Mbeya. Viongozi wa dini na machifu mkoani Mbeya wamekemea vikali lugha za kejeli dhidi ya Serikali kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025, huku wakisisitiza umuhimu wa kudumisha amani na mshikamano miongoni mwa wanajamii.
Kauli hizo zilitolewa leo Jumanne, Julai 29, 2025, katika kongamano maalumu la kufanya maombi kwa ajili ya kuliombea Taifa na Rais Samia Suluhu Hassan, kuelekea uchaguzi huo.
Kongamano hilo limeandaliwa na Jumuiya ya Maridhiano Mkoa wa Mbeya, likihusisha viongozi kutoka madhehebu mbalimbali ya dini, ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Solomon Itunda, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa, Beno Malisa.
Akifungua kongamano hilo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano, Profesa Donald Mwanjoka amesema lengo kuu ni kuiombea nchi na Rais Samia, ili aendelee kulindwa na kupewa hekima katika kipindi hiki nyeti cha kuelekea uchaguzi.
“Nchi ya Tanzania italindwa na maombi kutoka kila kona, sala na dua zetu zitamfikia Mungu ambaye atashughulika na wale wote wanaopanga au kuthubutu kuharibu amani ya nchi kuelekea Uchaguzi Mkuu,” amesema Profesa Mwanjoka.
“Ni wakati wetu sasa kusimama pamoja, kuombea amani ya Taifa letu na kumwombea Rais wetu. Kwa kutambua juhudi zake, tutamkabidhi tuzo ya heshima kama alama ya kuthamini mchango wake katika kuimarisha nchi,” alieleza.
Kwa upande wake, Sheikh Ismail Abdallah, aliyemwakilisha Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, alisema maombi hayo yanalenga kuilinda nchi dhidi ya machafuko ambayo yanaweza kutokea kipindi hiki cha uchaguzi.
“Tunaendelea kuliombea Taifa letu na Rais wetu, lakini pia tunakemea vikali wale wote wenye nia ovu ya kuvuruga amani iliyojengwa kwa misingi ya maelewano na upendo tangu enzi za Mwalimu Julius Nyerere,” alisema.
Mchungaji Erica Mwakyolile wa Kanisa la Pentekoste Ushirika wa Shilo, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati Kuu Tendaji ya Jukwaa la Wakristo Mkoa wa Mbeya, amesema;
“Kila siku tunamlilia Mungu kwa ajili ya Taifa letu na Rais wetu. Tumtie moyo, ajue kuwa Tanzania ina amani na sisi kama viongozi wa dini tutaendelea kuililia nchi mbele za Mungu.
Chifu wa Mkoa wa Mbeya, Rocket Mwansinga, amebainisha kuwa wao wameamua kujitenga na kwenda kufanya maombi porini kwa ajili ya kulinda amani na kuwakemea wale wanaoitumia mitandao ya kijamii kuikejeli Serikali kupitia picha za video zisizofaa.
Akihitimisha kongamano hilo, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Solomon Itunda, ameipongeza Jumuiya ya Maridhiano kwa kuandaa tukio hilo lenye tija kwa Taifa, na kupongeza uamuzi wa kutoa tuzo ya heshima kwa Rais Samia na aliyekuwa Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson.
“Wengine waliotunukiwa tuzo ya heshima ni aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera, Mkuu wa Mkoa wa sasa, Beno Malisa; pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM mkoani humo, Patrick Mwalunenge.