Dar es Salaam. Watu wanane, wakiwemo maofisa watano wa Jeshi la Polisi nchini, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka 16 ya kughushi vibali vya kumiliki silaha.
Maofisa hao ni Mkaguzi wa Polisi mwenye namba PF. 19931 Fredrick Malekela (45), mkazi wa Kilwa Road; E.4627 Sajenti Kalemwa Kaunga (54), mkazi wa Chanika; E.7855 Sajenti Edger Mlogo (54), mkazi wa Kibamba; F.1126 Sajenti Robert Titus (47), mkazi wa Kisarawe na F.5092 Sajenti John Kaposwe (46), mkazi wa Kurasini.
Wengine ambao si maofisa wa jeshi hilo ni Damson Mnyilenga (59), mkulima na mkazi wa Chanika; Simon Aloyce (60), mfanyabiashara na mkazi wa Mwanza pamoja na Venrand Liberio (29), mfanyabiashara na mkazi wa Tataba.
Washtakiwa hao wamefikishwa mahakamani hapo leo, Ju-matano, Julai 30, 2025, na kusomewa mashtaka hayo na Wakili wa Serikali, Frank Rimoy, aliyedai mwaka 2024, ndani ya Jiji la Dar es Salaam, kwa nia ya kudanganya walitengeneza nyaraka ya uongo ambayo ni kibali cha ku-miliki silaha cha Desemba 5, 2024, chenye jina la Ahmed Ally, huku wakijua kuwa si kweli.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geodrey Mhini, wakili huyo amedai katika shtaka la pili hadi la 13, katika kipindi cha mwaka 2024 ndani ya Mkoa wa Dar es Sa-laam, walitengeneza vibali vya kumiliki silaha vyenye majina ya Ahmed Ahmed Sandrudin, Omary Abdallah, Robert Koka, Fathi Ally, Mohamed Salim, Suleman Mbewa, Mickdad Chakindo, Irfan Nafari, Gulam Abbas Najafi, Is-mail Ismail na Salim Salim.
Shtaka la 14 hadi 16, washtakiwa hao wanadaiwa kuwa mwaka 2025 jijini Dar es Salaam, kwa nia ya kulaghai wali-tengeneza nyaraka za uongo ambazo ni vibali vya kumiliki silaha vyenye majina ya Marwaan Habretsh, Maurice Kiti-we na Said Mohamed, huku wakijua kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.
Washtakiwa walikana tuhuma hizo baada ya kusomewa mashtaka, upande wa mashtaka ulidai upelelezi bado unaendelea, hivyo kuomba Mahakama iwapangie tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
“Mheshimiwa Hakimu, kulingana na mashtaka ya-nayowakabili washtakiwa hawa, upande wa mashtaka hatuna pingamizi dhidi ya washtakiwa kupata dhamana, ila tunaomba itoe masharti yatakayowafanya washtakiwa ha-wa wafike mahakamani kila tarehe kesi yao inapoitwa,” amedai Wakili Rimoy.
Hakimu Mhini ametoa masharti matatu ya dhamana, ambayo ni kila mshtakiwa awe na mdhamini mmoja atakayesaini bondi ya Sh4 milioni.
Pia, wadhamini hao wanatakiwa wawe ni wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam na wenye barua kutoka Serikali za mitaa au barua ya utambulisho kutoka ofisini kama ni wafanyakazi.
Vilevile, wadhamini hao wanatakiwa wawe na vit-ambulisho vya Taifa (NIDA).
Hata hivyo, washtakiwa hao wameshindwa kutimiza masharti hayo, , hivyo wamepelekwa mahabusu.
Washtakiwa ‘wapekuwa’ mahakamani
Tofauti na washtakiwa wengine wanaofikishwa mahaka-mani hapo kwa mara ya kwanza wakitokea Polisi wakiwa wamevaa viatu, wao walikuwa hawajavaa viatu (wapeku-wa).
Kati ya washtakiwa hao wanane, ni washtakiwa wawili tu waliokuwa wamevaa kandambili rangi ya buluu na nyekundu.
Washtakiwa wasota rumande siku 70
Baada ya Hakimu kutoa masharti ya dhamana, washtakiwa waliulizwa kama wana wadhamini ili wadhaminiwe.
Hakimu: Washtakiwa mna wadhamini? Kama wadhamini wapo nje, waitwe waingie ndani ya Mahakama wasikilize masharti ya dhamana.
Kutokana na kauli ya hakimu huyo, mmoja wa askari wali-okuwepo ndani ya chumba cha Mahakama alitoka nje kui-ta wadhamini wa kesi hiyo.
Baada ya muda mfupi, alirudi na kuingia ndani ya Ma-hakama akiwa na wadhamini wawili ambao hawakuwa na barua za utambulisho.
Hali hiyo ilimfanya mshtakiwa wa tatu katika kesi hiyo, E.7855 Sajenti Mlogo, kunyoosha mkono akiashiria kuom-ba Mahakama imruhusu kuongea.
Hakimu Mhini alimruhusu mshtakiwa huyo kuzungumza, ndipo alipoiomba Mahakama ipange tarehe fupi ili waje na wadhamini kwa kuwa wamekaa ndani (mahabusu ya Poli-si) kwa siku 70 hadi walipoletwa mahakamani, hivyo ndugu zao hawajui kuwa wapo mahakamani.
“Mheshimiwa Hakimu, naomba utupangie tarehe fupi ili tu-je kudhaminiwa kwa sababu tumekaa siku 70 ndani hadi leo hii tunaletwa mahakamani. Ndugu zetu hawajui kama tupo hapa mahakamani,” amedai Mlogo na kuongeza:
“Tumechukuliwa tu na kupakiwa katika gari, hatukuambi-wa tunaletwa huku, hivyo hatuna mawasiliano na ndugu zetu. Ndiyo maana unaona hakuna wadhamini waliokuja, kwa sababu hawana taarifa.” Hoja hiyo iliungwa mkono na washtakiwa wenzake.
Hakimu Mhini ameeleza kuwa anapanga tarehe inayotam-bulika kisheria ya siku 14 kwa washtakiwa waliokosa dha-mana, ili iwapo wadhamini watapatikana, wapelekwe ma-hakamani kwa hati ya wito kutoka rumande, ili waende kupata dhamana.
Hakimu Mhini baada ya kutoa ufafanuzi huo ameahirisha kesi hadi Agosti 12, 2025 kwa ajili ya kutajwa, na washtakiwa wamepelekwa rumande.