Ilianza kwa mgombea wa urais kupitishwa mapema zaidi ya nyakati zote katika historia ya Chama cha Mapinduzi (CCM), ikafuata kusogezwa mbele kwa ratiba ya uchukuaji na urejeshaji fomu za ubunge, uwakilishi na udiwani.
Katikati ya hayo yote, ikachapishwa ratiba iliyohusisha kalenda ya matukio kuanzia vikao vya kata, wilaya, mikoa hadi Taifa kwa ajili ya mchujo wa wagombea, lakini baadaye ikavurugika.
Kama hiyo haitoshi, ndani ya miezi saba, ikafanyika mikutano mikuu ya Taifa mitatu, iliyokuwa na ajenda tofauti, kati hiyo mmoja ulifanyika kwa njia ya mtandao. Haijawahi kutokea.
Vikao vya mchujo vikaketi, kutwa moja haikuvitosha kumaliza kazi zake. Mathalan, kikao cha kamati ya usalama na maadili kilianza mapema asubuhi ya Julai 27, 2025 na kutamatika saa 9 usiku wa Julai 28, 2025.
Kamati Kuu nayo, pamoja na mchujo kupitia vikao kadhaa vya awali, chenyewe kilichoanza saa 4 asubuhi ya Julai 28, kilitamatika saa 3 usiku.
Hata hivyo, muda huo haukumtosha Katibu wa Halmashauri Kuu, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla kuweka hadharani orodha ya waliopendekezwa, licha ya kuwaalika wanahabari waliokaa saa zaidi ya 10 usiku wa manane bila taarifa hiyo kutolewa na hatimaye ikaahidiwa saa 4 asubuhi ya Julai 29.
Huo ni mfululizo wa machache kati ya matukio mengi ya pekee, yaliofanywa na CCM katika michakato ya ndani ya kuwapata wagombea wa ngazi mbalimbali. Kwa maneno mengine unaweza kusema ni uchaguzi ndani ya uchaguzi.
Ni uchaguzi ndani ya uchaguzi, kutokana na uhalisia wa milolongo inayopitiwa na chama hicho, ikiongeza hofu, wasiwasi na kuteka hisia za wengi, kiasi kwamba kinafuatiliwa utadhani ndio uchaguzi wenyewe.
Ushindani uliopo ndani ya michakato hiyo, ndio unaosadifu mitazamo ya wadau wa siasa kuwa, ni mwaka wa uchaguzi ndani ya uchaguzi, kwa sababu inahusisha purukushani nyingi ndani na hata nje ya chama hicho.
Inawezekana yanayoshuhudiwa, yanatokana na idadi kubwa ya watiania na pengine wengi wazuri, hivyo inaweka ugumu wa kuamua yupi apitishwe na yupi aachwe, kama inavyoelezwa na Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Ajali Nguyuhambi.
Mwanazuoni huyo anasema kwa upande mwingine, pengine, watiania wengi ni wale waliojitokeza kuonyesha sura zao, lakini hawana dhamira ya dhati ya kuwa wabunge au wawakilishi, hivyo kamati inaongeza umakini isikosee kuwapitisha.
Katika siku za karibuni, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla alisema zaidi ya makada 10,000 wamejitokeza kuomba nafasi ya ubunge na uwakilishi.
Sababu nyingine ya purukushani zinazoshuhudiwa ikiwamo vikao kuchukua muda mrefu au kubadilishiwa ratiba, anasema ni uhalisia wa vitendo vya uvunjifu wa maadili vilivyosikika mara kadhaa, hivyo umakini wa vikao unaongezeka.
Hata hivyo, kuchelewa kumalizika kwa vikao hivyo, anasema kunaashiria vikao vya ngazi za chini havikuwa na umakini wa kutosha kiasi cha kuvisaidia vikao vya juu kufanya uamuzi kwa urahisi zaidi.
“Mwisho wa siku ni kutafuta wagombea ambao chama kinadhani hakitaangushwa,” anasema Dk Nguyuhambi.
Kwa upande wake, Mchambuzi wa Masuala ya Siasa na Uongozi, Dk Revocatus Kabobe anasema mwaka huu imeshuhudiwa michakato ya ndani ya CCM ikiibua mvuto mkubwa wa kisiasa, kiasi kwamba imeonekana kama uchaguzi ndani ya uchaguzi.
“Hali hii si ya kawaida kwa kiasi, na ina sababu kadhaa za msingi zinazoweza kuelezea kwa nini mambo yamekuwa namna hii,” anaeleza.
Anasema kinachoshuhudiwa ni ishara kwamba CCM ina nguvu kubwa katika siasa za Tanzania. Kushinda uteuzi wa ndani ya chama hicho, mara nyingi huwa na maana kubwa ya kushinda uchaguzi halisi, hasa katika maeneo ambayo upinzani hauna mizizi imara.
“Hivyo, ushindani mkali unaonekana katika hatua za awali kabisa kabla hata ya wananchi kupiga kura,” anasema.
Jambo lingine, anasema kinashuhudiwa ni ishara kwamba upinzani nchini kwa sasa uko katika hali ya udhaifu wa kimkakati au kimuundo. Kwa hiyo, ushindani mkubwa wa kisiasa umehamia ndani ya CCM.
“Matokeo yake ni kwamba michakato ya ndani ya chama inakuwa kama uwanja mkuu wa mapambano ya kisiasa, badala ya kuwa kwenye uchaguzi mkuu au wa kata, majimbo kwa maana ya vyama pinzani kushindana na CCM,” anasema Dk Kabobe.
Dk Kabobe anasema kwa miaka ya karibuni, CCM imeongeza hatua mbalimbali kwenye mchakato wa uteuzi, ikiwamo usaili, vikao vya mchujo, vikao vya kamati za siasa, uamuzi wa halmashauri kuu na vingine.
Anaeleza kila hatua ina nafasi ya ushawishi na hivyo kuibua sintofahamu, mihemko, mara vikao vya usiku wa manane.
“Mambo haya yote yanaongeza mvuto na mara nyingine mkanganyiko kwa wananchi na vyombo vya habari,” anasema.
Anasema katika dunia ya sasa, habari huenea haraka. Mitandao ya kijamii imekuwa jukwaa kuu la mijadala ya kisiasa.
Kutokana na hilo, anasema kila hatua ya ndani ya chama, iwe ni malalamiko, matokeo ya mchujo, au mabadiliko ya tarehe, hutangazwa na kuchambuliwa kama habari kubwa.
“Hili nalo limechangia sana kufanya mchakato wa ndani wa CCM kuonekana kama uchaguzi kamili,” anasema.
Mchambuzi wa Masuala ya Siasa, Dk Faraja Kristomus anasema mchakato wa ndani ya CCM kwa mwaka huu ni mkubwa na ni kama wanakamilisha uchaguzi mkuu kwa sababu hakutakuwa na ushindani mkubwa kutoka vyama vya upinzani.
“Atakayepita kwenye mchujo huu na ule wa wajumbe mashinani atakuwa ana nafasi kubwa ya kuwa mbunge ukizingatia chama kikuu cha upinzani nchini kimefungwa mikono na miguu na hakiwezi kushiriki uchaguzi huu,” anasema.
Naye, Dk Faraja Kristomus, mchambuzi wa masuala ya siasa, anasema mchakato wa ndani ya CCM kwa mwaka huu ni mkubwa na ni kama wanakamilisha uchaguzi mkuu kwa sababu hakutakuwa na ushindani mkubwa kutoka vyama vya upinzani.
“Atakayepita kwenye mchujo huu na ule wa wajumbe mashinani atakuwa ana nafasi kubwa ya kuwa mbunge ukizingatia chama kikuu cha upinzani nchini kimefungwa mikono na miguu na hakiwezi kushiriki uchaguzi huu,” anasema.
Mbali na mitazamo hiyo ya wanazuoni, imejengeka dhana kwamba mshindi wa kura ya maoni ndani ya CCM ndiyo ana nafasi zaidi ya kushinda ubunge kwenye uchaguzi mkuu unawashindanisha na wagombea wengine wa upinzani.
“Ukiona mpinzani ameshinda, basi ujue kuna nguvu kubwa ya umma imetumika kuhakikisha anatangazwa. Bila hivyo, CCM wanawapambania watu wao kwa gharama yoyote, tuliona uchaguzi wa 2020 na 2024,” anasema Emmanuel Funga, mkazi wa Tabata.
Kwa upande wake, kada wa CCM, John Mengo anasema uchaguzi ndani ya chama hicho ni mkali kwa sababu kina watu wengi wenye sifa, hivyo wanapokutana wengi, kazi inakuwa nguvu ya kuwachuja ili kupata mmoja mwenye sifa zaidi.
“Upinzani hauna nguvu mbele ya CCM, shughuli ipo huku ndani. Nafasi moja mnagombea watu watano, halafu unakuta kila mmoja ana CV iliyoshiba, unafanyaje? Ukiangalia huku nje wapinzani wazuri ni wachache, mnashinda kirahisi tu,” anajigamba kada huyo.