Upepo wa Fei Toto umebadilika!

UPEPO umebadilika. Ndicho unachoweza kusema kutokana na sakata la usajili wa kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’.

Awali, Yanga ilikuwa ikitajwa na kuonekana kuwa karibu kumrejesha nyota huyo aliyemaliza Ligi Kuu msimu wa 2024-2025 kinara wa asisti akiwa nazo 13.

Dili la Yanga lilikuja siku chache baada ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini inayonolewa na kocha wa zamani wa mabingwa hao wa Tanzania, Nasreddine Nabi iliyomtaka ili kwenda kuitumikia Sauzi.

Hata hivyo, dau ililokuja nalo Kazier la Dola 350,000 badala ya 500,000 ilizotaka Azam lilifanya dili hilo kufa na Yanga kuelezwa imeenda hadi kuzungumza na mama mzazi wa mchezaji huyo kurejea kikosini kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Stephane Aziz Ki aliyeuzwa Wydad AC ya Morocco.

Dili la kutua Yanga lilikolezwa zaidi baada ya kudaiwa Fei Toto kwamba amegoma kuongeza mkataba mpya aliopewa na mabosi wa Azam ili kuendelea kusalia kikosini, ukiongezwa katika mkataba wa awali unaomalizika mwakani.

Lakini, hivi unavyosoma taarifa hii ni kwamba upepo unadaiwa kubadilika na lolote linaweza kutokea kwa Fei Toto kutua Msimbazi kutokana na kile kinachoendelea kwa sasa kwa vigogo walioamua kuingilia kati dili hilo ili nyota huyo avae uzi  mwekundu na mweupe.

Ipo hivi. Mwanaspoti limepenyezewa taarifa kwamba, vigogo wa juu wameamua kuingilia dili la Fei ili atue Msimbazi na pengine kabla ya timu kuondoka kwenda kambini nje ya nchi kila kitu kitakuwa kimekamilika.

Inaelezwa kuwa, kigogo mmoja wa taasisi moja nyeti (jina tunalo) ameamua kulivalia njuga suala la Fei ili kuhakikisha anatua Msimbazi kwa mkataba wa miaka miwili kwa kuununua mkataba uliosalia Azam na kilichobaki kimeachwa kwa Simba kumalizana na Fei kwa ishu ya dau la usajili na mshahara.

Taarifa za ndani ilizozipata Mwanaspoti zinadai kigogo huyo baada ya kutoa pesa ya usajili, makubaliano ilikuwa Fei Toto amalize mkataba wa mwaka mmoja uliosalia Azam, lakini Simba inaonekana inapambana ili awe sehemu ya kikosi msimu ujao.

“Simba inapambana Fei Toto ajiunge nao msimu ujao, lakini kocha wa Azam, Florent Ibengé anasisitiza mchezaji huyo amalizie mkataba kwanza ndipo aendelee na maisha mengine. Hapo ndipo pana mtihani mkubwa,” kilisema chanzo.

“Japo Azam ilikuwa inapambana kumuongezea mkataba ila imeshindikana, kwani mchezaji alihitaji kwenda kupata changamoto mpya, hivyo lolote linaweza likatokea baina ya Simba na Fei Toto.”

Chanzo hicho kilidai Fei Toto kasaini mkataba wa miaka miwili na pesa ya usajili anayotakiwa kuchukua kama mchezaji ni zaidi ya Sh700 milioni huku ukitajwa mshahara kuwa mkubwa.

“Kama nilivyosema mwanzo kwamba japo kigogo huyo kasimamia usajili, lakini mshahara utakuwa jukumu la viongozi na huenda akawa mzawa anayelipwa vizuri zaidi,” kilisema chanzo hicho.

Ndani ya misimu miwili mfululizo Fei Toto data zake zimekuwa kubwa 2023/24 akimaliza na mabao 19 na asisti saba na 2024/25 ni kinara wa asisti 13 na mabao manne, ikiwa na maana kwamba misimu miwili ya kuitumikia Azam katika Ligi Kuu amehusika na mabao 43, akifunga mabao 23 na asisti 20.

“Kwa hali iliyofikia ni ngumu kwa Azam kuendelea kumng’ang’ania Fei, licha ya kwamba ni kweli mabosi wa klabu hiyo wameombwa na kocha Florent Ibenge kwamba wahakikishe mchezaji huyo anabaki kikosini kwa hali yoyote,” kilisema chanzo hicho.

“Kuna mwanafamilia wa mmiliki wa timu akishirikiana na kigogo huyo wa taasisi nyeti ndio wanaojadili dili la Fei na bahati nzuri mchezaji mwenyewe ameshaonyesha nia ya kuondoka Azam kwa kuamua kugoma kusaini mkataba mpya tangu Oktoba mwaka jana.

“Kwa ishu ya hela inayotakiwa kulipwa Yanga kama sehemu ya kipengele cha mkataba wakati anaenda Azam ya Sh1 bilioni, hilo limemalizwa na kigogo huyo. Kilichobaki ni viongozi wa Simba kuwafuata wenzao ili kuzungumza kama utaratibu unavyotakiwa, lakini Fei na Simba lolote linaweza kutokea.”

Licha ya kwamba baadhi ya viongozi wa Azam wanakomaa kutotaka Fei Toto aachwe, lakini ushawishi uliofanywa na kigogo huyo wa serikali kukubali kutoa fedha hiyo kisha nyingine kumalizwa na vigogo wa Simba imeelezwa imefanya kazi iwe rahisi.

“Huenda Fei akavuta si chini ya Sh800 milioni za usajili na mshahara mnono zaidi ya ule anaolipwa Azam kwa sasa. Nadhani Jumatano ndio viongozi wa Simba wataenda kuzungumza na wenzao wa Azam, lakini hata mchezaji ni vile tu yupo kambi ya taifa, lakini angekuwa katika msafara wa Simba,” kilidai chanzo hicho.

“Huyu ndiye aliyewalainisha wachezaji wa Simba waliokuwa kwenye mgomo wa kudai posho zao na kutishia kutoicheza mechi ya Juni 25 (ya Dabi ya Kariakoo), lakini baada ya kuonana na mabosi na kuwapa fedha za kuwalipa wachezaji muda mchache kabla ya kuanza kwa pambano kuliokoa mengi,” chanzo hicho kilisema na kuongeza kuwa, tayari mabosi wa Azam wanajiandaa kuishi bila Fei Toto msimu ujao.