Dar es Salaam. Upelelezi katika kesi ya mauaji inayomkabili Fred Chaula (56) na wenzake wawili, upo katika hatua za mwisho kukamilika.
Wakili wa Serikali, Tumaini Mafuru, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Jumanne, Julai 29, 2025, wakati kesi hiyo ilipotajwa.
Mbali na Fredy, washtakiwa wengine ni Bashir Chaula (49), dereva bodaboda na mkazi wa Tegeta, pamoja na Denis Mhwaga, mkazi wa Iringa.
Washtakiwa hao wanadaiwa kumuua mwanafamilia, Regina Chaula (62).
Wakili Mafuru ametoa taarifa hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Rahim Mushi, ambapo alidai upelelezi upo katika hatua za mwisho kukamilika, hivyo kutokana na hali hiyo, aliomba Mahakama iwapangie tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Baada ya kueleza hayo, wakili wa utetezi, Kung’e Wabeya, aliomba upande wa mashtaka ukamilishe upelelezi kwa wakati ili kesi hiyo iendelee na hatua nyingine.
Hakimu Mushi, baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote, ameahirisha kesi hiyo hadi Agosti 11, 2025, kwa ajili ya kutajwa.
Hata hivyo, kesi hiyo imesikilizwa kwa njia ya video, huku washtakiwa hao wakiwa rumande kutokana na shtaka la mauaji linalowakabili kutokuwa na dhamana.
Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Machi 12, 2025, na kusomewa kesi ya mauaji.
Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo Januari 18, 2025, eneo la Bahari Beach, Wilaya ya Kinondoni.
Inadaiwa kuwa siku hiyo ya tukio, washtakiwa kwa pamoja walimuua Regina Chaula, ambaye ni mwanafamilia wao, na kisha mwili wake kuutupa kwenye shimo la maji machafu lililopo katika nyumba ya Regina, wakati wakijua kuwa kufanya hivyo ni kosa kisheria.