Unguja. Wakati mashindano ya Michuano ya Mataifa ya Afrika (CHAN) yakitarajiwa kuanza Agosti 2, 2025 katika viwanja mbalimbali, mamlaka husika Zanzibar zimeeleza namna zilivyojipanga katika utoaji wa huduma za afya, usalama, na mapokezi ya mashindano hayo, huku zikitaja hoteli kufurika kutokana na tukio hilo muhimu.
Kwa Zanzibar, Uwanja wa Amaan Complex Stadium utatumika kwa ajili ya timu nne ambazo zinatarajiwa kuanza Agosti 5, 2025.
Timu hizo ambazo zipo katika Kundi D ni pamoja na bingwa mtetezi wa Kombe la CHAN, Senegal, Nigeria ambaye ni bingwa wa kihistoria katika mashindano hayo, Congo na Sudan.
Mkurugenzi Masoko, Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Rahma Sanya amesema mashindano hayo ni fursa kubwa katika sekta ya utalii, na kamisheni imejipanga kuhakikisha fursa hiyo inanufaisha Taifa, kuongeza idadi ya watalii na kuzidi kuitangaza Zanzibar katika anga za kimataifa.

Mkurugenzi wa Masoko Kamisheni ya Utalii, Rahma Sanya akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya Utalii na mapokezi ya wageni katika michuano ya CHAN
“Kwa sisi katika sekta ya utalii, hii ni fursa kubwa haijawahi kutokea kwa sababu nchi yetu itazidi kujitangaza. Maana tunategemea wageni wengi wa ndani na nje ya nchi kutoka mataifa mbalimbali kuja kuangalia mechi hizi,” amesema.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, hoteli zimesheheni wageni watakaoingia, si tu kwa ajili ya kucheza, bali wanaokuja kushuhudia mpira ukichezwa.
Amewasihi wananchi, wafanyabiashara na wajasiriamali kuchangamkia fursa hiyo adhimu, hivyo ni muda wa kujitangaza kwa vitu tulivyonavyo katika kisiwa hiki.
“Mpaka sasa, kwa taarifa tulizopata, hoteli zimejaa. Wageni ni wengi kwa sababu kuna timu na wageni ambao wamekuja kwa ajili ya shughuli hii. Kwa hiyo tunaishukuru Serikali kwa kuboresha mazingira kuhakikisha michezo kama hii inafanyika hapa nchini,” amesema.
Amesema kamisheni imejipanga tangu waliposikia CHAN itachezwa Zanzibar na kuhakikisha hoteli zote kwa upande wa usalama na huduma zipo vizuri, hivyo wanawahakikishia wageni wote hakuna atakayeingia akapata changamoto kwani mazingira yameandaliwa vizuri na ya kutosha.
Hata hivyo, pamoja na wingi wa wageni, amesema kuna fursa za nyumba ambazo si hoteli lakini zimesajiliwa kwa ajili ya kulaza wageni, hivyo katika malazi na makazi, wapo vizuri na hakuna atakayekwenda katika kisiwa hicho akakosa sehemu ya kulala.
Wakati Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi anaingia madarakani, alihamasisha kuongeza vivutio vya utalii, mojawapo kikiwa ni utalii wa michezo na afya ambavyo sasa vimeanza kuzaa matunda kutokana na kuimarisha miundombinu yake kwa kiwango cha kimataifa.
Kutokana na uhamasishaji unaoendelea na kuwapo kwa michuano hiyo ya CHAN, mkurugenzi huyo amesema kwa mwaka huu wanategemea kuvunja rekodi ya wageni watakaotembelea Zanzibar kutoka wageni laki sita hadi wageni laki nane.
Daktari Bingwa wa Mifupa na Ajali, Hospitali ya Mkoa wa Mjini Magharibi Lumumba, Abdumajid Hussein Said amesema kuelekea mashindano hayo wamejipanga kutoa matibabu iwapo zikitokea majeraha.

Hospitali ya Mkoa Mjini Magharibi, Lumumba ambayo imechaguliwa na CAF itakayotumika kwa ajili ya kutoa matibabu kwa wachezaji watakaopata majeraha na wageni katika mashindano ya michuano ya CHAN Zanzibar
Itakumbukwa CAF wameichagua hospitali hiyo kuwa ndiyo itakayotumika kutoa huduma za afya kwa wageni watakaopata majeraha au majanga ambayo yatajitokeza.
“Tumejiandaa vema kuzipokea timu, kuhakikisha usalama wote wa kiafya na majanga mengine yanyoaweza kutokea vyote kuvishughulikia kwa hali ya juu. Kwa hiyo tunawathibitishia kwamba usalama upo, tumejiandaa kupitia kamati mbalimbali ambazo zitahusika na majanga ndani na nje ya uwanja,” amesema.
“Hii ni pamoja na mashabiki, wachezaji, afya ya akili, magonjwa ya mlipuko ikiwa yatatokea sisi tupo vizuri sana,” amesema.
Amesema mpaka Zanzibar ifikie hatua ya kuendesha mashindano hayo makubwa ni kutokana na miundombinu bora iliyotengenezwa na Rais Mwinyi, ikiwemo kujenga kiwanja cha mpira na miundombinu ya hospitali za kisasa zikiwa na wataalamu.
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Tabia Maulid Mwita amesema kuna marekebisho madogo waliyoambiwa na Shirikisho la Mpira Afrika (CAF) yamefanyiwa kazi na wapo katika hatua za mwisho za ukamilishaji wake.
“Tulitakiwa mabenchi ya kiufundi ya timu yachimbwe chini ili kuwapa fursa watazamaji kuona mpira ukichezwa wote. Kwa sababu mwanzo yalivyokuwa watu walikuwa hawawezi kuona. Tumelitekeleza hilo na mkandarasi wetu anaendelea kumalizia,” amesema.

Waziri wa Habari, Vijana, Michezo na Utamaduni, Tabia Maulid Mwita akizungumza kuhusu maandalizi ya CHAN
Kwa upande wa kamera (CCTV), licha ya zilizokuwapo awali, lakini CAF walitaka ziongezwe kwani zilizokuwapo zilionekana hazina uwezo mkubwa na chache, ambapo zimeongezwa zaidi ya kamera 42 ambazo zimefungwa ndani na kwenye mageti ya kuingilia uwanjani kwa ajili ya kunasa kila kitu kitakachoingia.
“Pia tuliambiwa kuweka majukwaa ya ziada (VIP extra) kwa ajili ya CAF na kuweka majukwaa mengine kwa ajili ya viongozi wengine, utalii na biashara. Haya yatakuwa kwa muda katika matumizi ya aina tatu tofauti,” amesema.
Amesema maandalizi ya CHAN yamefikia asilimia 90, kwani mahitaji yote yaliyotakiwa na CAF yameshafanyiwa kazi na wameridhishwa na maandalizi hayo.
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF), Suleiman Mahmoud Jabir amesema hatua hiyo si tu kufanya marekebisho ya uwanja, bali kuweka hadhi ya viwango vya kimataifa vinavyokubalika. Kwa hiyo katika hilo lazima kutoa shukrani nyingi kwa viongozi waliofanikisha jambo hilo.
“Viongozi wetu wamefanya mambo mengi mazuri katika miundombinu ya michezo. Hakika zinatia moyo na kufurahisha. Tunaona makubwa yaliyofanywa. Tulianza na matengenezo ya uwanja huu wa Amaan, sasa yamefanyiwa marekebisho kuanza kupata mashindano ya kimataifa,” amesema.
Amesema New Amaan Complex kimekuwa kivutio kikubwa si kwa nchi wanachama wa Cecafa bali pia kwa nchi wanachama wa Shirikisho la Soka Afrika.
Jabir, ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Maandalizi na Makamu Mwenyekiti wa Huduma za Timu, amesema uwanja huo mbali na timu hizo nne, utatumika kwa timu ambazo kundi zitazotoka Dar es Salaam, kisha kuna mechi moja ya robo fainali ambayo nayo itachezwa Zanzibar.
“Hizi ni rehema kuu Zanzibar kufikia katika hatua hii ni moja ya kuitangaza Zanzibar, na haya ni mambo makubwa. Tupo katika hatua nzuri ya neema kubwa,” amesema.
Kuhusu usafiri, tayari amesema kila kitu kimeandaliwa na kipo sawa, ukiwemo usafiri wa ndani kwa ajili ya kuwasafirisha wachezaji ambapo zimeandaliwa Costa nane kwa ajili ya kuwapeleka uwanjani na kuwarejesha hotelini, yote yakiwa na rangi moja ya njano ambayo ndiyo alama inayotumiwa na CHAN.
Amewahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi katika uwanja huo kuangalia mechi hizo ambapo vimewekwa viingilio vidogo: daraja la tatu Sh1,000, daraja la pili Sh2,000 na daraja la kwanza Sh5,000.
“Wazanzibari tunataka nini? Hizi ndiyo neema tunazotaka. Sasa zimetufikia. Kwa hiyo tujitokeze kwa wingi katika uwanja huu kwa mujibu wa ratiba ili kushuhudia michuano hii,” amesema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Richard Mchomvu, licha ya kueleza bado wapo kwenye vikao vya mwisho na wadau muhimu katika michuano hiyo, kuhusu hali ya usalama wamejipanga kuhakikisha unadumishwa kwa siku zote za wageni hao watakapokuwa Zanzibar.