Dar es Salaam. Rais wa Ivory Coast, Alassane Ouattara ametangaza kugombea muhula wa nne kwenye kiti cha urais katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25, 2025.
Ouattara mwenye umri wa miaka 83, aliyeiongoza nchi hiyo ya Afrika Magharibi kwa karibu miaka 15 sasa, ametangaza jana Jumanne Julai 29, 2025, ingawa awali alinukuliwa akisema angependa kuachia ngazi.
Kwa mujibu wa RFI na Reuters Rais huyo, alichaguliwa tena kwa muhula wa tatu wenye utata mwaka 2020. .
“Katiba ya nchi yetu inaruhusu mimi kutumikia muhula mwingine na afya yangu inaruhusu,”aliandika Ouattara kwenye mtandao wa X.
Rais huyo alichaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa rais wa nchi hiyo inayoongoza kwa uzalishaji wa kakao duniani mwaka 2010.
“Ninagombea nafasi hii kwa sababu nchi yetu inakabiliwa na changamoto zisizokuwa na kifani za kiusalama, kiuchumi na kifedha ambazo zinahitaji uzoefu kuzisimamia.”
“Hii ndiyo sababu baada ya kuzingatia kwa makini na kwa dhamira safi, ninatangaza leo kwamba nimeamua kuwa mgombea katika uchaguzi wa rais wa Oktoba 25, 2025,” Ouattara alimalizia.
Mwaka 2011 baada ya uchaguzi uliomuingiza madarakani watu 3,000 waliuawa kwenye mapigano, yaliyotokana na rais aliyekuwepo madarakani wakati huo Rais Laurent Gbagbo kukataa kukubali ushindi wa Ouattara kwenye uchaguzi huo wa 2010.
Gbagbo alifurushwa madarakani, kukamatwa na baadaye kushitakiwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC).
Katika mapigano hayo, waliokuwa wanamuunga mkono Ouattara walikuwa wakipigana dhidi ya majeshi yanayomtii Rais Gbagbo aliyeng’ang’ania madaraka.
Gbagbo alikaidi wito wa kimataifa wa kukabidhi madaraka kwa amani kwa Ouattara, ambaye Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika unamtambua kama mshindi wa uchaguzi wa Rais uliofanyika Novemba 2010.
Ouattara katika andika hilo la mtandaoni amewaahidi wananchi wa nchi hiyo uchaguzi wa amani, demokrasia na uwazi, ingawa viongozi wa vyama vya upinzani wa nchi hiyo wanashutumu mchakato wa uchaguzi, hasa kutokana na kukataliwa kwa wagombea wakiwamo Tidjane Thiam na Gbagbo.