DILI MOJA LA KIBABE | Mwanaspoti

UHAMISHO wa Luis Diaz kwenda Bayern Munich utaibua mshikemshike kwenye klabu nyingi za Ligi Kuu England zitakapopigana vikumbo huko sokoni.

Supastaa huyo wa kimataifa wa Colombia, 28, ameachana na Liverpool ili kwenda kukipiga Bayern Munich kwa dili la uhamisho wa Pauni 65.5 milioni.

Kutokana na dili hilo la Diaz kwenda Ujerumani, Liverpool sasa itapambana kunasa mtu wa kuja kuziba pengo lake na kwenye hilo inampigia hesabu straika wa Newcastle United, Alexander Isak.

Isak, 25, wiki iliyopita aliwaambia mabosi wake wa Newcastle kwamba anataka kuachana na maisha ya St James’ Park kwenye dirisha hili la majira kiangazi.

Kutokana na hilo, Isak hakwenda na timu yake kwenye ziara ya pre-season huko Asia na kuzidi kuchochea uvumi wa kuachana na timu hiyo.

Ripoti zinafichua kwamba straika huyo wa mabao ameshafikia makubaliano binafsi na miamba ya Anfield, Liverpool. Hata hivyo, Liverpool italazimika kulipa mkwanja mrefu sana kukamilisha dili hilo.

Kutokana na Isak kubakiza mkataba wa miaka mitatu, Newcastle inahitaji ada ya Pauni 150 milioni. Klabu hizo mbili zinatarajia kukutana siku chache zijazo, huku Liverpool ikiripotiwa kutenga Pauni 120 milioni kwa ajili ya kumnasa Isak.

Kama Liverpool itampata Isak, basi hiyo ina maana Newcastle itaingia sokoni kusaka straika mpya wa kuja kuziba pengo lake. Na kwenye hilo, kikosi hicho kinachonolewa na kocha Eddie Howe kimeshakosa huduma ya straika Hugo Ekitike, ambaye amejiunga na Liverpool kwa ada ya Pauni 79 milioni.

Newcastle sasa inampiga hesabu za kwenda kumsajili staa wa RB Leipzig, Benjamin Sesko, ambaye ameripotiwa atapatikana kwa Pauni 70 milioni.

Newcastle imemruhusu pia straika Callum Wilson kuondoka bure kwenye dirisha hili, hivyo kuna ulazima mkubwa kwa miamba hiyo ya St James’ Park kunasa mshambuliaji mwingine kama Isak ataondoka.

Straika Ollie Watkins, ambaye klabu yake ya Aston Villa inamthaminisha kwa Pauni 40 milioni hadi Pauni 45 milioni, yupo kwenye rada za Newcastle. 

Mastaa wengine Yoane Wissa na Nicolas Jackson, nao wapo kwenye mipango ya Newcastle kwenye msako wa straika mpya.
Ndoto za Newcastle zinaweza kutibuliwa na Manchester United, ambayo pia ipo sokoni kusaka straika mpya kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi.

Man United imeshafanya usajili wa Pauni 130 milioni kunasa huduma za mastaa Matheus Cunha na Bryan Mbeumo kwenye kuboresha safu yao ya ushambuliaji.

Lakini, licha ya kutumia pesa nyingi, kikosi hicho cha kocha Ruben Amorim bado kinahitaji straika wa mabao. Na kinachoelezwa kwenye hilo, majina ya mastraika wawili yamewekwa ubaoni, ambao ni Sesko na Watkins.

Aston Villa imekuwa ikiweka ugumu kiasi wa kuhusu straika wao Watkins. Na kama wataamua Watkins aondoke, basi chama hilo linalonolewa na Unai Emery litahitaji saini ya straika mpya kabla ya dirisha la usajili kufungwa.

Na kinachoripotiwa ni kwamba straika huru, Dominic Calvert-Lewin, ameanza kuwekwa kwenye hesabu za Aston Villa ikihitaji huduma yake endapo kama Watkins atafungasha virago vyake kuondoka Villa Park.

Dili zote hizo na hekaheka za klabu za Ligi Kuu England kusaka mastraika wapya zitakuwa kali baada ya Diaz kukamilisha dili la kutua Bayern.