Haya hapa matokeo waliopenya ubunge viti maalumu

Dar /Mikoani. Baadhi ya watiania ubunge viti maalumu wanaomaliza muda wao, katika mikoa minne wamefanikiwa kutetea nafasi hizo kwa kupenya kwenye mchakato wa kura za maoni uliofanyika leo Jumatano Julai 30,2025.

Kura za maoni hizo zimefanyika katika mikoa mbalimbali kupitia mikutano mikuu ya Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT). Baadhi ya mikoa iliyopata wagombea ubunge viti maalumu ni pamoja na Dar es Salaam, Njombe, Shinyanga na Kilimanjaro.

Mchakato wa kura za maoni ni miongoni mwa hatua za awali, ambapo baada ya hapo watiania walioibuka kidedea watakwenda hatua nyingine kujadiliwa kisha kupitishwa na Kamati Kuu tena.

Katika Mkoa wa Shinyanga, waliokuwa wabunge wa viti maalumu mkoani humo waliomaliza muda wao, wamefanikiwa kutetea viti vyao kwa kuongoza kwa kura za maoni kati ya wagombea wote walioshinda nao.

Akitangaza matokeo hayo  msimamizi mkuu  wa uchaguzi huo, Halima  Dendego ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Singida, amesema  uchaguzi huo umefanyika kwa uhuru na  haki.

Dendego amesema aliyeongoza kwenye kura za maoni ni Santiel Kirumba (730) akifuatiwa na Christina Mnzava na Salome Makamba ambaye kipindi kilichopita alikuwa mbunge wa viti maalumu.

Mkoani Dar es Salaam, walioshinda ni Janeth Mahawanga ambaye ni mbunge anayemaliza muda wake huku anayemfuatia Amina Said akiingia kwa mara kwanza.

Msimamizi mkuu wa uchaguzi  huo,  Idrisa Ramadhani amesema katika wagombea tisa waliokuwa wakipigiwa kura Mahangwa ameongoza kwa kupata kura 448 huku Amina kura 421 na Jane Jerry kura akiwa wa tatu kwa kupata kura 300.

Naye, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Pindi Chana, ameibuka mshindi matokeo ya awali ya viti maalumu mkoani Njombe kwa kupata kura 700, akifuatiwa na Rebecca Nsemwa kura 588.

Msimamizi wa Uchaguzi, ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu CCM Taifa (MNEC) wa Mkoa wa Mbeya, Ndele Mwanselela amesema wajumbe katika uchaguzi huo waliopaswa kuwepo ni 861, lakini waliohudhuria na kupiga kura ni 841 na kura moja pekee ndiyo imeharibika.

Mwanselela amewataja wagombea wengine kuwa ni Neema Mgaya (263), Anna Mwalongo (53), Dk Scholastika Kevela (47) Tegemea Mbogela (22), Magreth Kyando (5) Tulalumba Mloge (3).

Katika Mkoa wa Kilimanjaro aliyekuwa mbunge wa viti maalumu mkoani humo, Esther Malleko ameongoza kura za maoni kwa kupata kura 1,149 akifuatiwa na Zuena Bushiri kura 964.

Katika uchaguzi huo uliofanyika katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika, Mjini Moshi, umehusisha wagombea wanane huku wajumbe wa mkutano mkuu maalumu wa UWT wakiwa 1,329.

Matokeo hayo yalitangazwa na msimamizi wa uchaguzi huo, Dk Batilda Burian, ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga, akiwataja wengine ni  Regina Chonjo (145), Caroline Lyimo (109), Never Zekeya (108), Pamela Mallya(69), Marry Nashanda(19) na Aika Ngowi aliyepata kura(12).

Msimamizi huyo wa uchaguzi, amesema hayo ni matokeo ya awali na kwamba mchakato bado unaendelea.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa matokeo zaidi.