Simulizi ya Profesa Mwandosya, shujaa wa saratani ya damu

Dar es Salaam. Ni safari ya huzuni, maumivu na mafunzo. Ndivyo unaweza kuelezea simulizi ya matibabu ya saratani aliyopitia mwanasiasa mkongwe, Profesa Mark Mwandosya wakati akipambania maisha yake nchini India.

Ni kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Juni 17, 2011 hadi Julai 14, 2012, kilichompa sababu ya kuandika kitabu kuhusu aliyopitia katika harakati za matibabu tangu alipobainika kuwa na saratani ya damu.

Leo, Julai 29, 2025, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Madini, Dk Doto Biteko amezindua kitabu kilichoandikwa na Profesa Mwandosya kikijulikana kama: “Living With Cancer: Diaries of Multiple Myeloma Patient.”

Kitabu hicho kilichochapishwa na kampuni ya Mkuki na Nyota Publishers Ltd, kinaelezea kumbukumbu yake katika kipindi chote alichokuwa akitibiwa ugonjwa huo nchini India, nyakati ngumu na za faraja alizopitia hadi kupona.

Akisimulia safari hiyo kwa kuonyesha picha mbalimbali kwa kila hatua aliyopitia, Profesa Mwandosya amesema alianza safari ya matibabu baada ya madaktari kubaini kwamba alikuwa mgonjwa licha ya yeye kujiona yuko sawa, huku akiendelea na kazi zake.

Amesema Julai 2011 baada ya kutoka kuonana na daktari wake, Dk Patrick Kisenge ambaye sasa ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), aliondoka kuelekea bungeni kwa ajili ya kuwasilisha hotuba yake ya bajeti akiwa Waziri wa Maji.

Akiwa njiani na dereva wake, alipokea simu ya Dk Kisenge ikimwamuru arudi Dar es Salaam kwa ajili ya safari ya kwenda kutibiwa nje.

“Nakumbuka aliongea na dereva wangu, akamwambia ‘mwendeshe polepole, usipite kwenye mabonde’. Alijua kwamba tayari hali yangu ilikuwa mbaya, namshukuru sana na kweli ugonjwa ulikuwa umefikia katika hatua ya juu,” amesema.

Profesa Mwandosya ambaye amekuwa waziri katika wizara mbalimbali nchini, amesema aliondoka kwenda India kuanza matibabu. Madaktari walimpokea na kumfanyia vipimo n a kumwanzishia matibabu.

“Baada ya kuchukuliwa vipimo, ilibainika kwamba pingili ya sita kwenye uti wa mgongo ilikuwa imeanza kupukutika. Ukiangalia picha hii (akionyesha), utaona kuna uwazi, hapa maana yake mifupa yangu ilikuwa inasagika, basi nikafanyiwa upasuaji,” amesema.

Akiwa hospitali nchini humo, amesema anakumbuka alitembelewa na watu mbalimbali akiwemo hayati Maalim Seif Sharif Hamad, Profesa Ibrahim Lipumba, Dk John Kijazi ambaye wakati huo alikuwa Balozi wa Tanzania nchini India.

Wengine ni pamoja na aliyekuwa Waziri Mkuu, Frederick Sumaye, Spika wa Bunge wakati huo, Anna Makinda, Adam Kimbisa, aliyekuwa Naibu Waziri wa Maji, Gerson Lwenge pamoja na Watanzania wengine wengi, jambo ambalo anasema lilimpa faraja kubwa.

“Nilipoanza kupata nafuu, nilipelewa kwenye wodi ya kawaida na baada ya muda nilipoimarika, nilipewa wiki mbili za kurudi nyumba kabla ya kurejea tena India kuendelea na matibabu,” amesimulia Profesa Mwandosya ambaye kitaaluma ni mhandisi.

Baada ya kurudi tena India, amesema ndipo akaanza matibabu yenyewe ya saratani, anasema yalikuwa matibabu magumu kwenye hatua alizopitia hasa ya kubadilisha damu mwilini mwake ingeweza kuchukua uhai wake.

Amesema matibabu aliyofanyiwa yalikuwa makubwa, miguu yake ilikuwa haifanyi kazi kabisa, umeme wa mwili ulikuwa hausambai mwili wote, nywele zake zote zilinyonyoka, lakini alikuwa akipata matumaini kutoka kwa watu waliokwenda kumtembelea.

“Nilipigwa dozi kubwa ya chemo-therapy kwa ajili ya kujaribu kuua seli za saratani. Madaktari wakaniambia kwa matibabu hayo nitapoteza nywele zote, mmoja akawa ananitania kwamba wana ma-wig mengi ya Kihindi, watanipatia nivae,” amesimulia huku watu wakicheka.

Amesema saratani siyo jambo dogo kwani ni kama hukumu ya kifo, kuipokea ni ngumu. Amesema watoto wake walipopata taarifa kwamba amebainika kuwa na saratani walianza kulia, lakini walikuwa mstari wa mbele kwenda hospitali kumfariji.

Profesa Mwandosya ametumia fursa hiyo kumshukuru Mungu kwa kumponya maradhi ya saratani, anaamini kwamba Mungu ndiye daktari mkuu anayeponya. Ameishukuru pia familia yake, madaktari wa Tanzania na India kwa kuhakikisha anapata matibabu bora.

“Hatua hii si mwisho, mapambano yanaendelea, lakini niko katika hali nzuri,” amesema Profesa Mwandosya wakati akielezea picha zilizopigwa na mke wake, Lucy Mwandosya, akiwa kwenye matibabu ya kila siku.

Kiongozi huyo mstaafu, ameishukuru pia nchi yake kwani imekuwa mstari wa mbele kutoa matibabu kwa magonjwa makubwa kwa Watanzania wote, na huko alikutana na Watanzania wengi waliokwenda kupatiwa matibabu.

“Watu wengi wanadhani kwamba nilikwenda kutibiwa India kwa sababu nilikuwa waziri, siyo kweli. Kwenye hospitali niliyokuwa, walikuwa wanakuja Watanzania wengi wa kawaida kutibiwa. Kwa hili, kwa kweli naishukuru nchi yangu, siyo zote zinafanya hivyo,” amesema.

Dk Biteko amempongeza kwa kuamua kuandika kitabu hicho akiwashirikisha Watanzania uzoefu wake katika kukabiliana na saratani, jambo ambalo wengi wasingependa kufanya.

Amesema kwa umaarufu wake, angeweza kuandika kitabu kwenye eneo lolote lile na watu wakanunua kwa kuwa ni maarufu, lakini amechagua kuisaidia jamii kwa kuandika kuhusu ugonjwa wa saratani.

“Nakupongeza sana Profesa Mwandosya kwa kuandika kitabu hiki. Ungeweza kuandika kuhusu katibu mkuu aliyekuja kuwa waziri, watu wangesoma. Ungeweza kuandika simulizi ya ndoa yenye mafanikio, watu wangesoma, lakini umeamua kuishirikisha jamii uzoefu huu, hongera sana,” amesema.

Amesema watu 45,000 wamekuwa wakigundulika kuwa na ugonjwa wa saratani duniani na umekuwa ukisababisha vifo vya watu 30,000 kila mwaka. Amebainisha saratani zinazoongoza nchini kuwa ni ya mlango wa kizazi, tezi dume, ya matiti, ya koo na utumbo mpana.

“Shajara hii ni darasa kwa kila mmoja wetu, umeamua kufanya maisha yako binafsi kuwa maisha ya umma, hongera sana,” amesema Dk Biteko.

Ameongeza kuwa: “Katika miaka 14 ya kishujaa ya Profesa Mwandosya, imetuonyesha kwamba ukiishi kwa kufuata masharti, unaweza kupona kabisa saratani.”

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Seif Shekalaghe amesema Serikali imeweka mpango wa Mtanzania yeyote atakayekosa huduma za matibabu ndani ya nchi (huduma zisizopatikana), atagharamiwa huduma hiyo nje ya nchi.

“Sasa uwekezaji mkubwa umefanyika kwenye vifaatiba, magonjwa mengi sasa yanatibika hapa. Namshukuru Profesa Mwandosya kwa kueleza hili,” amesema.

Mkuu wa Idara ya Haematolojia na Uhamishaji wa Damu kutoka Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi (Muhas), Dk Clara Chamba amesema kitabu cha Profesa Mwandosya kitakuwa msaada mkubwa kwa wanataaluma, wauguzi na wanafunzi kwa ujumla.

“Simulizi hii ya Profesa Mwandosya inawapa faraja wagonjwa wengine wanaopitia safari hiyo. Ameonyesha kila kitu ambacho amepitia, amewataja wote waliomtembelea na ametaja vyakula alivyokuwa anapenda kula hasa saa tisa za usiku,” amesema.