Dar es Salaam. Watu wanne wakiwemo maofisa wa benki ya Equity Tanzania Limited, wamefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka saba yakiwemo ya kutakatisha fedha na wizi wa Sh4.4 bilioni mali ya benki hiyo.
Wakili wa Serikali, Tumaini Mafuru amewataja washtakiwa hao ni Jasmine Fredrick Elphas ambaye ni ofisa wa benki ya Equity makao makuu pamoja na baba yake, Fredrick Elphas Ogenge, ambaye sio mfanyakazi wa benki hiyo.
Wengine ni Caroline Masayanyika na Lilian Koka, wote ni maofisa wa benki hiyo kutoka makao makuu.
Washtakiwa hao wamefikishwa mahakamani hapo, leo Jumatano Julai 30, 2025 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi namba 18447 ya mwaka 2025.
Elphas na wenzake, wamesomewa mashtaka yao mbele ya hakimu Mkazi Mfawidhi, Franco Kiswaga.
Kabla ya kuwasomewa mashtaka hayo, Hakimu Kiswaga amesema washtakiwa hawatakiwi kujibu chochote mahakamani hapo kwa sababu mahakama ya Kisutu, haina uwezo wa kusikiliza kesi za uhujumu uchumi isipokuwa kwa kibali maalumu.
Pia mashtaka ya kutakatisha fedha yanayowakabili hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.
Baada ya kutoa maelezo hayo, wakili Mafuru aliwasomea mashtaka yao washtakiwa hao.
Katika shtaka la kwanza, washtakiwa kwa pamoja wandaiwa kati ya Agosti 30, 2024 na Juni 28, 2025 ndani ya Jiji la Dar es Salaam, waliongoza genge la uhalifu kwa lengo la kuiba.
Inadaiwa katika kipindi hicho, washtakiwa kwa makusudi waliongoza genge la uhalifu kwa kuiba fedha katika benki ya Equity Tanzania Limited.
Shtaka la pili ni la wizi na linamkabili mshtakiwa wa kwanza na wapili(Jasmine na Ogenga) ambapo wanadaiwa kati ya Agosti 30, 2024 na Juni 28, 2025 makao makuu ya benki hiyo yaliyopo Ilala, waliiba fedha taslimu Sh3.68 bilioni kutoka katika akaunti namba 3000110010220 yenye jina la Clearing and Settlement Account, mali ya benki ya Equity Tanzania Limited.
Shtaka la tatu ni wizi na linamkabili mshtakiwa Masayanyika pekee yake, ambapo anadaiwa katika tarehe hizo, makao makuu ya benki hiyo iliyopo Ilala, mshtakiwa anadaiwa kuiba fedha kiasi cha Sh728.97 milioni kutoka katika akaunti namba 3000110010220 yenye jina la Clearing and Settlement Account, mali ya benki hiyo.
Shtaka la nne ni wizi na limakabili mshtakiwa Elphas, Ogenga na Koka, ambapo katika tarehe hizo na eneo hilo, kwa pamoja wanadaiwa kuiba fedha Sh26.22 milioni kutoka katika akaunti hiyo, mali ya benki hiyo.
Shtaka la tano, sita na saba ni utakatishaji wa fedha linalowakabili washtakiwa wote, ambapo wanadaiwa katika kipindi hicho na eneo hilo, walijipatia fedha kiasi cha Sh4.43 bilioni wakati wakijua fedha hizo ni mazalia ya zao tangulizi la wizi.
“Upelelezi wa kesi hii bado unaendelea, hivyo tunaomba mahakama itupangie tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa” alidai Wakili Mafuru.
Hata hivyo, wakili wa utetezi Dickson Sigara anamtetea mshtakiwa Elphas na Ogenga pamoja na wakili Mganyizi Godwin anayemtetea mshtakiwa Msayanyika na Koka, waliomba upande wa mashtaka ukamilishe upelelezi kwa wakati kwa kuwa wateja wao hawana dhamana.
Hakimu Kiswaga baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote mbili, ameahirisha kesi hiyo hadi Agosti 11, 2025 itakapotajwa.
Washtakiwa wamepelekwa rumande kutokana na mashtaka ya kutakisha fedha yanayowakabili hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.