Pamba Jiji yamfuata Ikangalombo | Mwanaspoti

PAMBA haitaki mchezo msimu ujao. Tetesi zinasema imetuma maombi kwa Yanga kumtaka winga wa mabingwa hao Jonathan Ikangalombo hata kwa mkopo ili aongeze nguvu msimu ujao.

Ikangalombo ambaye alikuwa akiichezea AS Vita, alitua nchini katika dirisha dogo huku mabosi wa Yanga wakimnunua na kumsainisha mkataba wa miaka miwili kukitumikia kikosi cha Wananchi.

Taarifa kutoka ndani ya Pamba Jiji zinasema; “Ni kweli tunamtaka Ikangalombo unajua wenzetu wale ni wakubwa inawezekana wao wanaona hawafai, lakini kwetu ni mchezaji mzuri ni kama amekosa nafasi tu ya kuonyesha uwezo wake.

“Tumewaomba watupe hata kwa mkopo hatuna shida kwenye malipo, tunachotaka ni kuwa na timu itakayoundwa na wachezaji wenye uwezo mkubwa kwa msimu ujao, tutasubiri majibu yao tu.”

Tangu atue Yanga ameonekana kuwa na wakati mgumu hasa kwa upande wa namba, huku hesabu za mabosi wa timu hiyo wakijipanga kumtoa kwa mkopo kwenda Singida Black Stars.

Taarifa za ndani zililiambia Mwanaspoti; “Uongozi wa mchezaji huyo umegoma kupelekwa kwa mkopo timu yoyote ila wanachotaka ni kuvunja mkataba kama hana nafasi ndani ya kikosi cha Yanga.”

Ikanga ana uwezo wa kutumika kwenye maeneo matatu tofauti eneo la mbele, winga wa kushoto, winga wa kulia na eneo la ushambuliaji.

Kocha Francis Baraza ameagiza kutafutiwa winga mwenye uwezo mkubwa, atakayesaidiana na John Nakibinge, ambaye amebakishwa ndani ya timu hiyo.

Mbali na winga, Pamba pia inatafuta beki wa kati, kiungo mkabaji na washambuliaji wawili kwenye hesabu za kukiongezea nguvu kikosi chao.

Pamba imetema wachezaji wake sita walioitumikia msimu wao wa kwanza uliopita tangu warejee Ligi Kuu wakiwemo, Abalkassim Suleiman, Cherif Ibrahim, George Mpole, Ibrahim Isihaka, Modou Camara na Lazaro Mlingwa