WATAALAMU WASISITIZA MATUMIZI SAHIHI YA AI

Mkurugenzi
Mkuu wa Tume ya Taifa ya TEHAMA Dkt Nkunde Mwasaga (kushoto),akiwa Dkt George
Mulamula (katikati) pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Datavera Bilal Hmede katika
siku ya pili ya Jukwaa la Akili Unde la Tanzania 2025 ambalo limefanyika
kuanzia Julai 28-29 mwaka huu jijini Dar es salaam

………………….

NA MUSSA KHALID

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya TEHAMA Dkt
Nkunde Mwasaga amewasisitiza watanzania hasa vijana kutumia fursa ya uwepo wa
Akili Unde kwa kutegeneza bunifu mbalimbali zitakazosaidia nchi kuwa shindani
kiuchumi.

Dkt Mwasaga ameeleza hayo leo jijini Dar es salaam
wakati akziungumza na waandishi wa habari katika siku ya pili ya Jukwaa la
Akili Unde la Tanzania 2025 ambalo limewakutanisha wadau kutoka mataifa
mbalimbali.

Aidha Dkt Mwasaga amesema kuwa kutokana na Akili
Unde kuwa na uwezo wa kutoa maamuzi hivyo wamejadili kuhusiana na maadili ili kujenga
kizazi kilichobora ambacho kitatumia mfumo huo kwa faida.

‘Tunaangalia maadili katika Akili Unde kwa sababu
saa hivi inakuwa na uwezo fulani kwa ajili ya kutoa maamuzi yenyewe na kama
inaweza wote tunafahamu masuala ya maadili ni ya msingi hivyo hii mifumo tujue
kwamba inafanya kwa kuangalia tamaduni zetu,mila zetu na kufata sheria zetu za
Tanzania”amesema Dkt Mwasaga

Akizungumza katika Jukwaa hilo,Jaji wa Mahakama Kuu
Tanzania na Jaji Mfawidhi wa Mahakama kuu kanda ya Tabora Dkt Adam Mambi
amesema matumizi ya Akili Unde yamekuwa yakirahisisha katika utendaji wa haki
kwenye mahakama za Tanzania.

Amesema
kuwa takriban Mahakama 11 za Mahakama kuu za Tanzania wameweza kuweza kuweka
mfumo wa Akili Unde ambao unaweza kurikodi wakati shahidi au mwanasheria
anaongea halafu baadae sauti inaweza kugenuzwa kuwa kama maneno.

Jukwaa
hilo ambalo limeanza Jana na kuhitimishwa leo limewaleta pamoja wataalamu wa
teknolojia, watunga sera, wawakilishi wa sekta binafsi, na wadau wa maendeleo
kwa lengo la kujadili mwelekeo wa AI nchini Tanzania ambapo umelenga kuweka
msingi wa sera jumuishi na endelevu zitakazoiwezesha Tanzania kuongoza katika
matumizi salama na jumuishi ya teknolojia ya Akili Bandia barani Afrika.