Pamba Jiji yamtambulisha Baraza akichukua mikoba ya Minziro

Pamba Jiji FC ya Mwanza imemtambulisha rasmi Francis Baraza kuwa Kocha Mkuu kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Bara akisaini mkataba wa mwaka mmoja.

‎Baraza ametambulishwa leo Jumatano Julai 30, 2025  jijini Mwanza, ambapo katika benchi lake atasaidiana na Temi Felix (Kocha Msaidizi), John Waw (kocha wa makipa), Shaban Kado (kocha msaidizi wa makipa), na George Aaron (Kocha wa viungo).

‎Baraza anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Fredy Felix ‘Minziro’ na msaidizi wake, Mathias Wandiba ambao mkataba wao umemalizika mwishoni mwa msimu uliopita.

‎Kocha huyo raia wa Kenya ana uzoefu mkubwa wa kufanya kazi Tanzania, akiwa ameshazifundisha Biashara United (Mara), Kagera Sugar (Kagera), Dodoma Jiji (Dodoma) na Tanzania Prisons (Mbeya).

‎Akizungumza baada ya kutambulisha benchi hilo jipya la ufundi, Mwenyekiti wa Pamba Jiji, Bhiku Kotecha amesema uongozi umempa baraka zote Baraza na hautamuingilia kwenye majukumu yake ya kuitengeneza timu hiyo ili ifanye vizuri.

‎Kotecha amempongeza kocha aliyemaliza muda wake, Fredy Felix ‘Minziro’ kwa kazi kubwa aliyoifanya na kuisaidia klabu hiyo kubaki kwenye Ligi Kuu, huku akimtakia kheri kwenye majukumu yake mapya.

‎”Minziro alifanya kazi nzuri akatufikisha hapa tulipo lakini tumeamua kubadilisha benchi, alifanya kazi yake na tunamtakia kila la kheri huko aendako,” amesema Kotecha.

‎Ameongeza kuwa; “Tumemwambia Mwalimu sisi uongozi hatutamuingilia katika mipango yake ya timu wala kumpangia cha kufanya tunachotaka ni atufanyie kazi tupate matokeo.”

‎Naye, Francis Baraza amesema yuko tayari kwa kibarua hicho kigumu kwani anajiamini kwa uzoefu alionao nchini akiwa anawafahamu wachezaji wengi, anaamini ana uwezo wa kuifanya timu hiyo kuwa kubwa na kumaliza katika nafasi tano za juu kwenye ligi.

‎”Uzoefu wangu niliokaa hapa niko tayari kwa hii kazi, najua ni kazu ngumu lakini naamini tukishikana pamoja matokeo yatapatikana na tutaona timu itabadilika,” amesema Baraza na kuongeza;

‎”Minziro amenifundisha tulikutana Yanga miaka hiyo akiwa kocha, na hapa Pamba amefanya kazi yake nampa heshima, pale alipoishia tutaendeleza. Wachezaji wengi wa Tanzania nawafahamu, tayari meneja amenitumia majina ya kikosi na nimewapitia wote.”

‎Kocha huyo raia wa Kenya aliyewahi kuzinoa Biashara United, Dodoma Jiji na Kagera Sugar, amesema ameifuatilia Pamba Jiji na anaifahamu kwa undani, huku akiomba uongozi kuhakikisha mambo ya usajili yanakamilika mapema ili kuanza maandalizi haraka na kikosi kiwe tayari Ligi itakapoanza.

‎”Lazima tushikane sisi Mwanza tukiweza kufanya kazi yetu vizuri kwa kushirikiana Pamba ina uwezo wa kumaliza katika nafasi tano bora hilo naliona,” amesema Baraza.

‎Ameongeza kuwa; “Tunachotakiwa ni kujiamini sisi wenyewe, jana nimeongea na viongozi nikawaambia kwamba nilichokifanya Biashara United kinawezekana hapa pia, tukifanyia mipango ya mapema timu itaimarika.”