Majimbo haya ‘kitaumana’ kura za maoni CCM

Dar es Salaam. Kwa majimbo haya, joto lake ni asilimia 100. Hivi ndivyo unavyoweza kubashiri haraka.

Ni majimbo ambayo vigogo wanakwenda kuchuana katika mchakato wa kura za maoni za Chama cha Mapinduzi (CCM) zitakazofanyika Agosti 4, 2025.

Wakati kukiwa na mchuano huo, baadhi ya majimbo wagombea wake watakuwa hawana kibarua kigumu kutokana na wagombea wake waliojitokeza kuomba uteuzi, kujikuta hawana wapinzani hali iliyoirahisishia kazi Kamati Kuu ya CCM iliyokuwa ikifanya kazi ya kuteua.

Hali hiyo inawafanya wagombea wake sasa kusubiri hatua inayofuata ya kupigiwa kura ya ‘ndiyo’ au ‘hapana’ na wajumbe wa CCM, kabla ya majina yao kupelekwa kwa ajili ya uteuzi rasmi na Tume Huru ya Uchaguzi (INEC). 

Mchuano unaozungumzwa ni wa baada ya Kamati Kuu ya CCM iliyoketi jana Jumatatu Julai 28, 2025, kuhimitisha shughuli yake ya kuchuja majina ya watiania wa ubunge kwenye majimbo na viti maalumu.

Jana, Kamati Kuu ilihitimisha kazi ya mchujo iliyoanzwa kufanywa na kamati za siasa za wilaya na mikoa.

Miongoni mwa majimbo ambayo makada wa CCM watakuwa na kibarua kigumu cha kuchagua mmoja atakaye peperusha bendera ya chama hicho, kabla ya jina hilo kujadiliwa tena na kamati kuu kwa hatua zaidi, ni Makambako.

Jimbo hilo ambalo lipo mkoani Njombe, linawaniwa na Deo Sanga anayetetea nafasi hiyo na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo.

Licha ya kuwa RC, Chongolo pia alishawahi kuwa Katibu Mkuu wa CCM na kabla ya nafasi hiyo, aliwahi pia kuwa Mkuu wa Wilaya ya Longido na Kinondoni. 

Mtifuano mwingine utakuwa katika Jimbo la Kinondoni, ambako mbunge wa sasa, Abbas Tarimba anakwenda kukabiliana na makada wanane katika hatua ya kura za maoni ambao ni Iddi Azzan aliyewahi kuwa mbunge wa jimbo hilo mwaka 2015-2020. 

Makada wengine watakaokabiliana na Tarimba ni Wilfred Nyamwija, Michael Wambura, Jerusa Kitoto, Julieth Rushuli, Wangota Salum na Zena Kiputiputi.

Mbali na hilo, jimbo lingine ni la Chemba mkoani Dodoma, linalowakutanisha  Juma Nkamini, Kunti Majala aliyekuwa mbunge wa viti maalumu anayemaliza muda wake, mwanahabari Hamis Mkotya ambaye mara kadhaa amejaribu kutiania bila mafanikio, Omar Futon na Francis Julius.

Pata shika nguo kuchanika nyingine iko Jimbo la Geita Mjini ambako Kamati Kuu imerejesha majina ya Constantine Kanyasu anayetetea nafasi yake, Upendo Peneza aliyewahi kuwa mbunge wa viti maalumu, Gabriel Robert aliyewahi kushika nyadhifa za ukuu wa wilaya na mkoa, John Saulo na Chacha Wambura.

 Jesca Msambatavangu mbunge anayemaliza muda wake, anakwenda kuvaana na Mchungaji Peter Msigwa aliyewahi kuwa mbunge wa Iringa Mjini kwa miaka 10 kuanzia 2010 hadi 2020.

Lakini wapo makada wengine ambao ni pamoja na Fadhil Ngajilo, Edward Chengula, Islam Huwel na Moses Ambindwile.

Ukiachana na majimbo hayo, kibarua kingine kwa wajumbe kitakuwa katika Jimbo la Bunda Mjini, mbunge wa sasa Chacha Maboto atakabiliana na wenzake wanne akiwamo mbunge wa viti maalumu anayemaliza muda Ester Bulaya.

Bulaya aliwahi kuwa mbunge wa jimbo hilo mwaka 2015/2020.

Uchaguzi Mkuu uliofanyika 2020, Bulaya alijitosa tena kugombea jimbo hilo kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) lakini Maboto akaibuka mshindi.

Safari hii wanapambana wakiwa ndani ya CCM sambamba na makada wengine wa chama hicho, Kambarage Wasira, Joseph Buluba na Exavery Rugina.

 Kibarua kingine kwa wajumbe kipo Jimbo la Sengerema ambako kuna vigogo wanaowania uteuzi huo ambao ni Hamis Tabasamu anayemaliza muda wake, William Ngeleja aliyewahi kuwa mbunge wa jimbo hilo kwa miaka kadhaa, lakini alishindwa katika kura za maoni za mwaka 2020. 

Makada hao watachuana na wenzao kina Martin Lubango, Omar Nigura, Wilson Shimo, Joshua Shimiyu na Rachel Nyarusanda.

Kitimutimu kitakuwa Jimbo la Buchosa ambako Eric Shigongo atakabiliana na Dk Charles Tizeba aliyewahi kuwa mbunge wa jimbo hilo.

Wengine ni Nandi James, Kelebe Luteli, Jackline Milazi na Leonard Masai.

Jimboni Namtumbo mkoani Ruvuma nako hakujapoa, mbunge anayemaliza muda wake, Vita Kawawa atakabiliana na Dk Juma Homera aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya.

Pia, watachuana na makada Dk Sharif Ngonyani, Mussa Chowo, Shaibu Majiwa. Lakini katika Jimbo la Nyasa kutakuwa na mchuano kati ya Stella Manyanya mbunge wa sasa na aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya, John Nchimbi.

 Manyanya na Nchimbi watakabiliana na Johnes Liombo, Duwa Chengula, John Kapinga na Stanley Mahundi katika kura za maoni.

Jimbo la Shinyanga Mjini kutakuwa na kazi kati ya mbunge wa sasa, Patrobas Katambi na Stephen Masele aliyewahi kuwa mbunge kwenye jimbo hilo.

 Katika mchakato wa kura za maoni za mwaka 2020, Masele alikatwa na jina la Katambi lililochomoza, sasa wawili hawa wanakutana tena wakienda kupambana na Paul Blandy, Hassan Fatiu, Abubakar Mukadamu, Eustad Ngatale na Hosea Karume.

Jimbo la Singida Magharibi, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba atakabiliana na makada watatu katika kura za maoni ambao ni Jumbe Katala, Michael Lemmy na Emiliana Samson.

Funga kazi pia itakuwa Jimbo la Makete, huko  Festo Sanga anayetetea jimbo hilo, atakuwa na kibarua kizito katika kura za maoni mbele ya Toba Nguvila aliyewahi kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Lakini pia yumo aliyewahi kuwa mbunge wa jimbo hilo, Profesa Norman Msigala pamoja na makada wengine waliopitishwa na kamati kuu ambao ni Award Mpandila na Selina Msigwa.

Wakati wagombea wengine wakisubiri hekaheka za kushinda na wenzao katika kura za maoni, kwa majimbo ya Kiwani, Kojani, Chalinze na Mchinga, hali itakuwa tofauti huenda wajumbe watapiga kura za ndio au hapana kutokana na kuwa na mtiania mmoja.

Mathalani, Bukombe aliyechukua fomu ni Dk Doto Biteko ambaye ni Naibu Waziri Mkuu, vivyo hivyo Jimbo la Kiwani kisiwani Pemba ni Hemed  Suleiman Abdullah (Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar) na Hamad Hassan Chande wa Jimbo la Kojani (mjumbe wa kamati kuu CCM).

Wengine ni Salma Kikwete (Mchinga) na Ridhiwani Kikwete (Chalinze).