MABOSI wa Tabora United wamekamilisha usajili wa mabeki wawili kutoka visiwani Zanzibar tayari kwa ajili ya kuitumikia timu hiyo msimu ujao 2025-2026 na kuifanya klabu hiyo ya Ligi Kuu kufikia watano kwani awali ilishawanyakua viungo watatu.
Tabora imesajili beki wa kati kutoka Zimamoto, Mudathir NassorĀ Ally ‘Agrey 15’ na beki wa kulia kutoka Uhamiaji, Ally Juma Maarifa ‘Mabata’ na chanzo kutoka Zanzibar kiliiambia Mwanaspoti kuwa ni kweli wachezaji hao wamemalizana na timu hiyo na wameanza mipango ya kujiunga kwa pre season.
“Wawili hao ni wachezaji wazuri na uongozi wa Tabora United uliweka kambi huku kwa mechi za mwisho za ligi kabla haijamalizika na kuridhishwa na ubora wa wachezaji hao ndipo walipoamua kufanya mazungumzo na hatimaye kunasa saini zao,” alisema mtoa taarifa huyo na kuongeza;
“Mpira wetu unakuwa na unatazamwa sasa sio suala geni kuona wachezaji wanatoka Ligi ya Zanzibar na kwenda Bara tunawatakia vijana wetu upambanaji mwema waiwakilishe vyema ligi yetu na tunaamini kutoka kwao kutawavuta wachezaji wengine.”
Mtoa taarifa huyo aliongeza mbali na nyota hao kuna wachezaji wengine wapo kwenye mazungumzo na timu hiyo mambo yakienda vizuri pia atatoa taarifa zao na anaamini kila kitu kitaenda vizuri.
Wachezaji wengine kutoka Zenji wanaotajwa kunyakuliwa na Mashujaa ni viungo Haruna Shaaban Abdallah ‘Boban’ na Abdullatif Shauri “Camavinga’ wote wakitokeaZimamoto na Suleiman Juma Kidawa ‘Pogba’ ambaye awali alikuwa akitajwa na Simba, lakini akaibukia kwa maafande hao kutoka Kigoma.