisi za umma zinaepuka matumizi yasiyo na tija na kuelekeza fedha zaidi katika maeneo ya vipaumbele vya kitaifa kama vile miundombinu, afya, elimu na huduma za kijamii.
“Watendaji wakuu wana jukumu la kuhakikisha taasisi zao zinaendeshwa kwa misingi ya ufanisi na uwajibikaji mkubwa,” amesema.
Amesema ili taasisi za umma ziongeze ufanisi, zinapaswa kujenga uwezo wa ndani wa taasisi kwa kuboresha rasilimali watu, teknolojia na miundombinu.
Pia amesisitiza kuwa taasisi za umma, kila moja kwa nafasi yake, zihakikishe zinashiriki katika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Dira hii imelenga kuiwezesha Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati wa juu, yenye viwanda, mifumo ya kiutawala yenye uwazi, na ustawi kwa wananchi wote.
“Tunatarajia pato la Taifa kufikia Dola trilioni moja ifikapo 2050, huku pato la mtu mmoja mmoja likifikia Dola 7,000 za Marekani. Hii siyo kazi ndogo, lakini tuna kila sababu ya kufikia lengo,” amesema Dk Kusiluka.
Awali, akizungumzia changamoto iliyopo ndani ya mashirika ya umma, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Juma Mkomi, amesema wanaamini baada ya mafunzo hayo wakuu wa taasisi watakuwa wapya na wataboresha utendaji kazi na miradi ya taasisi zao.
Hiyo ni kutokana na kile alichokieleza kuwa changamoto zipo, hasa kwa baadhi ya wakuu wa taasisi kuwa na tabia ya kuwakataa watumishi wapya wanaopelekewa pamoja na wale wanaohamia.
“Baadhi wakihamishiwa watumishi wanawakataa, kwa sababu tu hamjui alikotoka. Kama humjui alikotoka niulize mimi niliyemleta ametokea wapi. Lakini ukimkataa haileti maana nzuri. Umepewa kusimamia taasisi hiyo ni pamoja na watu, hivyo mtu yoyote utakayeletewa mpokee,” amesema Mkomi.
Pia, wapo baadhi ya watu wakiteuliwa kwenda kuongoza taasisi fulani, wanapofika ofisini wanaanza kutaka baadhi ya wafanyakazi waliowakuta waondolewe na kudai wana changamoto mbalimbali.
“Kama wana changamoto, ni jukumu lako kuwabadilisha. Imani yangu ni kuwa mafunzo haya yatatusaidia kujenga msingi imara wa usimamizi wa rasilimali watu katika taasisi,” amesema Mkomi.
Kwa upande wake, Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu, amesema anatarajia kuona taasisi za umma zenye mwelekeo wa kibiashara zinaongeza ufanisi wa kiutendaji, mapato na faida, na hivyo kupunguza utegemezi wa ruzuku kutoka Serikali Kuu.
“Taasisi hizi lazima ziendeshe shughuli zao kwa misingi ya kibiashara, zenye ushindani, ubunifu na tija, ili kuchangia kikamilifu kwenye pato la Taifa kupitia gawio na michango mingine,” amesema Mchechu.
Amesema jambo hilo linakwenda sambamba na kukumbatia matumizi ya Tehama, na hivyo taasisi za umma zinapaswa kuendelea kutenga bajeti kwa ajili ya uwekezaji katika Tehama na kuhakikisha mifumo inasomana ili kuongeza ufanisi.
“Lazima tukumbatie matumizi ya Tehama kikamilifu ili kuleta tija iliyotarajiwa. Mwisho wa siku tunataka kuona taasisi za umma zenye mrengo wa biashara, zinajiendesha kibiashara, na hivyo kupunguza au kuondokana kabisa na utegemezi kutoka Serikali Kuu,” amesema Mchechu.