Simba yamalizana na straika Rwanda

MABINGWA wa zamani wa Ligi Kuu ya Wanawake, Simba Queens wamemalizana na straika wa AS Kigali, Zawadi Usanase kwa mkataba wa mwaka mmoja.

Huu unakuwa usajili wa pili rasmi kwa Simba baada ya awali kukamilisha taratibu zote na beki wa Yanga Princess, Asha Omary.

Kwa mujibu wa uongozi wa mchezaji huyo, Local Champions ni kwamba Usanase alisaini mkataba huo Julai 25, mwaka huu na atakuwa analipwa mshahara wa kiasi cha Dola 1000 za (sawa na Sh2.6 milioni).

Mbali na Simba kukamilisha dili hilo ambalo liko rasmi sasa, lakini Mratibu wa Simba, Selemani Makanya yupo mawindoni huko Rwanda yuko katika katika hatua za mwisho kumalizana na Umutesi Uwase Magnifique anayekipiga Indahangarwa WFC.

“Kiasi hicho kinamfanya kuwa mmoja wa wachezaji wa kike kutoka Rwanda kulipwa mshahara mrefu, kila kitu kimekamilika na alisaini mkataba wa mwaka mmoja wenye kipengele cha kuongeza kama atafanya vizuri,” alisema mmoja wa viongozi wake.

Inaelezwa kuwa Usanase huenda atavaa jezi namba 19 na atasafiri kutoka Rwanda kuja Tanzania Agosti 15, 2025 ili kujiunga na timu mpya kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa mashindano.

Usanase alijiunga na AS Kigali akitokea timu ya Scandinavia ya Rubavu Septemba 2020 kwa mkataba wa miaka mitatu na kwa kipindi hicho aliisaidia timu hiyo kushinda mataji mawili ya ligi, vikombe viwili vya Peace Cup, na Super Cup moja.

Msimu wa 2022/23 Usanase alimaliza na mabao 24 katika mashindano yote na uliopita aliibuka mfungaji bora akiweka kambani mabao 28.

Kiasili ni mshambuliaji wa kati lakini anamudu kucheza nafasi ya winga zote mbili kwa kasi, nguvu na ubora wa kufunga.

Nyota huyo anakuja kuziba pengo la mshambuliaji Jentrix Shikangwa aliyepewa mkono wa kwaheri akiitumikia Simba misimu mitatu. Katika msimu wa kwanza aliipa timu hiyo ubingwa na akaibuka mfungaji bora akiweka kambani mabao 17 ilhali uliofuata akamaliza na mabao manane akicheza mechi nane na huu mabao 24.

Hivyo Usanase ana kazi ya ziada kuonyesha ubora wa Shikangwa ambaye alikuwa hatari kwa makipa wa Ligi Kuu Bara akiwatungua atakavyo katika mashinmdano hayo.