Mbeya City yazidi kujiimarisha yambeba Kelvin Kingu

BAADA ya kumalizana na Ame Ally akitokea Mashujaa, uongozi wa Mbeya City umemuongezea nguvu mkongwe huyo kwa kunasa saini ya beki wa kati, Kelvin Kingu Pemba kutoka Tabora United kwa mkataba wa mwaka mmoja.

Msimu uliopita Pemba alikuwa na kiwango bora sana akiwa na nyuki wa Tabora, lakini klabu hiyo imeshindwa kumbakisha akitimkia Mbeya City iliyopanda daraja kushiriki Ligi Kuu Bara msimu ujao.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Mbeya City kimeliambia Mwanaspoti kuwa wameamua kuongeza nguvu eneo hilo ili kuendelea kuimarisha safu yao ya ulinzi malengo yao ni kuwa na timu shindani msimu ujao.

“Ni kweli tumemalizana na beki huyo, ataungana na Ame ambaye tayari tumemtambulisha, lengo ni kuongeza nguvu na kuwa na kikosi kipana ambacho kitatoa ushindani kwenye Ligi Kuu msimu ujao.

“Tumetoka kucheza Championship nguvu nyingi imetumika ni wakati sahihi dirisha hili kuongeza nguvu ili kujiweka kwenye nafasi nzuri ya ushindani hatutarajii kufanya makosa msimu ujao.”

Chanzo hicho kilisema bado wanaendelea kufanya usajili ili kuboresha timu yao na wanaamini wachezaji waliowaongeza watakuwa chachu ya ushindani kutokana na uzoefu walionao.

Katika utambulisho wa nyota huyo, Mbeya City ilisema: “Karibu Purple Nation. KINGU KELVIN PEMBA.”

Pia klabu hiyo imeendelea kuboresha kikosi kwa kuwaongezea mikataba baadhi ya nyota walioipandisha timu hiyo akiwamo Eliud Ambokile, Memory Pillar na Baraka Maranyingi.