Arusha. Hofu imezidi kutanda katika mtaa wa Olmokea iliyoko kata ya Sinoni baada ya leo tena mwili wa dereva bodaboda aliyefahamika Bosco Massawe ‘Rasta’(43) kukutwa umetundikwa juu ya mti mita chache kutoka nyumba aliyopanga, huku ukiwa na majeraha makubwa.
Mwili wa Bosco umekutwa katika hali hiyo, ikiwa imepita siku mbili tangu mwili wa mtoto Mishel Amani mwenye umri wa miaka miwili na nusu kukutwa umetupwa katika Mto Naura Julai 27, 2025 baada ya kutoweka katika mazingira ya kukutatanisha kwa zaidi ya masaa 27 akiwa nyumbani kwao Mtaa wa Olmokea, Kata ya Sinoni.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo leo Julai 30, 2025 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo amesema kuwa upelelezi umeanza juu ya tukio hilo.
“Tukio ndio kwanza limetokea leo na upelelezi ndio kwanza umeanza, bado hatuna taarifa ya kuwapa zaidi ya hayo mliyosikia kwenye tukio,” amesema Kamanda Masejo.
Jirani wa marehemu, Amina Issa amesema kuwa usiku wa kuamkia leo majira ya saa saba usiku aligongewa na kijana huyo akiomba hifadhi akidai kuwa hayuko sawa na kuna watu wanamfuatilia.
“Mimi niliangaza na sikuona hao watu hivyo nilimuondoa hofu kumwambia akalale wala hakuna shida, nashangaa alfajiri saa kumi anakuja jirani yangu mwingine na kuniambia kuwa Rasi amepotea na mlango wake uko wazi”.
“Tulitoka na kuanza kumtafuta bila mafanikio ikabidi tuite na majirani wengine kuungana ambapo asubuhi hii tuliona matone ya damu na m’buruzo kuelekea shambani na katika kufuata ndio tukakuta mwili unaning’inia juu ya mti,” amesema.
Amesema kuwa mwili huo uliotundikwa kwa kunyongwa kwa mkanda wake wa suruali, umekutwa ukiwa umetapakaa damu hadi usoni, huku akiwa na alama za kuteswa kwa kuchomwa na vitu vyenye ncha kali sehemu mbalimbali.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Olmokea iliyoko Kata ya Sinoni jijini Arusha, Abdallah Mgongo amesema alivyoona mwili inaonekana marehemu ameuawa na watu kisha kutundikwa ili ionekane amejiua kwa kujinyonga kwa kutumia mkanda wake wa kiunoni.
“Kutokana na majeraha makubwa ya kuashiria kupigwa sehemu mbalimbali za mwili wake, inaonekana marehemu ameuawa na watu hao ambao bado hawajafahamika na kisha kuburuza mwili wake na kwenda kuutundika juu ya mti ule,” amesema.
Naye Emmanuel Mallya amesema kuwa wanaliomba Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina kubaini undani wa tukio hilo la kuuawa kwa kijana huyo ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.