Morogoro: Wafanyakazi wa majumbani wameiomba Serikali kukamilisha mchakato wa kuridhia na kupitisha mkataba wa kazi zenye staha kwa wafanyakazi wa majumbani, ili kuwezesha upatikanaji wa haki zao za msingi, kutambua haki, stahiki na sheria zinazohusu haki na wajibu wao.
Mmoja wa wafanyakazi hao, Desdelia Saimon, amesema kuchelewa kuridhiwa kwa mkataba huo kumeendelea kuwafanya wafanye kazi katika mazingira hatarishi, ikiwa ni pamoja na kukosa haki ya faragha, maisha binafsi na kinga ya kutosha ya kisheria.
Naye Nasra Seleman, mfanyakazi mwingine wa majumbani, amesema endapo mkataba huo utaridhiwa, utawasaidia kwa kiasi kikubwa, kwani unalenga moja kwa moja masilahi ya kundi hilo.
“Tunamuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuridhia mkataba huu ili na sisi tutendewe haki kama wafanyakazi wengine,” amesema Nasra Seleman kutoka Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Wafanyakazi wa Majumbani Tanzania, Zanini Athuman amesema mkataba huo unaweka wazi stahiki halali za wafanyakazi wa majumbani, zikiwemo mapumziko ya kutosha na kuishi katika mazingira ya heshima, hasa kwa wale wanaoishi na waajiri wao.
Amesema licha ya kuwepo kwa sheria mbalimbali hapa nchini zinazolitambua kundi hilo, utekelezaji wake bado ni mgumu kutokana na sheria kutoruhusu nyumba ya mtu binafsi kuwa ofisi ya kazi na mwarobaini pekee unaotarajiwa ni kuridhiwa kwa mkataba huo.
Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Majumbani, Mahoteli, Huduma za Kijamii na Ushauri (Chodawu), Said Wamba amesisitiza umuhimu wa wafanyakazi wa majumbani kujiunga na vyama vya wafanyakazi ili kuwa na sauti ya pamoja katika kudai haki na stahiki zao.
“Tunajaribu kuwainua hawa wafanyakazi wa majumbani. Wapo chini mno, na hili si jukumu la Chodawu pekee, bali ni la jamii nzima ya Watanzania. Wanafanya kazi kubwa na muhimu kwa waajiri wao na kwa taifa kwa ujumla, lakini hawapati matunda ya jasho lao,” amesema Wamba.
Ili kuhakikisha haki za wafanyakazi hao zinalindwa ipasavyo, shirika hilo limewakutanisha mkoani Morogoro katika kikao kazi cha siku mbili Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), taasisi ya Serikali inayohusika na utatuzi wa migogoro ya kazi Tanzania Bara, pamoja na wawakilishi wa wafanyakazi wa majumbani.
Lengo la kikao hicho ni kutafuta mwarobaini wa pamoja wa changamoto zinazolikumba kundi hilo muhimu katika jamii na taifa.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, Mratibu wa Mradi wa ILO wa kuboresha utambuzi na mazingira ya kazi kwa wafanyakazi wa majumbani, Chiku Semfuko, amesema mafunzo hayo yatawasaidia wafanyakazi wa majumbani kutambua mahali sahihi pa kupeleka migogoro yao na kupata utatuzi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa CMA Tanzania Bara, Usekelege Mpulla amesema tume imeandaa mwongozo maalumu wa utatuzi wa migogoro ya wafanyakazi wa majumbani, kwa lengo la kutafsiri vizuri mchakato wa migogoro na kutekeleza matakwa ya kisheria pamoja na kuridhia mkataba huo Na. 189.
“Tumejipanga kuhakikisha haki za wafanyakazi wa majumbani zinatolewa kwa wakati. Mafunzo haya yakikamilika, tunaamini wasuluhishi wa migogoro watakuwa na uwezo wa kumaliza migogoro kwa haraka,” amesema Mpulla.
Awali, Kamishna Msaidizi wa Idara ya Kazi – Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Rehema Moyo ambaye alikuwa mgeni rasmi, amesisitiza kuwa CMA ipewe kipaumbele katika kushughulikia migogoro ya wafanyakazi wa majumbani kutokana na ugumu wa mazingira wanayokumbana nayo ili kupata stahiki zao.
“Ni muhimu pia wafanyakazi wa majumbani wenyewe wajue haki zao. Pamoja na kuwepo kwa vyombo vya kisheria, lazima wapewe elimu ya kutambua ni wapi waende kupata utatuzi wa migogoro yao,” amesema Rehema Moyo.