Malumbano ya hoja kesi dhidi ya Lissu kuahirishwa

Dar es Salaam. Ombi la kuahirishwa kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu limeibua mvutano wa hoja za kisheria katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, huku mshtakiwa huyo anayejitetea mwenyewe akieleza azma ya kwenda Mahakama ya Rufaa kupinga Kanuni za Ulinzi wa Mashahidi za mwaka 2025.

Mbali ya hayo, Mahakama imezuia Lissu kupewa maji ya kunywa kutoka kwa kaka yake Alute Mughwai, ambaye ni sehemu ya jopo la mawakili wake waliokuwa wakimtetea awali, kabla ya kuamua kujitetea mwenyewe.

Badala yake Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu, Franco Kiswaga anayesikiliza shauri hilo ameelekeza Lissu amepewe maji na Mahakama.

Hayo yamejiri leo Julai 30, 2025 shauri hilo lilipotajwa mbele ya hakimu Kiswaga.

Lissu anakabiliwa na kesi ya uhaini mahakamani hapo ikiwa ni hatua za awali, kabla ya shauri kuhamishiwa Mahakama Kuu yenye mamlaka ya kisheria kuisikiliza.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) amefungua shauri la maombi ya jinai Mahakama Kuu namba 17059 la mwaka 2025 akiomba amri ya ulinzi wa baadhi ya mashahidi wanaotarajiwa kutoa ushahidi katika kesi hiyo inayosubiri kuamuliwa.

Kutokana na hilo, upande wa mashtaka umeieleza Mahakama kuwa bado kesi ya uhaini dhidi ya Lissu haijasajiliwa Mahakama Kuu, hivyo umeomba ahirisho la kesi hiyo hadi tarehe nyingine kusubiri uamuzi.

Kiongozi wa jopo la waendesha mashtaka katika kesi hiyo, Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga akiwasilisha taarifa kuhusu usajili wa kesi hiyo, amesema Jamhuri bado haijapeleka Mahakama Kuu hati ya mashtaka kwa kuwa Mahakama hiyo haijatoa uamuzi wa maombi ya kuwalinda mashahidi na imepanga kuutoa Agosti 4, 2025.

Amesema sababu hiyo imemfanya DPP kushindwa kupeleka Mahakama Kuu hati ya mashtaka kwa kuwa taarifa hiyo inatakiwa iambatane na maelezo ya mashahidi ambao ndio wanaombewa amri ya kulindwa kabla ya upelekaji hati ya mashtaka Mahakama Kuu.

Katuga ameiomba Mahakama ione kwamba, sababu ya kusubiri uamuzi wa Mahakama Kuu ni ya msingi kwa kutumia kifungu cha 265 cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA), Sura ya 20, Marejeo ya Mwaka 2023.

Wakili huyo ameomba kesi iahirishwe hadi Agosti 14, 2025 ili kupata muda wa kuandaa nyaraka za mashahidi kama maombi yao yatakubaliwa.

“Ahirisho tena…, ahirisho… tena,”ndivyo Lissu alivyoanza kujibu hoja za Jamhuri akieleza maombi yasiyoisha ya ahirisho kuwa, ni ushahidi mwingine wa matumizi mabaya ya utaratibu wa mwenendo wa Mahakama na kwamba, hayo yanatokea kwa sababu mahakama inayaruhusu.

“Kwa hiyo tunaendeshwa na mawakili wa Serikali kwa sababu Mahakama yako tukufu imeruhusu kuendeshwa na mawakili wa Serikali,” amesema Lissu.

Amesema amri ya mwisho ya Mahakama hiyo ya Julai 15, 2025 ilisema Julai 30, 2025 upande wa mashtaka walete taarifa ambayo walitakiwa wawe wemeipeleka Mahakama Kuu ili leo (Julai 30) aweze kusomewa taarifa hiyo.

Amedai upande wa mashtaka haukufanya hivyo kwa sababu unatarajia hakimu atakubali kama ambavyo amekuwa akiwakubalia kila walichoomba.

Lissu amedai ni mwendelezo wa matumizi mabaya ya utaratibu wa Mahakama unaotokana na ushirikiano wa Mahakama.

Katika hoja zake, Lissu amenukuu kitabu kilichoandikwa na Jaji Mkuu wa Tanzania mstaafu, Barnabas Samatta kuwa: “Majaji dhaifu ni chanzo cha ukiukwaji wa haki za watu.”

Lissu amedai majaji dhaifu ni pamoja na mahakimu dhahifu na kwamba, kutokutekeleza amri zake mwenyewe na yeye kuwekwa mahabusu kwa siku ya 112 ambazo wanataka ziongezwe, ni kwa sababu ya udhaifu wa Mahakama hiyo kuwakubalia kila kitu.

Amerejea hoja alizotoa Julai 15, 2025 kwa ombi la Jamhuri la ahirisho kwa baadhi ya kesi alizozinukuu siku hiyo ikiwamo ya Yahya Upanda kwamba, Mahakama ilisema Mahakama zisije zikajiruhusu kuendeshwa na mawakili wa Serikali.

Hata hivyo, amedai Mahakama hiyo imekubali kutumiwa vibaya na mawakili wa Serikali, jambo ambalo si sawasawa.

Vilevile amerejea nukuu za sheria kwamba, wakishakamilisha yale  waliyosema yamekamilika, upelelezi na jalada kutolewa maoni ya kisheria na kuamua kuwa ushahidi, unatosha kumshtaki mshtakiwa; kwa mujibu wa kifungu cha 262 (6) cha CPA Marejeo ya 2023, kinachofuata ni kupeleka taarifa Mahakama Kuu.

Hivyo, Lissu amesema upande wa mashtaka haurudi tena mahakamani hapo kuomba ahirisho bali kusoma maelezo hayo.

“Kama ulivyosema tuje tumejiandaa, mimi nimekuja nimejiandaa, nina statement (maelezo) ya kurasa 102 za maelezo yangu kwa mambo yao, nimejiandaa kama ulivyoamuru, wao wanakuja kukwambia ahirisho…, ahirisho ili uwakubalie kama ambavyo umewakubalia mara zote,” amesema Lissu.

“Kuna collusion (ushirikiano) na Mahakama. Kama hakuna collusion, kama hakuna njama za kuendelea kuniweka mahabusu ili wapange mambo yao ya uchaguzi, wakatalie for once (angalau kwa mara ya kwanza). Thibitisha kwamba, Mahakama yako iko huru…, haiendeshwi na mawakili wa Serikali.”

Amesema kwa mujibu wa Kanuni za Kulinda Mashahidi ambazo amepata nakala yake hata zipambwe namna gani, lakini athari zake ni kuficha mashahidi kwa kuwa hawataonekana, kwani watakuwa katika kizimba maalumu ambako hata Mahakama haitawaona wakati wakitoa ushahidi.

Lissu amesema kwa kanuni hizo, licha ya kwamba mashahidi hao hawataoneka lakini pia majina na taarifa zao nyingine muhimu zitafichwa, sawa na utaratibu wa Waingereza uliojulikana kama Star chamber court ambao mtu anashtakiwa na kutolewa ushahidi na watu wasiojulikana, zilizofutwa mwaka 1641.

“Nina ushahidi hapa kuna watu 27 wamehukumiwa kifo hawajawahi kuona shahidi hata mmoja akitoa ushahidi dhidi yao,” amedai Lissu.

“Na mimi kesi yangu adhabu yake ni kifo. Itabidi Mahakama ya Rufaa ituambie kama hizi Kanuni za Jaji Mkuu George Masaju ni kanuni halali kwa mujibu wa Katiba yetu, kabla hamjaruhusu kuona shahidi yeyote.”

Amedai kwa kuwa upande wa mashtaka haujatekeleza maelekezo yake (hakimu) basi asiwakubalie tena kutoa ahirisho, bali wawasilishe taarifa waliyoelekezwa waisome mahakamani hapo kisha waende kukabiliana Mahakama Kuu.

“Kwa hiyo usipowakubalia, ukiwakatalia what is the option (nini cha kufanya). Leo nimekuja na kesi ya Abdallah Kondo iliyoamuliwa na Mahakama ya Rufaa. Ili Mahakama isichezewe na mawakili wa Serikali wazembe wanarefusha mashauri bila sababu, Mahakama ya Rufaa ilisema Mahakama yako ikichoka na maahirisho, ikikataa maahirisho ifute kesi. Kwa hiyo, nakuomba kwa heshima ya Mahakama hii, usiwakubalie kuahirisha.”

Akijibu hoja hizo, wakili Katuga amedai wakati Lissu anasoma kifungu cha 262 amekisoma kwa jumla wake, lakini kifungu hicho kina mazingira mbadala na kwamba, hakuirejesha Mahakama katika kifungu cha 194 cha CPA ambacho kinaruhusu ulinzi wa mashahidi.

Amedai kifungu cha 262 kinaelekeza taarifa ya kesi iwasilishwe Mahakama Kuu sambamba na maelezo ya mashahidi, basi huwezi kuwasilisha kwanza taarifa hiyo halafu ndipo uombe ulinzi wa mashahidi.

Kuhusu Kanuni za Ulinzi wa mashahidi amedai Mahakama hiyo si sehemu ya kupinga kanuni hizo na kwamba, sheria zipo wazi kama anaona zinamuathiri.

Wakili Katuga amedai Mahakama inapaswa kuheshimiwa kwa kuwa ndiyo imepewa mamlaka ya Kikatiba kuamua kesi na kwamba, katika kuiheshimu  kuna lugha za staha.

Amesema licha maandiko aliyoyarejea Lissu, katika kulinda Mahakama ndiyo maana kikatungwa kifungu cha 114 (k).

Katuga amedai kuwa,  kuiita Mahakama dhaifu kwa sababu tu ya kuahirisha kesi na kwamba Mahakama inachangia yote aliyoyalalamikia wakati inaamua kwa sheria, ni kutokuiheshimu Mahakama.

“Kama huridhiki na Mahakama ya chini, kuna taratibu, sifungi darasa la kufundisha. Tunaamini chochote ulichokiamua ni kwa mujibu wa sheria, Mahakama yako ilikuwa ikialikwa na Jamhuri na haujaahirisha, haujaamua chochote kwa utashi wako,” amesema Katuga.

Amesema suala la kuahirisha kesi ni la kisheria na maombi ya kulinda mashahidi yako kisheria.

Vilevile, amesema Mahakama hiyo ya chini haiwezi kuielekeza Mahakama Kuu cha kufanya kwa kuwa, uamuzi wa Mahakama Kuu unazifunga Mahakama za chini zinazopaswa kuufuata.

Katuga amesema Mahakama Kuu imeshatoa uamuzi kuwa, uamuzi wa maombi ya kulinda mashahidi utatolewa Agosti 4, 2025 hivyo, Mahakama hiyo haina mamlaka ya kuiamuru Mahakama Kuu vinginevyo, hivyo hawana budi kusubiri mpaka tarehe hiyo ili watekeleza kile itakachokiamua.

Katuga amesema kuwa, madai mengine anayoyatoa mshtakiwa ni kwa ajili ya kutafuta huruma ya Mahakama.

Hoja kuwa Mahakama hiyo haijawahi kuunyima upande wa mashtaka unachokiomba, Katuga amesema chochote Jamhuri inachokiomba ni kwa mujibu wa sheria na si kwa huruma.

Kuhusu hoja ya Lissu kwamba kesi ifutwe, amedai mashauri aliyoyanukuu ni tofauti na kesi hiyo na kwamba, amerudia na kusisitiza hoja zake za awali kuwa, ni jambo la ajabu mshtakiwa ndiye anaomba apelekwe Mahakama Kuu badala ya upande wa mashtaka.

Hakimu Kiswaga baada ya kusikiliza hoja za pande zote ameahirisha kesi hiyo hadi Agosti 13, 2025 kwa ajili ya uamuzi wa hoja za ahirisho la kesi.