Mbinu 36 za Kushinda Mapambano, yaani Thirty-Six Stratagems, zilizochorwa Karne ya Tano kama ramani ya vita na Jenerali wa China ya Kale upande wa Kusini, Wang Jingze na kuwekwa kwenye Kitabu cha Qi (Book of Qi), nazitumia kujenga muktadha.
Lengo ni kuunda picha pana dhidi ya vuguvugu la ‘uasi’ CCM na matokeo yanayotarajiwa. Kutoka sauti kubwa ya Humphrey Polepole hadi Josephat Gwajima, mitandaoni. Je, mbinu zao zinaweza kuleta matokeo wanayokusudia?
Mafundisho ya kihistoria zama za kale hadi mpya, yana maelekezo ya kimsingi, kwamba kumshinda mtawala, inabidi kwanza uheshimu nguvu zake, utambue mamlaka yake, na umkabili kwa kumzunguka.
Kiongozi (mtawala), akishakula kiapo na kupata utii kamili wa dola, huyo siyo wa kumwendea kwa mzaha. Unaweza kuwa na akili nyingi, lakini kama hutambui kuwa kumkabili mwenye mamlaka inataka nidhamu, subira, mipango na uchaguzi wa mbinu, utakwenda na maji.
Hakuwezekana Hussein Radjabu kumtikisa Pierre Nkurunziza, Burundi, wala Bakili Muluzi kwa Bingu wa Mutharika, Malawi. Radjabu ndiye alikuwa Kiongozi wa chama tawala, CNDD FDD, sawa na Muluzi, UDF.
Nguvu alizokuwa nazo Edward Lowassa, hazikuwa za kawaida. Hata hivyo, hakuweza kupenya mbele ya Jakaya Kikwete, aliyekuwa Rais na Mwenyekiti wa CCM, chama kinachoongoza dola. Madaraka yaleyale ya Kikwete, yameshikwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Katika Thirty-Six Stratagems, sura ya Kwanza, somo ni Mbinu za Kushinda (Winning Stratagems). Wang aliandika; ‘vuka bahari bila ufahamu wa mfalme.’
Hapo Wang alimaanisha kuwa kwa sababu alikuwa kwenye mapambano na mfalme, yaani mtawala, ilikuwa lazima apange mipango yake bila kumfanya Mfalme Ming amshtukie. Unaficha lengo kuu, ukitanguliza lengo bandia ili adui asikushtukie unataka nini.
Wang alikuwa Jenerali wa Southern Qi, hivyo vikosi vya jeshi la China Kusini vilikuwa chini yake. Kutokana na hali hiyo, ingedhaniwa yeye kumpindua au kumuua Mfalme Ming ni rahisi. Hata hivyo, alitambua nguvu ya mfalme, ndiyo maana alituliza kichwa na kuandika mbinu 36.
Polepole, jinsi alivyojitokeza, ni dhahiri ameamua kupambana. Ikiwa mapambano yake yana lengo la kuonesha udhaifu wa kiuongozi, sawa.
Kama shabaha yake ni kufanikisha kuona Rais Samia hashiriki Uchaguzi Mkuu 2025 au haapishwi kuendelea na muhula wa pili, hapo anajidanganya.
Mahali pa kumrejesha ni mifano iliyotangulia. Radjabu alikuwa mwenye nguvu kuliko wote ndani ya CNDD FDD. Hata hivyo, alipotofautiana na Nkurunziza, ambaye ni mwanachama wake, Radjabu alifungwa jela. Ni kwa sababu Nkurunziza ndiye alikuwa Rais.
Muluzi, kwa vile yeye ndiye alikuwa bosi wa UDF, na alimpa tiketi Mutharika, alijaribu kutumia chama kumdhibiti. Alichelewa kukumbuka kuwa Rais ana mamlaka makubwa na kumshinda, inataka utumie mbinu za Jenerali Wang.
Sura ya Tatu ya Thirty-Six Stratagems ni Mbinu za Kushambulia (Attacking Stratagems). Mbinu ya pili katika sura hiyo inasema; Borrow a corpse to resurrect a soul.
Tafsiri ya neno kwa neno ni kusema; kodisha maiti ufufue nafsi. Hata hivyo, kile ambacho Wang alikimaanisha ni kuwa ukishajua mbinu za adui unazikodi kisha unazitumia au timu yake pia unaichukua.
Mtu hawezi kuifahamu timu unayoitegemea kama hujajiweka wazi. Kitendo cha kutoka nje na kutangaza hadharani kumkabili Rais Samia, papo hapo Polepole ameshatengeneza mazingira ya kuchunguzwa.
Inafahamika, hakuna mwenye nyenzo za kuendesha uchunguzi kuliko rais wa nchi. Je, Rais Samia atakaa kimya bila kumzingatia Polepole au atataka kujua yupo na kina nani? Akishawajua waliojibanza kwenye upenyo wa Polepole, hatacheza karata zake na kusababisha kikundi kisambaratike?
Hoja za Polepole ukizichakata ni nadharia na hadithi za mtaani kuliko hali halisi. Nilimsikia Polepole akisema Rais Samia, alitakiwa kuongoza mchakato wa kupata mgombea mwingine wa urais. Yaani, Rais Samia hapaswi kugombea uchaguzi wa sasa.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ibara ya 37 (5), imeelekeza namna ambavyo Makamu wa Rais, anapaswa kushika madaraka ya nchi, baada ya Rais kupoteza sifa, ama kwa kifo, kujiuzulu, kuondolewa na Bunge, Baraza la Mawazuri au kiafya. Ibara ya 40 (4), inaelekeza fursa za Makamu Rais aliyeapishwa kuwa Rais, kugombea tena urais.
Sujui Polepole anatumia Katiba ipi kujenga hoja zake? Katiba ya CCM, ibara ya 100 (2), imetaja mamlaka ya Mkutano Mkuu CCM, na imesema uamuzi wake ndiyo wa mwisho. Kwamba Mkutano Mkuu CCM, unaweza kutengua, kuthibitisha, na kuamua chochote, 101 (3). Na Mkutano Mkuu ndiyo uliomteua Rais Samia kuwa mgombea. Mkutano Mkuu ulitumia mamlaka yake.
Polepole anatumia zaidi maneno “desturi” na “utamaduni”, wakati nchi inaongozwa na Katiba, vilevile CCM, ni chama kinachoendeshwa kwa Katiba yake. Kushupalia mambo, nje ya Katiba, ni nongwa. Halafu, nongwa ikizidi, hufubaza maarifa.
Inafahamika kuwa Rais Samia alipata wakati mgumu kukubaliwa kuapishwa kuwa Rais, baada ya kifo cha Dk John Magufuli. Wapo watu walijaribu kutaka kupindisha Katiba. Aliweka wazi, Jenerali mstaafu, Venance Mabeyo.
Nongwa za kushindwa kumzuia asiapishwe, hazipaswi kuendelea kuishi, hadi kujaribu kuinajisi Katiba. Ushauri kwa wahusika ni kuwa kumshinda Rais Samia, inataka kwanza kumheshimu, kuheshimu mamlaka na nguvu zake, kisha utumie akili, badala ya kupayuka. Hadi sasa, Polepole anapigana vita batili katika uwanja batili. Ni vigumu kushinda.