Mama aliyemchoma mwanaye kwa petroli jela miaka saba

Geita. Mahakama ya Wilaya ya Geita imemuhukumu kifungo cha miaka saba jela, Devotha Nestory baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kumshambulia mwanawe kwa kumchoma moto kwa kutumia mafuta ya petroli na kumsababishia ulemavu wa kudumu.

Hukumu hiyo imetolewa leo Julai 30, 2025 na Hakimu Mwandamizi, Bruno Bongole baada ya kusikiliza ushahidi wa mashahidi 10 akiwemo mtoto aliyejeruhiwa na mama yake mzazi.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Desemba 2, 2024, katika kijiji cha Kasota kilichopo Wilaya ya Geita, mshtakiwa alimchoma moto mtoto wake, Daud Nestory (9), kwa kumwagia petroli akimtuhumu kuiba Sh6,000, tuhuma ambazo baadaye zilithibitishwa kuwa si za kweli baada ya fedha hizo kupatikana kwenye begi la dada yake.

Imeelezwa mahakamani hapo kuwa Devotha alimchapa mtoto huyo, kisha akamfungia ndani, akaenda kununua petroli na aliporudi alimwagia na kumchoma moto.

Devotha Nestory akitoka kwenye chumba cha Mahakama Wilaya ya Geita baada ya  kuhukumiwa kwenda jela miaka saba kwa kosa la kumshambulia mwanae kwa kumwagia petrol na kumchoma moto.

Mtoto huyo alikimbia nje akiwa anaungua kisha kuanguka chini, na kuokolewa na jirani aliyesaidia kuzima moto.

Ripoti ya daktari iliwasilishwa mahakamani ikionyesha kuwa mtoto huyo aliungua kwa asilimia 20 ya mwili wake, akipata madhara makubwa shingoni, mikononi na miguuni, hali iliyosababisha ulemavu wa kudumu.

Katika utetezi wake, mshtakiwa amekiri kutenda kosa hilo lakini amedai hakulenga kumchoma mwili wote, bali mikono tu.

Pia, ameiomba huruma ya mahakama akieleza kuwa ni mama wa watoto saba, wakiwemo watatu wadogo, mmoja akiwa na umri wa miaka miwili.

Hata hivyo, Hakimu Bongole amesema pamoja na utetezi huo, kitendo alichofanya hakiwezi kufanywa na mtu mwenye akili timamu.

“Mahakama imejiridhisha na utetezi na kitendo hicho hakiwezi kufanywa na mtu mwenye akili hata kama ulikuwa unamuadhibu, kitendo cha kumchapa kisha ukamfungia ndani ukaenda kununua petroli ukaja kumchoma moto, hiki sio kitendo cha kibinadamu.

“Ukiwa hapa mahakamani ulijitetea toka umezaa hujawahi kumuona baba yake hii sio sababu ya kumchukia mtoto kwa kuwa yeye pia hakuwaambia mumzae, ila wewe umehamisha hasira za baba kwa mtoto,” ameongeza.

Kwa upande wa Jamhuri, Wakili Deodatha Dotto ameiomba Mahakama itoe adhabu kali ili iwe fundisho, akieleza kuwa hawakuwa na kumbukumbu ya makosa ya nyuma ya mshtakiwa, lakini kwa ukatili alioufanya dhidi ya mtoto wake, apewe adhabu stahiki.

Aidha, Hakimu Bongole amesema Mahakama imejiridhisha kuwa mshtakiwa alidhamiria kutenda kosa hilo, na adhabu ya kifungo cha miaka saba jela inastahili kama funzo kwa wazazi wengine wanaojihusisha na adhabu kali zisizo za kibinadamu kwa watoto.

Mahakama pia imeamuru mtoto aliyefanyiwa ukatili kubaki kwenye kituo cha malezi ya watoto, chini ya uangalizi wa Serikali, ili aendelee kupata matibabu ya upasuaji na elimu, hadi pale atakapokuwa mtu mzima anayeweza kujitegemea.

Aidha, imeelekeza Idara ya Ustawi wa Jamii kufuatilia hali ya watoto wengine waliobaki nyumbani kwa mama huyo, na iwapo mazingira yatabainika kuwa si salama, nao wachukuliwe na kuwekwa kwenye kituo cha malezi.