Camara alivyoruka viunzi mkataba mpya

LICHA ya kuwa kipa bora wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2024/25 kwa takwimu na hata ushindani wa kimataifa, Moussa Camara alijikuta kwenye sintofahamu kuhusu hatma yake ndani ya Simba.

Tishio la kupigwa chini lilikuwa wazi, si kwa sababu ya kuruhusu mabao 13 kwenye ligi, bali kwa sababu ya mfululizo wa makosa katika mechi muhimu yaliyowagharimu wekundu wa Msimbazi.

Camara, raia wa Guinea, aliweka rekodi ya kuvutia msimu uliopita kwa kutoruhusu bao  ‘clean sheets’ katika mechi 19 ligi kuu. Hilo pekee linamtambulisha kama mmoja wa makipa bora waliowahi kupita Ligi Kuu Bara katika miaka ya karibuni.

Lakini, takwimu hizo hazikutosha kuwahakikishia baadhi ya viongozi na mashabiki kuwa bado anastahili kuendelea kubeba mikoba ya kuwa kipa namba moja Simba kwa msimu wa 2025/26.

Achana na kosa la dabi ambalo aliutemea mpira ndani ambao ulikuwa ukionakana kutoka na Yanga ikapata bao pekee la ushindi katika mechi ya kwanza ya dabi, Oktoba 4, 2024, Simba ikiwa nyumbani iliikaribisha Coastal Union kwenye Uwanja wa KMC.

Mechi hiyo ilianza kwa matumaini makubwa kwa wekundu hao wa Msimbazi waliokuwa mbele kwa mabao 2-0, lakini ikaisha kwa sare ya 2-2. Mabao yote mawili ya Coastal yalitokana na makosa ya Camara, hali iliyowapa Coastal nafasi za kurudi mchezoni.

NGOMA ALIVYOMNYOOSHEA KIDOLE

Katika mechi ya marudiano wa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane iliyopigwa kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar, Camara alijikuta kwenye mvutano ndani ya uwanja.

Wakati timu ikihitaji kujilinda huku ikihitaji mabao ya kusawazisha, Camara alifanya uamuzi utata ambao ungeweza kuiangusha Simba kwa mara nyingine. Kosa lake lilimfanya kiungo wa Simba, Fabrice Ngoma kumjia juu kwa ukali muda mfupi baada ya tukio hilo.

Katika harakati za kuangalia mbadala wa Camara, jina la Issa Fofana kutoka Al Hilal ya Sudan lilianza kutajwa kwa uzito. Fofana ni kipa aliyeonyesha kiwango kikubwa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, huku pia akiwa na uzoefu mkubwa wa mechi za presha.

Mabosi wa Simba waliangalia uwezekano wa kumsajili, lakini bei yake haikuwa rafiki angalau dola 150,000 zilihitajika kumvua jezi ya Al Hilal.

Kwa timu ambayo tayari ilikuwa kwenye mchakato wa kusuka upya baadhi ya maeneo ya kikosi, na huku bajeti ikiwa imeshabana kwa sajili nyingine kama mshambuliaji, beki wa kati na kiungo mkabaji, gharama ya kipa wa kiwango hicho ilikuwa nje ya mipango ya muda mfupi.

Kocha mkuu wa Simba, Fadlu Davids, alishikilia msimamo kuwa Camara bado ana nafasi ya kuboresha kiwango chake.

Kwenye kikao cha tathmini ya msimu, Davids aliweka wazi kuwa makosa ya Camara ni ya kiufundi na kisaikolojia, na yanaweza kurekebishika.

Ndiyo maana, licha ya vuta nikuvute iliyodumu kwa karibu wiki mbili, Simba iliamua kumpa Camara mkataba mpya wa mwaka mmoja huku kukiwa na kipengele cha kuongezewa mwaka mwingine endapo atatimiza baadhi ya viwango vilivyowekwa.

Kwa upande wa takwimu, hakuna mjadala kuwa Camara alifanya kazi ya ziada. Alicheza mechi nyingi za Ligi Kuu Bara msimu wa 2024/25 na kufanikisha ‘clean sheet’ 19, sawa na asilimia 63. Hii ni rekodi ya kuvutia inayopaswa kuheshimiwa.

Katika mashindano ya kimataifa, Camara alicheza mechi 13 kwenye kampeni ya Kombe la Shirikisho Afrika – kwa jumla ya dakika 1,170. Katika hizo, aliruhusu mabao 10 tu, huku mechi sita akiwa hajafungwa kabisa.

Simba inapoingia msimu wa 2025/26 ikiwa na lengo la kuendeleza makali yake kwenye michuano ya kimataifa na kulinda heshima yake ya ndani, Camara atakuwa na mzigo mkubwa wa kuhakikisha hafanyi makosa tena kama ilivyokuwa msimu uliopita.

Atahitaji kuwa bora zaidi, kuongeza uwezo wake wa mawasiliano na mabeki, pamoja na kuwa na mwelekeo sahihi katika mechi kubwa.