Dk Biteko mgeni rasmi CHAN dinner gala, mbili kuwasili Dar kesho

Wakati timu za Burkina Faso na Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) zikitarajiwa kuwasili nchini Tanzania kesho Alhamisi, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya chakula cha jioni (Chan Dinner Gala) iliyopangwa kufanyika Ijumaa kwenye Hoteli ya Johari Rotana.

Msemaji Mkuu wa Serikali na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, amesema Dk Biteko amethibitisha kushiriki katika hafla hiyo maalum ambayo imepangwa kuanza saa 12:00 jioni.

Msigwa amesema mbali ya Dk Biteko, hafla hiyo pia itawakutanisha wageni mashuhuri wa ndani na nje ya nchi.

Amesema hafla hiyo ni ukaribisho rasmi wa wageni hao hapa nchini na wanatarajia Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Dk Patrice Motsepe atahudhuria pamoja na viongozi wakuu wa CAF na mashirikisho ya soka kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika.

“Gala hiyo pia itahudhuriwa na mawaziri wa michezo kutoka Kenya na Uganda, mabalozi wa nchi mbalimbali na wadau wakuu wa sekta ya michezo na utalii.

“Tumealika mabalozi, viongozi wa michezo nchini na wadau wakubwa wa sekta za utalii na utamaduni. CHAN si tu mashindano ya soka, bali ni jukwaa la kuonyesha ukarimu wa Watanzania, utamaduni wetu tajiri na vivutio vyetu vya utalii,” amesema Msigwa.

Amesisitiza kuwa CHAN 2024 ni fursa muhimu ya kuitangaza Tanzania kimataifa, huku miji ya Dar es Salaam na Zanzibar ikiwa kitovu cha matukio mbalimbali ya mashindano hayo.

Msigwa amebainisha kuwa uuzaji wa tiketi unaendelea vizuri na kuwataka mashabiki wa soka kuendelea kununua tiketi ili kuujaza uwanja.

“Tunahitaji uwanja ujazwe. Mashabiki wetu wanajulikana kwa hamasa yao, tujitokeze kwa wingi kuwapa Taifa Stars nguvu ya ziada. Maandalizi yote yamekamilika, Tanzania iko tayari kuikaribisha Afrika,” amesema.

Katika kuongeza burudani, msanii nyota wa Bongo Fleva, Rayvanny, atatumbuiza kwenye uzinduzi rasmi wa mashindano hayo.

Rayvanny ameahidi kutoa burudani ya kukumbukwa itakayoakisi utamaduni wa muziki wa Tanzania na furaha ya Chan.

Wakati huohuo, timu mbili za kundi B, Burkina Faso na Jamhuri ya Afrika ya Kati zitawasili kesho Alhamisi tayari kwa mashindano hayo.

Timu nyingine za kundi B ni wenyeji Tanzania (Taifa Stars), Madagascar, na Mauritania.

Taifa Stars itafungua dimba kwa kuvaana na Burkina Faso siku ya Jumamosi saa 2 usiku kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Katika hatua nyingine, Zanzibar, maandalizi pia yamekamilika. Timu za Kundi D zitakazocheza kisiwani humo Senegal, Nigeria, na Congo Brazzaville tayari zimewasili kwa ajili ya mechi zao kwenye Uwanja wa Amaan. Timu ya mwisho kwenye kundi hilo, Sudan, inatarajiwa kuwasili hivi karibuni.