ASKARI watano na raia watatu wa Jiji la Dar es Salaam wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashitaka 16, yakiwemo ya kughushi vibali vya umiliki wa silaha na kuwasilisha nyaraka za uongo.
Katika hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani hapo na Wakili wa Serikali, Frank Rimoy, washtakiwa wametajwa kuwa ni PF Inspekta Fredrick Malekela (45), E 4627 Sajenti Kalemwa Kaunga (54), E 7855 Sajenti Edger Mlogo (54), F 1129 Sajenti Robert Titus (47), na F 5092 Sajenti John Kaponswe (46).
Washtakiwa wengine ni Damson Minyilenga (46), Simon Aloyce (60) ambaye ni mfanyabiashara, na Verand Liberio (29).
Katika kesi hiyo, washtakiwa wanakabiliwa na shtaka moja la kuwasilisha nyaraka ya uongo na mashtaka 15 ya kughushi.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Geofrey Mhini, ilidaiwa kuwa mwaka 2024 ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam, washtakiwa kwa pamoja walitengeneza nyaraka ya uongo kwa nia ya udanganyifu, ikionyesha kibali cha kumiliki silaha chenye jina la Ahmed Abdallah Ally, huku wakijua kuwa taarifa hizo si za kweli.
Imeelezwa kuwa washtakiwa hao pia waliwasilisha nyaraka ya uongo iliyodai kuwa ni kibali cha kumiliki silaha chenye jina la Ahmed Sandrudin, wakiwa na nia ovu ya kulaghai mamlaka husika.
Katika mashtaka ya kughushi, kwa mujibu wa upande wa mashtaka, inadaiwa kuwa katika kipindi hicho cha mwaka 2024, washtakiwa wote, wakiwa na nia ovu ya kulaghai, walitengeneza vibali vya umiliki wa silaha kwa kutumia majina na namba mbalimbali za watu tofauti tofauti, huku wakijua kuwa nyaraka hizo ni za kughushi.
Hata hivyo, washtakiwa wote wamekana kutenda makosa hayo na wamerudishwa rumande kwa kushindwa kutimiza masharti ya dhamana, ambapo mahakama ilimtaka kila mshtakiwa kuwa na mdhamini mmoja atakayesaini bondi ya Sh. Milioni nne, awe na kitambulisho cha NIDA na barua ya utambulisho kutoka serikali za mitaa.
Kesi hiyo imepangwa kutajwa tena Agosti 12, mwaka huu.
