Shaka atangaza kiama genge la wahalifu Kilosa

Dar es Salaam. Wakati Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka akitangaza kiama kwa kundi la watu alilolitaja ‘genge dogo la wachochezi linalotaka kuvuruga amani kwenye moja ya vijiji vya wilaya hiyo’, imeelezwa kuwa watu sita wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma hizo.

Shaka amezungumza na wananchi wa Kijiji cha Masungo ambao hivi karibuni walikuwa kwenye taharuki iliyosababisha watu wawili kujeruhiwa, huku baadhi ya wananchi wakitaja moja ya sababu ni mgogoro wa mipaka.

Akizungumzia katika mkutano wake na wananchi, Shaka amesema wote waliosababisha taharuki hiyo ni wachochezi wanaotaka kuleta uvunjifu wa amani katika kijiji hicho.

Amesema vitendo hivyo haviwezi kufumbiwa macho, akionya pia chokochoko za baadhi yao kuhusu mipaka na kuonya lugha ya “kuna migogoro ya mipaka kwenye kijiji hicho”.

“Leo ndiyo mwanzo na mwisho, kama kuna watu wana dhamira mliyoniambia sijui ya kumwaga damu, hawatomwaga hata mkojo, katika hiki kigenge kidogo cha wavunjifu wa amani, hakuna atakayekuwa salama, tutalisambaratisha lote na mtaishi kwa amani, umoja na upendo,” amesema.

Akizungumzia migogoro ya mipaka, Shaka amesema eneo hilo lilikuwa ni kata moja ya Namamboya kabla ya kugawanywa.

“Yalipogawanywa maeneo ya kiutawala wananchi mlishirikishwa ndipo uamuzi sahihi ukafanyika kwa mujibu wa sheria na eneo hili likagawanywa.

“Tangu wakati huo tumekuwa na vipindi vitatu vya uchaguzi, 2014, 2019 na 2024, kwanini hili la mipaka liibuke sasa? wanaoleta hii taharuki ni wachochezi na wanataka kuleta uvunjifu wa amani,” amesema.

Amesema genge dogo la watu linachochea taharuki hiyo kwa masilahi yao binafsi huku wananchi wakipinga kile kilichozungumzwa na baadhi yao, kwamba walipata hasira na kupigana si la kweli, limetengenezwa na watu wachache kwa masilahi yao binafsi.

“Niwaombe vijana msikubali kushawishika kwa namna yoyote kuingia kwenye uvunjifu wa amani,” amesisitiza Shaka.

Katika tukio hilo, Shaka amesema watu sita watuhumiwa wa kuhusika na vurugu hizo wamekatwa huku msako zaidi ukiendelea.

Amewataka wananchi kumpa taarifa binafsi kupitia simu yake ya mkononi juu ya genge hilo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama alipotafutwa na Mwananchi kwa simu kutaka kufahamu kinachoendelea katika tukio hilo, ametaka mwandishi aende ofisi.

“Utaratibu wa taarifa unajulikana, njoo ofisini,” amesema RPC huyo kwa kifupi.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Harodi Makamba amesema taharuki hiyo ilitokea kufuatia, wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kukata miti mikubwa iliyokuwa imepita kwenye laini kubwa ya umeme.

“Nilipigiwa simu na mmoja wa wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji cha Masungo, Jackson Mcharo na kunipa taarifa hizo, ikabidi niende eneo hilo kushuhudia nikakuta ni watu wa Tanesco walikuwa na chensoo (msumeno wa mnyororo).

“Nikawauliza kwa nini mnakata miti? Wakasema ni hii ambayo ipo kwenye laini kubwa, nikaikagua na kujiridhisha, hata hivyo walipokuwa wakiikata mingine iliangukia barabarani,” amesema.

Amesema aliwasiliana na wajumbe wa halmashauri ya kijiji na wakashauriana itolewe na wakipata mtu ambaye anafyatua tofali wamuuzie, ili wapate pesa ya kuongezea kwenye mambo ya maendeleo.

“Tuliwaita vijana wawili waje kuikatakata ili kuisogeza pembezoni, walipokuwa wakiendelea na kazi, walipigiwa yowe na wamama wawili na kusababisha watu kujaa.

“Wakati matukio haya yanafanyika walinipigia simu, nikawaambia waondoke eneo hilo, wakasema hawawezi kutokana na wingi wa watu, ikabidi nisogee eneo hilo nikawakuta wale wenye dhamira akiwamo huyu mmoja aliyekuwa na shoka,” amesema.