Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania imetimiza ndoto yake ya kihistoria ya kuwa mzalishaji na mnufaikaji mkubwa wa madini ya urani duniani.
Rais Samia amesema hayo leo Jumatano Julai 30, 2025 alipozungumza na wananchi wa Namtumbo, mkoani Ruvuma baada ya kutembelea na kuzindua kiwanda cha majaribio cha uchenjuaji wa madini ya urani kilichojengwa na Kampuni ya Mantra Tanzania Limited kutoka Russia, katika eneo la Mto Mkuju wilayani humo.
Katika hafla hiyo, Rais Samia amesema kutokana na mradi huo wenye uwekezaji wa Dola 1.2 bilioni za Marekani (sawa na Sh3 trilioni) unakwenda kuwanufaisha Watanzania kapitia fursa mbalimbali zikiwamo za ajira, uzalishaji wa umeme na ongezeko la Pato la Taifa.
Amesema kutokana na mradi huo ambao Serikali imewekeza hisa ya asilimia 20, Serikali itajipatia kipato cha Dola 40 milioni za Marekani (zaidi ya Sh104 bilioni) kwa mwaka zitakazoingia katika mfuko wa Serikali na kuwezesha shughuli mbalimbali za maendeleo ya Taifa.
“Serikali ina asilimia 20 ya hisa katika kampuni hii, hivyo itanufaika kwa kujipatia Dola za Marekani 40 milioni kwa mwaka kutokana na uwekezaji wa kiwanda hiki.
Niwaombe ndugu zangu wa Namtumbo muupokee mradi huu na muone ninyi ni sehemu yake kwani utaleta maendeleo makubwa hapa Namtumbo,” amesema.
Mbali na gawio hilo linalotokana na hisa, mradi huo pia ulielezwa kuchangia katika uzalishaji wa umeme wa uhakika nchini ukibainishwa madini ya urani ni malighafi muhimu inayokuwa kwa kasi katika uzalishaji wa umeme duniani kwasasa.
“Mahitaji ya urani yameongezeka duniani kwani ni malighafi muhimu katika uzalishaji wa umeme kwa mataifa mengi kwasasa, hivyo kiwanda hiki kinakwenda kusaidia katika uzalishaji wa umeme wa uhakika hapa nchini,” amesema Rais Samia.

Rais Samia Suluhu Hassan akihutubia wananchi katika uwanja wa Shule ya Sekondari Likuyu mara baada ya uzinduzi wa Kiwanda cha Majaribio cha Kuchenjua Urani cha Mantra Tanzania Limited kilichopo katika Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, leo Julai 30, 2025.
Amesema kupitia mradi huo, Tanzania inaingia katika orodha ya nchi 10 wachenjuaji wa urani duniani huku ikiwa na mradi mkubwa zaidi katika ukanda wa Afrika.
Akitolea mfano mataifa yanayozalisha umeme wa urani kwa sasa, amesema asilimia 20 ya umeme unaozalishwa Marekani unatokana na madini ya urani huku Ufaransa ikizalisha asilimia 65 ya umeme kutokana na madini ya urani.
Nchi nyingine zinazozalisha umeme wa urani ni Korea Kusini ambayo asilimia 30 ya umeme wake unatokana na urani huku kwa Bara la Afrika, Rais Samia amesema tangu mwaka 1984 Afrika ya Kusini imekuwa mzalishaji pekee wa umeme wa urani huku Misri ikijenga mitambo ya nyuklia kuanza uzalishaji wa umeme huo.
Awali, akitoa taarifa ya kiwanda hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mantra Tanzania Limited, Aleksandrs Starikovs amesema kiwanda hicho kitazalisha zaidi ya ajira 4500 za muda na ajira 700 za kudumu kwa Watanzania.
“Kiwanda hiki, katika shughuli mbalimbali kitawezesha takribani ajira 4500 za muda na ajira 700 za kudumu kwa watanzania kupitia shughuli zake mbalimbali,” amesema.
Akiishukuru Serikali ya Russia kwa fursa hiyo kwa Watanznia, Rais Samia amesisitiza katika fursa za ajira hizo, kipaumbele kikubwa wapewe vijana wanaopatikana maeneo ya jirani na mradi huo ili kuchochea maendeleo kwa wananchi hao.
Akizungumzia mchango wa sekta ya madini katika uchumi wa Taifa, Rais Samia amesema sekta hiyo imeongeza mchango wake katika pato la Taifa kutoka Sh623.2 bilioni mwaka 2022/23 hadi kufikia Sh1.01 trilioni mwaka 2023/24.
Amesema uwekezaji wa kiwanda cha uchenjuaji wa madini ya kimkakati ya urani, unakwenda kuongeza zaidi mchango wa sekta hii katika pato la Taifa, hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi.
“Dira 2050 imeitazama sekta ya madini kama sekta muhimu sana katika ujenzi wa uchumi wa nchi, mradi huu wa madini ya kimkakati ya urani, ni sehemu ya utekelezaji wa dira yetu 2050,” amesema Rais Samia.
Mbali na manufaa makubwa ya mradi huo, Rais Samia ametoa wito kwa mamlaka za masuala ya mazingira nchini kuhakikisha mradi huo unaendeshwa kwa kufuata sheria zote za uhifadhi wa mazingira.
“Kwa kuwa nchi yetu inaanza mradi wa urani kwa mara ya kwanza, niwaombe mamlaka zote za mazingira kuhakikisha mradi huu unasimamiwa kwa kuzingatia sheria za utunzaji wa mazingira,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde ameitaka Halmashauri ya Namtumbo kuhakikisha wanabuni miradi yenye tija kwa wananchi itakayotekelezwa na kampuni hiyo kupitia utekelezaji wa miradi ya uwajibikaji wa kampuni kwa jamii (CSR).
Amesema mradi huo wa kimkakati utafungua milango ya ujenzi wa mtambo mkubwa zaidi wa urani Afrika Mashariki na Kati, na kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi tano pekee barani Afrika zenye uwezo wa kuchakata madini hayo.
“Mheshimiwa Rais, mradi huu unakwenda kuleta mapinduzi makubwa katika sekta ya madini na kuchochea maendeleo ya Wilaya ya Namtumbo, Mkoa wa Ruvuma na Taifa kwa ujumla,” amesema Mavunde.