MNIKWAMBIE MAMA: Mtuletee wagombea wenye sifa ya ubunifu

Endapo utaona tone la mvua likiangukia sofani, utashikwa na hofu ya kuharibika kwa sofa hilo. Utatupa macho juu kuona panapovuja na kukutana na alama kwenye dari.

Utaweka ngazi na kuparamia darini ambako utagundua kigae kilichovunjika. Usipoangalia utajikuta ukirudi chini na kuinamisha kichwa: kadha imekuwa kadha wa kadha! Namna hii ndiyo ambayo matatizo huitumia kumchanganya mwanadamu.

Katika siku za karibuni, tumekumbwa na jinamizi la Watanzania kujinyonga kwa mlipuko. Tofauti na nyakati zilizopita, watu sasa wamepoteza hofu ya kufanya maamuzi magumu. Inashangaza kuona mabadiliko makubwa kutoka kwenye kuuana hadi kujinyonga. Ingawaje yote mawili ni ya haramu, lakini kujinyonga kuna kitisho za ziada.

Kwenye pande fulani za imani, mwili wa mtu aliyejinyonga haupewi nafasi ya kuingizwa kwenye nyumba ya ibada kwa ajili ya maombezi.

Ili tupambane, ni lazima tujue nini hasa kiini cha jinamizi hili. Kila taarifa mpya inapozuka hutaja “wivu wa mapenzi”. Tatizo hili si jipya, lipo tangu enzi na enzi. Hapo kabla tulisikia watu wakidhuriana au kuteketezeana nyumba kwa sababu hizo. Ni kitu gani kilichowabadili ghafla hata wakahamia kwenye utaratibu huu wa kujinyonga? Bila shaka nyuma ya pazia kuna jambo la ziada.

Kujinyonga ni hatua ya mwisho kabisa ya kufanya maamuzi hatarishi. Mtu angeweza kuteketeza umati wa watu kwa nia ya kulipa kisasi na kuuridhisha moyo wake. Angekuwa tayari kuuawa na akajisifia kuwa “amekufa vitani”.

Au angeweza kuhukumiwa kifungo cha maisha na pengine hata kunyongwa, nafsi yake ikaridhia kuwa anakwenda huko bila kinyongo, woga wala majuto.

Ni kwa nini basi mtu mwenye akili timamu anafikia kujinyonga? Muda mfupi kabla hajachukua uamuzi kama huo alikuwa akiwalaani wote waliofanya kitendo hicho.

Alishangaa mtu anauachaje wingi wa madawati ya ushauri, taasisi za kidini na za kiserikali zilizo tayari kumsikiliza na kumshauri kwa unasaha. Lakini ilipofika zamu yake, aliwakwepa wote waliojaribu kumshauri na kuwaona kuwa adui zake.

Ni vigumu sana kupigia mstari jambo moja kama sababu ya kujinyonga. Kwa mfano kila mmoja anajua kwamba wivu wa kimapenzi ni matokeo ya mmoja ya walio kwenye mahusiano kuchepuka. Yule aliyetendwa ataumia, lakini apende au asipende ni lazima akubali matokeo na kufanya maamuzi. Aidha asamehe, au aachie ngazi. Hakuna namna ingine kwa sababu janga linakuwa limeshatokea.

Iwapo wivu huu ungelikuwa unalazimisha watu kujitoa uhai kila unapotokea, wasamehevu wangelikuwa wachache sana. Tusingeweza kuhesabu wanaojinyonga kila siku bila idadi katika janga hili. Lakini katika mifumo ya kawaida ya binadamu, husameheana mara saba mara sabini na maisha yakaendelea. Wengine hutalikiana na kusahauliana kama wanavyosahau kifo. Hilo linadhihirisha kuwa wivu wa mapenzi ni kisingizio tu cha watu kujinyonga. Nasema hivyo kwa sababu jinamizi la kujinyonga linakwenda sambamba na mauaji ya wivu wa biashara, ugumu wa maisha na changamoto ya afya ya akili. Ukiyajumlisha haya unaweza kupata sababu ya Watanzania kuchanganyikiwa. Juzijuzi kuna mama mmoja amewachinja watoto watatu wa mke mwenza, sababu ni mume kutumia muda mrefu na mke mdogo kuliko anavyoutumia kwake yeye mkubwa wake.

Mimi nafikiri changamoto ya afya ya akili ndio kichwa cha habari kwenye matatizo haya. Changamoto hii huweza kuibuka kirahisi kwa mtu aliye ndani ya shida. Shida humwandama yeyote asiye na kipato cha uhakika. Pale anaposhindwa kuendesha mahusiano yake, kulipa kodi, kulipa ankara za lazima, kulisha na kusomesha familia. Akifikia hapo, mtu yeyote hata awe nduli kiasi gani atalegea. Fanyeni tathmini ya wastani wa matukio baina ya nchi tajiri na masikini na watu wenye utofauti wa kipato. Mtaona kuwa masikini wengi wanajinyonga kutokana na matatizo ya kifamilia, wakati matajiri wanajinyonga baada ya biashara zao kuyumba na kuonesha dalili za kufilisika.

Lakini wote wanawekwa kwenye kapu moja linalosomeka “wivu wa kimapenzi”, ni kwa kuwa upana wa sababu halisi hauwezi kusomeka kwa mara moja. Mtanzania wa kawaida huweza kupatwa na msongo haraka pale anapoandamwa na shida.

Huona vigumu kuomba usaidizi kwa sababu bado hajaona vielelezo vya waliowahi kusaidiwa wakasaidika. Kwa mfano masikini wanaweza kusaidiwa vipi iwapo hata wasomi wanakosa vibarua. Matajiri nao huyumba pale biashara zao zinapoyumba, na haoni ni namna gani TRA wanaweza kumsaidia kuinuka kibiashara. Mambo yanayopangwa na binadamu huweza kurekebishwa kibinadamu. Serikali iingie kazini kurekebisha hali za maisha ya wananchi haraka sana. Imalize vita ya wafanyabiashara na TRA, iwawezeshe wamachinga mitaani kwa mikopo nafuu ya ujasiriamali na elimu ya ufundi, na isisitize elimu ya kujitegemea toka shuleni. Jambo hili lianze kufanyika kwa dharura kama mapambano na ajali ya moto.

Wakati huu tunapoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu 2025, mtuletee wagombea wabunifu wanaoweza kuchonga njia mbadala. Viongozi walioishiwa husubiri msimu mpya uanze watuletee mistari mingine watakayoikariri.