Simba yazoa Sh20 bilioni, ikitambulisha mdhamini mpya

Simba imesaini mkataba wa miaka mitatu wenye thamani ya Sh20 bilioni na Kampuni ya ubashiri wa matokeo ya michezo ya Betway kama mdhamini mkuu wa klabu hiyo.

Mkataba wa udhamini huo unasainiwa leo Jumanne, Julai 29, 2025 jijini Dar es Salaam.

Kampuni hiyo ndio itakuwa mdhamini mkuu wa klabu hiyo kufuatia kuvunjwa kwa mkataba baina ya Simba na mdhamini mkuu aliyepita.

Mtendaji Mkuu wa Simba, Zubeda Sakuru amesema kuwa udhamini huo utakuwa na faida kubwa kwa klabu hiyo.

“Mkataba ambao tumeingia unakwenda kuleta mapinduzi kwenye mchezo wa soka hapa Tanzania na unakwenda kuongezea nguvu dhamira ya Simba kuwa klabu namba moja barani Afrika.

“Udhamini huu ambao thamani yake ni Bilioni 20 kwa miaka mitatu, unaonyesha namna Simba imedhamiria kuleta mabadiliko ya kuwa klabu kubwa,” amesema Sakuru.

Mkuu wa Udhamini wa BetWay Afrika, Jason Shielda amesema kuwa mkataba huo una maana kubwa kwa pande zote mbili.

“Huu ni zaidi ya ushirikiano na inatakiwa klabu zote zifaidike na jambo hili. Tunashirikiana na timu nyingi kubwa ambazo tunadhamini hivyo uzoefu huo utatusaidia kufanikisha jambo hili.

“Tumeingia Simba sababu ni timu kubwa Afrika, ni timu ambayo inajulikana pande zote za bara hili na hilo ndio tunaangalia zaidi kwenye biashara. Tulikuwa tukiifatilia kwa miaka karibu sita lakini sasa imekuwa kweli. Tunafuraha kufanikisha jambo hili,” amesema Jason.