Dar es Salaam. Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango ametoa maagizo saba kwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Taasisi za Serikali, likiwemo la kudhibiti mikopo inayotolewa mitandaoni kinyume na taratibu huku ikingilia faragha za watu.
Mikopo hiyo ambayo mara nyingi huwa ni migumu kulipika kutokana na riba kubwa na masharti magumu, imekuwa ikitajwa kuwa chanzo cha kufilisika, kujiua, kuvunjika kwa ndoa na kupata magonjwa ya akili baada ya wakopaji kushindwa kuilipa kutokana na masharti magumu.
Mikopo hiyo ambayo imepachikwa majina mengi ikiwemo kausha damu, komandoo, pasua moyo, kichefuchefu, imekuwa ikitajwa kuwa chanzo cha kufilisika, kujiua, kuvunjika kwa ndoa na kupata magonjwa ya akili baada ya wakopaji kushindwa kuilipa kutokana na masharti magumu.
Mbali na hilo, pia ameagiza BoT kuongeza matumizi ya malipo kidijitali ili kuondoa matumizi ya fedha taslimu, kulinda mifumo ya kifedha, kutangaza maktaba na makumbusho za BoT na kuwezesha ubunifu wa ndani.
Dk Mpango ametoa maagizo hayo leo Julai 30, 2025 wakati akizindua Mfumo mkuu jumuishi wa Huduma za Kibenki (iCBS), uliotengenezwa na BoT ukiunganisha watoa huduma wa sekta ya fedha.
Dk Mpango amesema siku za hivi karibuni limeibuka wimbi kubwa la wakopeshaji kupitia mitandao ya simu ambao wamejipa majina mbalimbali, ambao licha ya kutotambuliwa kisheria, wamekuwa wakiendesha shughuli zao bila kufuata taratibu za ukopeshaji.
Amesema watu hao wamekuwa wakitoa riba kubwa, kuingilia faragha za watu na kusambaza taarifa za wakopaji bila ridhaa yao.
“Kupitia hadhara hii ninavionya vikundi hivyo viache mara moja shughuli hizo kwa kuwa ni kinyume na sheria na ninaiagiza Benki Kuu ya Tanzania kulitupia jicho suala hili, ili kuwahakikishia wananchi wetu ambao wengi ni wakopaji wadogo hawaendelei kutapeliwa,” amesema.

Kauli hiyo imekuja wakati ambao kumekuwa na malalamiko ya watu juu ya taarifa zao kutumiwa vibaya na kampuni za mikopo ikiwemo kutuma ujumbe kwa watu wao wa karibu kuwa wanadaiwa.
Hiyo imeenda sambamba na riba za mikopo hiyo kuwa kubwa kiasi cha kufanya wakopaji kulazimika kulipa fedha nyingi kuliko kiwango walichokopa.
Ili kukomesha hilo, ameitaka BoT kuendelea kutoa elimu kwa umma juu ya athari za kurubuniwa na matapeli hao mitandaoni na kuwaonyesha fursa sahihi za kupata mikopo katika benki zilizopo.
Tayari, BoT inaendelea na kampeni mbalimbali mitaani ili kuwaelimisha wananchi kuhusu ukopaji sahihi na namna wanavyoweza kuepuka mikopo umiza ili wawe salama.
Mbali na hilo, ameitaka BoT kwa kushirikiana na taasisi za usimamizi wa mawasiliano na wizara zinazohusika kusimamia mfumo wa iCBS na mingine ya malipo, ili itoe matokeo stahiki katika maendeleo ya uchumi.
“Pia nasisitiza kujikita katika matumizi ya sahihi ya mifumo kidijitali katika kufanya miamala na malipo, ili kupunguza matumizi ya fedha taslimu kwani kufanya hivyo kuna manufaa katika uchumi wa mtu mmoja mmoja, taasisi na taifa kwa ujumla,” amesema.
Ili kufikia azma hiyo ameiagiza BoT kuongeza kasi ya Taifa kuhamia katika malipo ya uchumi wa kidijitali na kupunguza matumizi ya fedha ya kidijitali huku wakienda sambamba na ulinzi wa mifumo hiyo dhidi ya uhalifu wa kimtandao.
Dk Mpango alitumia nafasi hiyo kutaka wabunifu wa ndani kuendelezwa na kuwatumia katika ujenzi wakati ambao Serikali itaendelea kuchukua hatua za kuimarisha utafiti na ubunifu kwa kuongeza fedha, kuanzisha vituo vya ubunifu na atamizi na kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za elimu ya juu, Serikali na sekta binafsi
Ulinzi wa hakimiliki wa mfumo huo nalo ni jambo alilisisitiza kwani itasaidia kukuza utamaduni wa ubunifu nchini, sambamba na kuongeza motisha kwa wabunifu wa ndani ambao wana mchango mkubwa katika kuokoa fedha za kigeni na kuongeza tija kwa ujumla.
“Pia kuhusu mifumo ya Serikali kusomana ni hatua muhimu kufikia azma ya Serikali ya kuunganisha mifumo, taasisi zote za Serikali zizingatie maelekezo haya mahsusi na wasiotekeleza unajua kwa kwenda ili watekeleze,” amesema.
Amesema mfumo wa iCBS ni mwanzo wa zama mpya za kuendesha benki, hasa katika kupata taarifa papo kwa papo na wakati halisi, ikiwa ni mafanikio muhimu yanayounga mkono jitihada za Serikali zinazoelekea katika kujenga mfumo wa kisasa unaoimarisha uwezo wa kukusanya taarifa za kiutawala ili kufanya maamuzi sahihi kwa wakati.
“Mhakikishe taarifa hizi zinaunganishwa katika mifumo ya kitaifa ya takwimu, ili kuwezesha na kuongeza wigo wa ukusanyaji wa taarifa na kusaidia ujenzi na uhifadhi wa kiasi kikubwa cha takwimu,” amesema.
Pia alitaka makumbusho ya benki kuu na maktaba ya kidijitali yatangazwe kupitia vyombo vya habari ili waliopo shuleni na vyuoni waweze kuchota maarifa hayo huku akiwataka Watanzania kutumia fursa hiyo kikamilifu.
Akielezea mfumo huo, Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba amesema unasimama kama mbadala wa ile uliokuwa ukitumika awali ambao ulikuwa umepitwa na wakati kiteknolojia, ufanisi na uwezeshaji.
Mfumo huo ulikamilika Septemba 2024 na ulianza kutumika kwa majaribio Oktoba mwaka huo, huku kukiwa hakuna changamoto yoyote iliyobainika, jambo lililowasukuma kuuzindua rasmi.
“Umekuwa ni mfumo unaokidhi mahitaji yaliyotarajiwa kwa mazingira ya Tanzania na unaoendana na viwango vya Tanzania. Hali hiyo inaweka urahisi wa kushughulikia changamoto yoyote inapotokea,” amesema.
Mfumo huo umeunganisha mingine ya utoaji huduma za kibenki ndani na nje ya nchi huku ikiifanya BoT kuwa benki kuu ya kwanza Afrika kutengeneza mfumo wa aina hiyo, ikitumia fedha na wataalamu wa ndani bila kutegemea usaidizi wa nje.
Amesema mfumo kama huo ungenunuliwa nje ya nchi ungegharimu Sh91.95 bilioni lakini gharama zote za ndani zilitumika hadi mfumo kuwa tayari ni Sh10.63 bilioni ndiyo zimetumika.
“Pia Sh5 bilioni kila mwaka zimeepukwa ambazo zingekuwa zikitumika katika uhudumiaji wa mfumo huu kila mwaka kama tungenunua nje,” amesema Gavana.
Amesema mfumo huo umesaidia kuboresha utoaji wa taarifa sahihi za Serikali, taarifa za miamala, ufungaji wa hesabu kwenye akaunti za wateja, upatikanaji wa taarifa kwa urahisi kwa wafadhili, usimamizi wa ukwasi na ukokotoaji wa riba za kibenki.
“Pia mfumo huu utasaidia upatikanaji wa taarifa za papo kwa papo, kuondoa makosa ya kibinadamu na kuongeza usahihi wa taarifa na kutoa uwanja mkubwa wa kufanya maamuzi sahihi kutokana na taarifa sahihi zinazopatikana kwa wakati, huku ukiongeza ujumuishi wa watu katika huduma rasmi za kifedha,” amesema.
Naibu waziri wa Fedha, Hamad Chande ameshauri mfumo huo ulindwe ili uwe salama na imara na watanzania wauthamini.
Amesema hayo kutokana na changamoto iliyopo kwa kuwa Watanzania huthamani kwa kiwango kikubwa vitu vinavyotoka nje kuliko vile vinavyotengenezwa nchini.
“Lazima uthamini cha kwako ndiyo maendeleo yako yanapatikana,” amesema Chande.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Dk Saada Mkuya Salum amesema kwa kipindi cha majaribio wameona ufanisi wa shughuli za benki kuongezeka baada ya kuundwa kwa mfumo huo na kuanza kutumika.
Kwa upande wake Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa amesema hadi sasa mifumo 898 ya Serikali na sekta binafsi inasomana na kati yake 14 ni ya sekta ya fedha.
“Kilichofanywa na benki kuu ni jambo kubwa kwani itawezesha sekta nzima ya fedha kuwa sehemu moja,” amesema.