Asilimia 86 ya watoto ‘huachishwa ziwa’ wakiwa na miezi 15, athari zatajwa 

Dar es Salaam. Wizara ya Afya imesema asilimia 86 ya watoto wote nchini, huachishwa kunyonya miezi 15 baada ya kuzaliwa, sawa na umri wa mwaka mmoja na miezi mitatu, suala ambalo husababisha athari kwa mtoto hapo baadaye.

Imesema takwimu zinaonyesha ni asilimia 35 pekee ya watoto wote nchini hunyonyeshwa kwa kipindi chote cha miaka miwili.

Kutonyonyesha mtoto kwa usahihi kumetajwa kuchangia tatizo la ukondefu, udumavu, utapiamlo na ukuaji duni wa mwili na ubongo wa mtoto.

Hayo yamebainishwa leo Jumatano, Julai 30, 2025 na Ofisa Lishe kutoka Wizara ya Afya, Elieth Rumanyika wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya Wiki ya Unyonyeshaji Kitaifa, inayoanza Agosti mosi, 2025, ulioenda sambamba na uzinduzi wa Mwongozo wa Kitaifa wa kuzuia na kutibu ukondefu na uvimbe unaotokana na ukondefu kwa watoto walio na umri chini ya miaka mitano.

Amesema mtoto anatakiwa kuendelea kunyonya maziwa ya mama mpaka anapofikisha umri wa miaka miwili.

“Hapa ndiyo pana changamoto kidogo, kinamama wengi wananyonyesha watoto wao mpaka miezi 15, wanahisi amekua wanaacha kunyonyesha,” amesema.

Ametaja sababu mbalimbali kuwa wengine husema mtoto anakataa kula anataka kunyonya muda wote na hiyo inasababisha kinamama wengi kukatisha kuwanyonyesha wakiwa na mwaka mmoja na miezi mitatu.

 “Huu ndiyo wakati ambao watoto wanakumbwa na utapiamlo na ukondefu, kwa sababu wanaachishwa kunyonyeshwa maziwa ya mama yenye virurubisho muhimu, wanaanza kupewa vyakula vingine ambavyo ulishaji wake hauzingatii usahihi wa lishe na kutofikia kula chakula kilichokidhi mahitaji,” amesema.

 “Mtoto asiponyonya kwa usahihi inaweza kuathiri ukuaji wake wa ubongo, atapata upungufu wa virurubisho muhimu mwilini ambavyo kusaidia ukuaji, itaathiri afya na Serikali itatumia fedha nyingi kuwekeza kwenye afya.

Akizindua wiki ya unyonyeshaji na mwongozo huo, Naibu Katibu Mkuu Tamisemi anayeshughulikia afya, Profesa Tumaini Nagu, amesema tafiti nyingi zilionyesha unyonyeshaji wa maziwa ya mama ni afua inayoongoza katika kupunguza vifo vya watoto duniani.

“Nawaasa wanajamii, hasa wanaume, kuwapa muda wa kupumzika wanawake walioajiriwa katika sekta isiyo rasmi, sekta binafsi na wanaofanya kazi za kilimo na shughuli nyingine za kiuchumi, ili kuwapunguzia kazi zinazowakabili katika familia na hivyo, kuwawezesha kupata muda wa kuwanyonyesha kikamilifu watoto wao,” amesisitiza.

Profesa Nagu amesema uzinduzi huo uwe chachu ya kuanzisha sura mpya katika utekelezaji wa programu za lishe nchini. 

Amesema jitihada za kulinda, kuhimiza na kuendeleza ziende sambamba na utekelezaji wa kitaifa wa kuzuia na kutibu ukondefu, ili kuboresha afua za utambuzi wa mapema na matibabu sahihi ya ukondefu ili kupunguza madhara na vifo.

Amesema nchini Tanzania, kiwango cha ukondefu kwa watoto chini ya miaka mitano kimepungua na kufikia asilimia 3, kiwango sawa na watoto 620,000 wenye ukondefu kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022.

Profesa Nagu amesema Serikali imeiboresha Sheria ya Ajira ya Uhusiano Kazini ya mwaka 2004 na kanuni zake za 2017, hususan kifungu cha 33 cha sheria mama, kinachohusu likizo ya uzazi na mapumziko ya kunyonyesha.

Amesema sheria hiyo inatoa haki kwa wanawake waliojifungua watoto kupata likizo ya uzazi siku 84 au 100 endapo mama atazaa watoto pacha, lakini pia atarudi na kupatiwa saa 2 za kunyonyesha.

“Mwaka 2025 maboresho yamefanyika kwa kuwaongezea likizo ya uzazi wanawake wanaojifungua watoto njiti hadi kufikia wiki 40 kwa kuzingatia muda wa ujauzito kamili,” amesema.

Amesema sheria hiyo inawalinda wanawake walio katika sekta ya ajira ili wasipoteze ajira na vipato vyao kutokana na wajibu wao wa kibaolojia wa kuzaa. 

Profesa Nagu amesema takwimu zinaonyesha kuwa viwango vya unyonyeshaji wa watoto nchini Tanzania vimeendelea kuimarika ambapo, asilimia ya watoto wanaonyonyeshwa maziwa ya mama pekee imeongezeka kutoka asilimia 58 mwaka 2018 hadi asilimia 64 mwaka 2022.

Mkurugenzi Mkazi wa Action Against Hunger, Zacharia Imeje amesema mwongozo huo utasaidia kuwaongoza wahudumu wa afya watakaokuwa wakitoa huduma kwa watoto wenye utapiamlo na pia kuhakikisha Taifa linaweza kushughulikia mahitaji ya watoto hao kwa njia nzuri.