INEC yataka asasi za kiraia kuzingatia Katiba utoaji elimu ya mpigakura

Dar es Salaam. Wakati mchakato wa uchaguzi mkuu ukitarajiwa kuanza mwezi ujao, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imezitaka asasi za kiraia na taasisi zilizopewa kibali cha kutoa elimu ya mpigakura kuzingatia Katiba, sheria na taratibu zilizowekwa.

INEC imesema lengo ni kuhakikisha mchakato huo unakuwa huru, uwazi, haki na kuaminika, kwa kuweka mazingira sawa ya ushindani kwa wagombea wa vyama vyote vitakavyoshiriki uchaguzi huo.

Pia, INEC imesisitiza matumaini makubwa kwa wadau hao katika kufanikisha uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumatano ya Oktoba 29, 2025, kwa kutegemea ushiriki wa asasi na taasisi hizo katika hatua zote zilizosalia hadi kufikia siku ya uchaguzi.

Kwa mujibu wa tume hiyo, kuanzia Agosti 9, 2025 hadi 27 utafanyika uchukuaji na urejeshaji wa fomu za urais na Makamu wa Rais, huku za udiwani na ubunge fomu zitatolewa kuanzia Agosti 14 hadi 27. Kampeni zitaanza Agosti 28, 2025 hadi Oktoba 28, na siku itakayofuata ni ya kupiga kura.

Akizungumza leo, Jumatano, Julai 30, 2025, kwenye mkutano wa INEC na wawakilishi wa taasisi na asasi za kiraia kuhusu uchaguzi mkuu, mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Jacobs Mwambegele, amewaomba wadau hao kutekeleza jukumu hilo kama walivyofanya kwenye uboreshaji wa daftari la mpigakura.

Jaji Mwambegele amefafanua kuwa mwaka 2024, Bunge lilitunga sheria mbili za uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani, pamoja na Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi ya mwaka 2024.

Kutokana na hilo, Jaji huyo amesema INEC ilitunga kanuni za uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani za mwaka 2025, pamoja na maelekezo ya uchaguzi kwa ajili ya wadau.

“Mtapatiwa nakala za sheria, kanuni na maelekezo mbalimbali, hivyo naomba mkazisome ili ushiriki wenu katika mchakato wa uchaguzi ufanyike kwa kuzingatia masharti na matakwa ya sheria na maelekezo husika,” amesema Jaji Mwambegele.

Hata hivyo, Jaji Mwambegele amesema INEC inawashukuru wadau hao kwa kuendelea kuiunga mkono Tume kwenye utekelezaji wa kutoa elimu ya mpigakura.

“Ni dhahiri bila ushirikiano huo, INEC isingeweza kufanikisha kwa ufanisi jukumu lake la kutoa elimu hiyo. Hadi sasa Tume imeshafanya maandalizi mbalimbali ya uchaguzi mkuu,” ameeleza.

Pamoja na maandalizi hayo kukamilika, Jaji Mwambegele amesema ili mchakato huo ufanikiwe kwa kiwango kikubwa, unategemea ushirikiano wa asasi na taasisi hizo katika kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa uchaguzi mkuu.

Ofisa Miradi wa asasi ya Restless Development, Fatma Mwinyiamiri, amesema hatua ya INEC kukutana na wadau hao inaendeleza ushirikiano miongoni mwa tume hiyo, asasi na taasisi hizo.

“Tunaishukuru INEC kwa mkutano wa leo, ni mwendelezo wa kupeana elimu miongoni mwetu. Tunataka kuhakikisha hii elimu ya mpigakura inawafikia walengwa ili kuelewa umuhimu wa kupiga kura Oktoba,” amesema Mwinyiamiri.