ALIYEKUWA beki wa kati wa Simba SC, Che Fondoh Malone, sasa ni mchezaji halali wa klabu ya USM Alger ya Algeria baada ya kufuzu vipimo vya afya na kusaini mkataba wa miaka miwili na mabingwa hao wa zamani wa Kombe la Shirikisho Afrika.
Akizungumza akiwa jijini Algiers mara baada ya kuthibitishwa kuwa mchezaji mpya wa timu hiyo, beki huyo raia wa Cameroon amesema licha ya kuondoka Simba, bado anaamini klabu hiyo iko kwenye njia sahihi na iko karibu kufika kilele cha mafanikio makubwa chini ya Kocha Fadlu Davids.
“Soka ni safari yenye hatua tofauti,” alisema Che Malone na kuongeza.
“Leo niko hapa Algeria, nikiwa na mwanzo mpya, lakini moyo wangu bado unaiheshimu Simba. Siwezi kuondoka bila kusema ukweli.
“Kocha Fadlu Davids anajenga kitu kikubwa. Nimekuwa naye, nimeona mbinu zake, namna anavyowasimamia wachezaji na ninayo imani Simba itafika nchi ya ahadi.”
Julai 2023, Che Malone alijiunga na Simba akitokea Cotton Sport ya Cameroon, na haraka akawa sehemu ya safu ya ulinzi ya wekundu hao wa Msimbazi sambamba na Henock Inonga Baka.
Alikuwa nguzo muhimu kuanzia katika ligi hadi michuano ya kimataifa. Kuondoka kwa Inonga ambaye alijiunga na AS FAR Rabat Julai 2024, kulimfanya kuwa mchezaji kiongozi kwenye eneo la beki ya kati akicheza na Abdulrazack Hamza na Chamou Karaboue.
“Simba ni taasisi kubwa yenye malengo makubwa. Kuondoka kwangu ni hatua nyingine ya maisha yangu ya soka,” alisema.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi kutoka kwa USM Alger, mkataba wa uhamisho wa Malone kutoka Simba una kipengele kinachoiruhusu Simba kupata asilimia 15 ya ada yoyote endapo atauzwa kutokea hapo.
Che Malone ameondoka wakati Simba imeshusha tayari beki mwingine wa kati Rushine De Reuck (29) kutoka Mamelodi Sundowns kwa mkataba wa mwaka mmoja wenye kipengele cha kuongeza.
Reuck atasaidiana na Abdulrazack Mohamed Hamza na Chamou Karaboue ambao ni mabeki wa kati waliosalia kwenye kikosi hicho.