Mpoki ateuliwa mhariri Mtendaji Mkuu MCL

KAMPUNI ya Mwananchi Communications Limited (MCL), imemteua Mpoki Thomson kuwa mhariri mtendaji mkuu mpya ili kuimarisha mabadiliko ya kihabari kuelekea mfumo wa kidijitali unaoongozwa na ubunifu na ushirikishaji jamii.

Taarifa iliyotolewa jana Jumanne na Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Rosalynn Mndolwa-Mworia ilieleza kuwa uteuzi wa Mpoki ni sehemu ya safari ya kampuni hiyo kuongoza mageuzi katika vyombo vya habari nchini kwa kipaumbele cha kidijitali.

“Nina furaha kutangaza uteuzi wa Mpoki Thomson kuwa mhariri mtendaji mkuu wa Mwananchi Communications Limited (MCL), hatua muhimu katika safari yetu ya kufikiria kwa ajili ya zama za kidijitali,” ilisema taarifa hiyo.

Mpoki ambaye alianza kufanya kazi ya uandishi wa habari mwaka 2010 akiwa mhariri wa jarida la Bang chini ya Relim Entertainment, ni mzoefu wa zaidi ya muongo mmoja katika tasnia ya habari kwenye magazeti na mitandao ya kidijitali, huku akiakisi ubunifu wa kiuandishi na maono ya kisasa.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa katika kipindi chake akiwa mhariri mtendaji wa The Citizen, Mpoki aliongoza kwa kuleta mabadiliko ya kimkakati akisukuma maudhui yanayomgusa msomaji, ubora wa uhariri na ujumuishaji wa teknolojia mpya.

Katika nafasi yake mpya atakuwa kinara wa mabadiliko ya kiuhariri kwa lengo la kuongeza kasi ya uandishi wa habari wa kidijitali akiboresha maudhui katika majukwaa mbalimbali ili kuongeza ushiriki wa watazamaji na fursa za mapato na kukuza ubunifu katika uwasilishaji wa habari kwa kutumia takwimu na mbinu mpya zinazogusa wasomaji wa kizazi cha sasa.

Pia atakuwa na jukumu la kuimarisha viwango vya uhariri na uwajibikaji ili kuhakikisha maudhui yanabaki kuwa ya kuaminika katika jamii pamoja na kujenga utamaduni wa chumba cha habari uliojikita katika ubunifu, wepesi wa kujifunza na kubadilika kulingana na mabadiliko ya mazingira ya kihabari.