Utegemezi wa Akili Unde sasa janga kwa vijana

Dar es Salaam. Katika dunia ya sasa ambapo matumizi ya akili unde (AI) yameshika kasi, jamii imetahadharishwa kuwa kuna hatari ya kizazi kijacho kikawa na maarifa mengi, lakini kikakosa uwezo wa kuishi pamoja, kuelewana na kushirikiana kijamii.

Angalizo hilo  limekuja ikiwa ni matokeo ya kushuka kwa kiwango cha maingiliano ya ana kwa ana miongoni mwa vijana na watoto wanaoweza kufikia teknolojia hiyo wakitajwa kutumia programu za Chatbot kama mbadala wa mawasiliano  kati yao na wazazi, marafiki na wanajamii kwa ujumla.

Programu hizi zinazotumia akili unde kuzungumza au kujibu maswali ya watumiaji kwa njia ya maandishi au sauti zimekuwa kivutio kikubwa kwa vijana wakitumia kufanya shughuli mbalimbali ikiwemo kujifunza, tafiti, kupata ushauri wa kitaalamu, au hata kwa mawasiliano ya kawaida.

Miongoni mwa programu hizo ni ChatGPT, Siri, Google Assistant, Gemini, Meta AI, Replika, Alexa, Duolingo, Woebot na nyinginezo ambazo hujibu kila swali analouliza mtu iwe kwa maandishi au sauti.

 Wanasaikolojia  wameeleza kuwa licha ya kuwa chanzo cha kutafuta maarifa, kwa upande mwingine mwenendo huo ni janga lingine ambalo litaleta athari kubwa kwa jamii kwani kuna hatari ya kuwa na kizazi ambacho hakihitaji binadamu wengine kwa kuwa utegemezi wake utakuwa kwenye teknolojia.

Akili Unde  kwa sasa imejikita kwenye programu ambazo vijana hutumia kila siku na wengi wameifanya sehemu ya maisha yao, hata hivyo wataalamu wanaeleza kuwa kadri utegemezi huu unavyoongezeka, ndivyo pia hatari ya kutengana kijamii inavyoongezeka.

Dk Kanchan Shukla kupitia andiko lake lililochapishwa kwenye jarida la International Journal of Advances in Engineering and Management (IJAEM) amesema matumizi ya AI yamepunguza kwa kiasi kikubwa watu kuwasiliana na athari kubwa inaonekana kwa vijana.

Anasema kupitia Akili Unde wanaweza kujifunza bila kushirikiana na wanafunzi wenzao au walimu, jambo ambalo linapunguza fursa za kujifunza kijamii  hali inayoashiria mabadiliko makubwa katika mitazamo ya kijamii, mahusiano, na hata afya ya akili.

Katika chapisho hilo lenye kichwa cha habari Impact of Artificial Intelligence of Youths, Dk Shulka amesema programu kama chatbots zinazojifanya kuwa marafiki zinapunguza motisha ya kutafuta uhusiano wa kweli wa kibinadamu.

Pia video, muziki, na michezo vinavyopendekezwa na Akili Unde huwafanya vijana kutumia muda mwingi wakiwa pekee, wakikosa kushiriki katika shughuli halisi za kijamii.

“Mambo haya husababisha vijana kuwa wapweke, huku wakihisi kutosheka na mazungumzo ya kidijitali pekee kitu ambacho si sahihi. Ujana ni kipindi muhimu kwa mtu kujifunza hisia, huruma, na ustadi wa mawasiliano.

“Stadi hizi hujengwa kupitia mawasiliano ya ana kwa ana kusoma hisia za watu, kuelewa lafudhi, na kushughulikia changamoto za mahusiano ya kibinadamu. AI haiwezi kufundisha mambo haya kikamilifu kwa sababu haina hisia wala uelewa wa kweli wa hali ya kibinadamu,”amesema Dk Shulka na kuongeza

“AI haileti changamoto za kweli kama binadamu anavyoweza kufanya. Haitokosea, haitapingana, wala haitahitaji msamaha, hivi ni vipengele muhimu katika kukuza uhusiano na ukomavu wa kijamii”.

Mwanasaikolojia David Rweyemamu anasema programu za Akili Unde zinaweza kuonekana kama marafiki wa kweli, lakini kwa uhalisia ni kwamba zinaendeshwa  mifumo ya kimtambo isiyokuwa na hisia.

“Hii hujenga hali ya uhusiano wa uongo, ambapo kijana anaweza kuhisi yupo na mtu ilhali yupo na mashine. Hali hii inaweza kuwafanya vijana kuwa na ugumu kuanzisha na kudumisha uhusiano wa kweli na wenzao”.

Kwanini AI imekuwa kimbilio

Wengi wa vijana huona ni   suluhisho la haraka na rafiki wa karibu katika mazingira ya kidijitali wakifurahishwa na uwezo wake wa  kutoa msaada wa papo kwa hapo na upatikanaji wa taarifa mbalimbali bila gharama kubwa.

“Mimi napenda kutumia chatbot kama ChatGPT kunisaidia na maswali ya masomo. Inanielezea kwa njia rahisi ambayo siipati hata darasani wakati mwingine,” anasema Neema, mwanafunzi wa shule moja ya sekondari jijini Dar es Salaam.

Akifafanua kuhusu hilo kwa mtazamo wa kisaikolojia, Rweyemamu anaeleza kuwa programu hizo zimekuwa kimbilio kwa vijana kwa sababu wengi kwa sasa wanakosa watu wa kuwaelezea mambo wanayokutana nayo hivyo kujikuta wakitafuta ushauri kupitia teknolojia.

Sababu nyingine anayoitaja ni woga wa kuhukumiwa, akieleza kuwa Akili Unde haitoi hukumu wala kushtumu tofauti na wafanyavyo binadamu badala yake inasikilzia na kujibu kwa subira na ustahimilivu wa hali ya juu.

Hili linathibitishwa na mzazi ambaye hakutaka jina lake linukuliwe, mama huyu ambaye yuko mbali na mtoto wake anasema ameshaanza kuona athari ya matumizi ya Akili Unde kwa kijana wake huyo umri wa miaka 13.

“Mtoto wangu ana simu ya mkononi sasa kuna kitu nilimzuia kutumia, alichofanya ni kwenda kwenye simu yake na kuanza kuchati na AI akiiuliza maswali mbalimbali kuhusu uamuzi niliochukua na namna anavyonichukulia na kile anachoona ni sahihi kwake.

“Baada ya majadiliano hayo na AI akascreenshot na kumtumia baba yake akimueleza kwamba anaona amekuwa na mazungumzo mazuri na AI kuliko mama yake, kwahiyo ameona huko anaeleweka zaidi,” anasimulia mama huyo.

Mwanasaikolojia anasema wakati mwingine vijana wanakimbilia kwenye matumizi ya teknolojia kupata majibu ya maswali yao kwa kwa sababu ya faragha.

Anasema “Kupitia AI kijana anaweza kuuliza swali lolote na akapata majibu bila mtu mwingine kujua, halafu pia huku kwenye teknolojia majibu yanayolewa kwa haraka haina kupanga vikao,”

Zipi hasara za utegemezi huu wa AI

Rweyamemu anasema mbali na kupunguza mwingiliano wa watu matumizi kupita kiasi ya Akili Unde husababisha ubongo wa mtumiaji kutofanya kazi inavyostahili

“Wakati mwingine vijana huanza kutegemea sana chatbot hata kwa mambo madogo ambayo wangeyatatua wao wenyewe. Hii inaweza kudumaza uwezo wa kufikiri kwa kina na kujitegemea.

“Halafu pia si mara zote utapata  taarifa sahihi. Vijana wanaweza kupokea habari zisizo sahihi au zenye upendeleo, hasa kama hawajui jinsi ya kuchambua vyanzo vya taarifa au kuhoji uhalali wake”anasema.

Ushauri kwa wazazi,walezi na jamii

Mshauri wa masuala ya malezi Magdalena Mbinga anasema Akili Unde ni zana muhimu ya kiteknolojia ambayo inaweza kuboresha maisha ya binadamu, lakini haipaswi kuchukua nafasi ya mawasiliano ya ana kwa ana ambayo ni  muhimu kwa ajili ya ukuaji wa kihisia, kiakili na kijamii.

Kwa sababu hiyo anasema ipo haja kwa vijana kuhamasishwa kushiriki katika michezo, vikundi na shughuli nyingine za kijamii zitakazowaunganisha na wengine.

Pia wafundishwe kutambua mipaka ya AI na kuelewa kuwa si mbadala wa uhusiano wa binadamu sambamba na kufundishwa kudhibiti matumizi ya muda mrefu wa skrini na kuwahimiza kushiriki shughuli halisi.

Mshauri huyo anasema jamii inataka kupunguza utegemezi huu, ni lazima ijenge mazingira ambapo vijana watahisi kusikilizwa, kueleweka, na kukubaliwa  bila kulazimika kugeukia AI kama rafiki wa dharura.

“Vijana hawakimbilii chatbot kwa sababu ni mtindo wa maisha, bali ni dalili kuwa mahitaji yao hayajafikiwa kikamilifu na watu wa karibu. Wazazi, walimu, viongozi wa dini na jamii kwa ujumla wanapaswa kujifunza kusikiliza zaidi, kuhukumu kidogo, na kutoa nafasi salama ya mazungumzo.

Akili Unde si adui wa maendeleo ya kijamii, hata hivyo, jamii inapaswa kuchukua hatua kuhakikisha kwamba vijana hawawi watumwa wa mashine, bali wanaendelea kukuza uhusiano na bindamu wengine Teknolojia inapaswa kuwa msaidizi, si mbadala wa hisia na ukaribu wa kweli”.