Ibenge asaka mrithi wa Fei Toto

WAKATI tetesi za kiungo wa Azam, Feisal Salum ‘Fei Toto’ zikizidi kuwa nyingi kwamba huenda akajiunga na Simba au Yanga, kocha mpya wa kikosi hicho Florent Ibenge amejiandaa kwa lolote.

Ibenge ambaye ametua Azam akitokea Al-Hilal ya Sudan ndiye atakayekiongoza kikosi hicho msimu ujao akirithi mikoba kutoka kwa Rachid Taoussi.

Taarifa kutoka ndani ya Azam ziliiambia Mwanaspoti; “Hatutaki kumuingilia kocha, kila kitu anafanya mwenyewe mnaona hivi karibuni alitajwa sana Chama (Clatous) lakini sio kweli mwenyewe kocha (Ibenge) anataka watu tofauti kabisa.

“Labda yule Mkongomani Basiala (Agee) ndio mmoja ya watu anaowataka, mwingine ni kutoka Rwanda anaitwa Djabel (Manishimwe) alikuwa Iraq ndio watu anaofikiria kuwaongeza.”

Kupitia Mwanaspoti Mkuu wa Idara ya Habari ya Azam, Thabit Zakaria alisema hadi sasa hakuna timu ambayo imetuma ofa ya kumnunua Fei.

Simba ilitangulia kumtaka Basiala mapema tu, lakini haikufanya uamuzi wa mwisho kisha juzi, wakarudi na dau la Dola 70,000 wakimtaka kiungo fundi huyo.

Hata hivyo, wakati Maniema wakiweka ngumu kumuachia kiungo huyo kwa dau hilo, Azam imetua ikitaka huduma ya Mkongomani huyo msimu ujao.

Inaelezwa kwamba kocha Florent Ibenge ndiye aliyependekeza usajili wa kiungo huyo anayeweza kucheza nafasi ya kiungo mshambuliaji.

Mwanaspoti iliwahi kuandika kuwa, Simba ilitajiwa bei ya kumpata kiungo huyo, huku ikitakiwa kumnunua kwa Dola 150,000 licha ya wao kutoa kiasi walichotoa.

Kama atatua Azam atacheza nafasi moja na Fei, lakini kama tetesi za Mzenji huyo kwenda Simba au Yanga zikikamilika, Agee atakuwa ndiye mrithi wake.