Dar es Salaam. Mbunge wa Kisesa anayemaliza muda wake, Luhaga Mpina ametoa kauli baada ya uamuzi wa kikao cha Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM), kutopendekeza jina lake katika mbio za kuwania ubunge wa jimbo hilo.
Wakati huohuo, Mbunge wa Bumbuli, January Makamba naye ameeleza kuhusu uamuzi huo, huku akigusia kile kinachodaiwa kuwa kuenguliwa kwake kumetokana na nia yake ya kuutaka urais.
Mpina aliyeliongoza jimbo hilo kwa miaka 20 tangu mwaka 2005 na Makamba tangu 2010 ni miongoni mwa wabunge zaidi ya 30 wanaomaliza muda wao, ambao majina yao si miongoni mwa yaliyoorodheshwa kuendelea na mchakato wa kura za maoni wa chama hicho, unaotarajiwa kufanyika Agosti 4, mwaka huu.
Mpina na Makamba pamoja na makada wengine 2,630 wamekatwa kati ya 4,109 waliochukua fomu komba ridhaa ya ubunge wa majimbo 272 ya Tanzania bara na Zanzibar.
Kutokana na hatua hiyo, Mpina na Makamba hawatakuwa wabunge wa majimbo anayetokana na CCM, kama wataipata nafasi hiyo, labda kupitia nafasi 10 za uteuzi ambazo Rais ndiye anayeamua.
Akizungumza na Mwananchi leo, Jumatano Julai 30, 2025, Mpina amesema kwa sababu vikao vya chama chake ndivyo vilivyoamua kuhusu kuendelea au kutoendelea kwake, hana la ziada.
“Nitasema nini wakati tayari chama changu kimeshaamua. Kweli mimi ni mwanasiasa, lakini ndiyo chama kimeamua nitasema nini,” amesema.
Alipoulizwa iwapo ana mpango wa kujiunga na chama kingine kuendeleza siasa, amejibu tayari yupo kwenye jukwaa la CCM, hivyo hana nia na kwingineko.
“Jukwaa si ndio hilo la CCM na vikao vimeamua, jukwaa lingine la nini tena ndugu yangu,” amejibu Mpina, aliyewahi kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi.
Kwa upande wake Makamba, amesema amepokea maelekezo na uamuzi wa kikao kama ilivyo wajibu wa mwanachama na amekubaliana nayo.
“Ukishaamua kuwa mwana-CCM maana yake unajiinamisha kwenye taratibu za chama, maana yake unapokea namna ambavyo utaratibu wa maamuzi ya kwenye chama unafanyika,” amesema.
Kwa kuwa wakati mwanachama anachukua fomu ya kuomba ridhaa ya chama hicho kwa nafasi yoyote, amesema anafahamu kuna kupendekezwa au kutopendekezwa, lolote litakalotokea hivyo anakubaliana na kilichotokea.
“Mimi nimepokea kwa moyo mkunjufu na kama mwanachama ninao wajibu wa kuhakikisha uamuzi wa vikao unatekelezwa,” ameeleza.
Kuhusu madai kuwa amekatwa kwa sababu ana malengo ya kuwania urais, Makamba amesema hizo ni ramli kama nyingine na kwamba mbio za urais zinategemea zaidi mkono wa Mungu.
“Siamini kwamba kuna uhusiano wowote kati ya haya na mambo ya urais. Lakini kwa kifupi tumeyapokea na kule kwetu Bumbuli, uamuzi umetoka tuyapokee maamuzi na tuyakubali na tushirikiane na viongozi wetu kuhakikisha utaratibu wa kupiga kura unakwenda vizuri.
“Kwa sababu ukivurugika inaweza ikajengeka dhana kwamba mbunge aliyekuwepo kaamua kavuruga mambo, kwa hiyo kama mnanipenda jamani toeni ushirikiano jambo liende vizuri,” amesema Makamba ambaye ni mtoto wa Katibu Mkuu wa zamani wa CCM, Yusuf Makamba.
Alipoulizwa changamoto aliyokutana nayo baada ya uamuzi huo wa CCM, Makamba amesema ilikuwa kuwaeleza watoto wake nini kimetokea hasa ikizingatiwa watoto kwa kisasa ‘Gen Z’ wana maswali mengi.
“Ilikuwa changamoto kuwaelewesha watoto kwa sababu watoto wangu mimi hawajui mambo ya siasa,” amesema Makamba.
Changamoto ya pili ambayo amesema ilikuwa ngumu ni kumweleza baba yake, Yusuf Makamba ambaye amesema anaumwa presha.
“Unajua Mzee anasema kadri muda unavyokwenda analisogelea kaburi lake na mzazi anapolisogelea kaburi, anapenda kuwaacha watoto katika mazingira mazuri ya mafanikio.”
“Akipata dhana kwamba kadhalilika anaumia licha amewahi kukutana na kadhia kama hizi huko nyuma,” amesema Makamba.
Makamba amesema amepokea ujumbe mwingi wa simu za mkononi ikiwemo zile anazomuomba kusoma maandiko ya Biblia na Quran.
Ukiacha Mpina wabunge wengine waliokatwa ni Vedasto Manyinyi wa Musoma Mjini na Cecil Mwambe wa Ndanda mkoani Lindi.
Kutokana na uamuzi huo wa kamati kuu, Manyinyi amesema ameamua kupumzika siasa kwa miaka mitano.
Kwa sababu ya umri wake, ameeleza hana kingine cha kufanya kwa wakati huu zaidi ya kupumzika na kuwa mwanachama wa kawaida ndani ya chama chake.
Alipoulizwa iwapo ana mpango wa kutafuta jukwaa lingine la kugombea ubunge, amejibu hana nia hiyo kwa kuwa haoni chama kingine kitakachofaa kwake kuingia bungeni.
“Sasa nitaenda chama gani kingine zaidi ya kubaki CCM. Mimi nitabaki kuwa mwanachama hapa na nitapumzika siasa kwa miaka mitano,” amesema.
Baada ya miaka mitano ya mapumziko, ameeleza huenda akajitosa tena katika mbio za ubunge, iwapo umri na nguvu zikimruhusu kwa wakati huo.
“Nikiona maji yamekuwa ya shingo, basi nitaamua kubaki kuwa mwanachama mtiifu wa muda wote wa chama changu CCM,” amesema.
Mbunge wa Ndanda anayemaliza muda wake, Cecil Mwambe amesema kwa kuwa ameshawahi kufanya siasa za upinzani na anayajua madhara yake, hafikirii kurudi huko.
Ingawa siasa ndiyo shughuli yake, amesema ataendelea kuifanya akiwa ndani ya CCM, huku akisisitiza kwa hatua ya sasa atakuwa mtulivu kama chama chake kinavyotaka.
“Nitaendelea kuwa mtulivu ndani ya CCM. Unajua mimi nilishafanya siasa za upinzani nayajua madhara yake. Sifikirii kurudi nyuma tena,” ameeleza.
Mwambe amesema kwa utumishi wake wa miaka 10 kwa wananchi wa Ndanda ni imani yake ameacha alama zisizofutika na atalazimika kurudi jimboni humo miaka ijayo iwapo ataona kuna ombwe la uongozi.
“Sijapanga wala sijawaza kuhusu 2030, lakini kwa kuwa umri wangu mdogo bado unaruhusu, nikiona kuna uhitaji mwaka 2030 nitaomba ridhaa ya chama changu kisha nitaendelea,” amesema Mwambe.
Mwambe amehudumu Ndanda akiwa Mbunge kwa tiketi ya Chadema, baadaye alijiunga na CCM na kushinda tena kiti hicho.