SERIKALI YAENDELEA KUTOA KIPAUMBELE KWA MAENDELEO YA MICHEZO – MSIGWA

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesisitiza
dhamira yake ya kuendelea kuwekeza katika sekta ya michezo kwa kujenga
miundombinu bora na kuweka mazingira wezeshi kwa maendeleo ya vipaji vya vijana
nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Ndugu
Gerson Msigwa, wakati wa mapokezi ya Timu ya One Tanzanite Football Academy
katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, mara baada ya
kurejea kutoka nchini Denmark.

Timu hiyo ya vijana iliitumikia vyema Tanzania kwa kushiriki
na kutwaa ubingwa wa Mashindano ya Kimataifa ya DANA CUP, mashindano maarufu
kwa kukuza vipaji vya soka la vijana duniani.

“Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa maendeleo
ya michezo, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa viwanja bora, vituo vya mafunzo na
programu za kukuza vipaji. Tunatoa wito kwa sekta binafsi kushirikiana nasi
katika kuendeleza vipaji vya vijana wetu,” amesema Msigwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa One Tanzanite
Football Academy, Bw. Agapiti Manday, ameishukuru Serikali kwa namna
inavyotambua mchango wa michezo katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Ameeleza kuwa kituo hicho kitaendelea kuwekeza katika
mafunzo ya vijana na kuhakikisha Tanzania inaendelea kushiriki katika
mashindano ya kimataifa kwa mafanikio.

“Ushindi huu ni matokeo ya kujituma kwa vijana wetu, pamoja
na mazingira mazuri ya mafunzo tunayowapa. Tunaiomba Serikali iendelee kuwekeza
katika ujenzi wa viwanja bora ili vipaji zaidi viweze kustawi,” amesema Manday.