Viongozi Simba, Yanga wawekwa kando uteuzi CCM

Rais wa Yanga, Hersi Said pamoja na mwenyekiti wa Simba Murtaza Mangungu ni kati ya watia nia ambao wamewekwa kando kugombea nafasi ya ubunge.

Mangungu alikuwa ameomba kugombea kupitia Jimbo la Kilwa, huku Hersi akiomba kupitia jimbo la Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Wakati hawa wakiwekwa kando Makamu wa Rais wa zamani wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Michael Richard Wambura amepenya hatua inayofuata.

Hayo yamesemwa jana Julai 29, 2025 na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla, wakati akitangaza majina ya walioteuliwa na CCM kwenda hatua inayofuata ya kura za maoni za kuwania kugombea ubunge kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.

Magungu ambaye ni mbunge za zamani, aliomba ridhaa hiyo kupitia Jimbo la Kilwa Mkoani Lindi, huku Wambura jina lake likipenya kupitia Jimbo la Kinondoni akiwa pamoja na aliyekuwa mwenyekiti wa zamani wa Yanga, Abass Tarimba ambaye alikuwa mbunge kipindi kilichopita.

Mbali na hao, mchambuzi wa soka ambaye pia ni mwanasoka wa zamani Jemedari Said naye amefanikiwa kupenya kwenye hatua inayofuatia akiwa anawania kupitia Jimbo la Mtama ambalo mbunge wake anayetetea kiti hicho Nape Mnauye ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo naye amepita kwenda hatua inayofuata.

Pia Ofisa Habari wa Azam FC, Hashim Ibwe naye amefanikiwa kupenya kwenye hatua inayofuata kupitia Jimbo la Mwanga mkoani Kilimanjaro.

Wanamichezo wengine waliopita ni aliyekuwa Ofisa Habari wa zamani wa Simba, Juma Nkamia, Ofisa Habari wa zamani wa Yanga, Jerry Muro mwanamuziki Clayton Revocatus Chipando ‘Baba Levo’ na Mchambuzi wa Soka, Shafii Dauda.