SIKU moja baada ya Singida Black Stars kuweka wazi, imefanya biashara ya kumuuza Josephat Bada kwenda JS Kabylie ya Algeria, habari njema kwa mashabiki wa timu hiyo ni kwamba mabosi wa timu hiyo wamefanya jambo moja la kuvuta mashine nyingine ya kuziba nafasi ya nyota huyo.
Bada ameitumikia Singidas kwa mkataba wa mwaka mmoja na kuipa mafanikio ambapo imepata nafasi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao na fasta mabosi wa Singida wakaamua kufanya jambo kwa kumzuia Khalid Aucho aliyeitumikia Ynaga kwa misimu minne kuondoka kwenda Israel ili atue kwa Wauza Alizeti hao.
Chanzo cha kuaminika kutoka Singida BS, kimeliambia Mwanaspoti kuwa, Aucho atakuwa mchezaji wa nne kutoka Yanga atakayeungana na kocha wa zamani wa timu hiyo, Miguel Gamondi baada ya Clatous Chama, Jonas Mkude na Nickson Kibabage pia kutua kikosini hapo.
“Biashara ya Bada ina manufaa kwa klabu, lakini tunawahakikishia kuwa nafasi yake inaletwa mchezaji bora na mzoefu wa ligi ya ndani na kimataifa tunaamini ni chaguo sahihi na ataisaidia timu yetu kufikia mafanikio,” alisema mtoa taarifa huyo na kuongeza:
“Mchezaji anayekuja ni pendekezo la kocha wetu na ameshawahi kufanya naye kazi anatambua ubora wake hilo tunaamini linaweza kuleta tija kikosini kwetu kama kocha alivyoagioza kufanya usajili kwa kuzingatia ubora na uzoefu.”
Mwanaspoti lilifanya jitihada ya kumtafuta Kocha Mkuu wa Singida, Miguel Gamondi ambaye alisema amefanya kazi ya wachezaji wengi bora na wenye uwezo mkubwa uwanjani, lakini kwake nyota saba kati yao walikuwa bora zaidi.
“Wachezaji ambao wapo katika ubora mkubwa ndani ya Yanga ni Mudathir Yahya, Maxi Nzengeli, Aucho, Ibrahim Hamad ‘Bacca’, Dickson Job na Clement Mzize ni miongoni mwa wachezaji ambao ningetamani kufanya nao kazi na wengine wengi hivyo ukiniambia ni nyota gani nimependekeza nifanye nao kazi Singida kutoka Yanga ni ngumu kuweka wazi,” alisema Gamondi na kuongeza:
“Soka ni mchezo wa wazi na kwa kuwa nataka kuwa na nyota wenye uzoefu na bora kikosini mwangu nafikiri muda ukifika kila kitu kitawekwa wazi na nitafanya kazi na yeyote ninachozingatia ni uzoefu na ubora hii ni kutokana na Singida kuwa miongoni mwa timu zitakazoiwakilisha Tanzania kimataifa nahitaji kuifikisha hatua nzuri.”
Awali Aucho ilielezwa alikuwa mbioni kumfuata swahiba wake, Kennedy Musonda anayecheza soka la kulipwa huko Israel na kutua kwake Singida kunaendelea kumfanya asalie katika Ligi Kuu Bara, lakini akikutana na Gamondi aliyefanya yake kazi misimu miwili iliyopita na kuipaisha Yanga kimataifa.