Mwandishi Mwanaspoti apewa cheti cha Heshima na Ubalozi wa Marekani

MWANDISHI wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited ambaye amekuwa akiandikia gazeti namba moja la michezo Tanzania, Mwanaspoti, Nevumba Abubakar, ameandika historia mpya katika taaluma yake baada ya kutunukiwa cheti cha heshima na Ubalozi wa Marekani, ikiwa ni sehemu ya kutambua umahiri wake kwenye utengenezaji wa maudhui ya kidigitali.

Nevumba amekuwa mmoja wa vijana wachache waliobahatika kushiriki katika warsha maalum ya miezi miwili iliyoandaliwa na ubalozi huo, ikilenga kuwawezesha waandishi na wabunifu wa maudhui kujifunza namna bora ya kusimulia simulizi za kijamii, kiutamaduni na kiuchumi kwa kutumia teknolojia za kisasa. 

Mafunzo hayo yalihusisha vipengele vya digital storytelling, multimedia production, content strateg na matumizi ya zana mbalimbali za kidigitali.

Kupitia uwezo na ubunifu aliouonyesha katika kipindi chote cha mafunzo, Nevumba alitunukiwa cheti rasmi kilichosainiwa na Kalisha Holmes, Afisa Habari wa Ubalozi wa Marekani, kama ishara ya kutambua mchango wake katika kizazi kipya cha watengenezaji wa maudhui wenye ushawishi na mwelekeo wa kimataifa.

Akizungumza baada ya kupokea cheti hicho, Nevumba amesema mafanikio hayo ni ya vijana wote wanaoamini katika nguvu ya maudhui yenye mwelekeo wa mabadiliko. 

“Ni heshima kubwa kwangu, na zaidi ni msukumo wa kuendelea kutumia kalamu na teknolojia kuandika stori zenye maana katika jamii,” amesema Nevumba.