Moshi. Serikali imetoa zaidi ya Sh28.2 bilioni kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa ujenzi wa barabara ya Lower yenye urefu wa kilomita 10 wilayani Rombo ambayo itasaidia kufungua fursa za kibiashara katika mpaka wa Holili na Tarakea, wilayani humo.
Mkataba wa ujenzi wa barabara hiyo umesainiwa leo Julai 30, 2025 baina ya Serikali na mkandarasi, kampuni ya M/S Kings Builders Ltd, inayotekeleza mradi wa ujenzi wa barabara hiyo ambayo itajengwa kwa muda wa miezi 18.
Akizungumzia ujenzi wa barabara hiyo, Meneja wa Tanroads Mkoa wa Kilimanjaro, Motta Kyando amesema tayari Serikali imetoa fedha zaidi ya Sh28.2 bilioni ambapo ujenzi huo utaanzia Ikuini na itaishia Kijiji cha Kirongo chini, kata ya Kirongo Samanga, wilayani humo.
Kyando amesema barabara hiyo ambayo inapita mpakani mwa Kenya na Tanzania, itasaidia kukuza shughuli za kijamii, kiuchumi na utalii kupitia nchi jirani ya Kenya katika mpaka wa Tarakea na Holili.
“Serikali kupitia Wakala wa Barabara (Tanroads) mwaka 2023/24 ilitenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa kiwango cha lami kipande cha kilomita 10, kinachoanzia Kijiji cha Ikuini na kuishia Kijiji cha Kirongo chini,” amesema Kyando.
Kyando amesema kukamilika kwa ujenzi wa barabara hiyo kutafungua fursa za kibiashara na kurahisisha usafirishaji wa bidhaa mbalimbali na hivyo kukuza uchumi wa nchi na kuongeza ufanisi katika sekta ya usafiri na usafirishaji.
Aidha, amesema barabara hiyo itatoa mchango mkubwa katika shughuli za utalii katika Ziwa Chala lililopo wilayani humo.
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha hizo kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo na kusema itaacha alama kubwa na kukuza uchumi wa wananchi.
Aidha, Profesa Mkenda amesema barabara inayotumika kwa sasa imekuwa na ajali za mara kwa mara kutokana na kona kuwa nyingi, hivyo kukamilika kwake kutasaidia kupunguza matukio hayo ya ajali.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amemtaka mkandarasi huyo kuhakikisha anatekeleza mradi huo kwa wakati kwani Serikali imeshatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo.
“Hii barabara tumeipigania kwa muda mrefu lakini leo tunaikamilisha, tunamshukuru Mungu,” amesema Babu.
Amesema: “Nikuombe mkandarasi, Rais Samia Suluhu Hassan hataki maneno kwenye kazi, ameshatoa fedha barabara ianze kujengwa,” amesema Babu.
Naye Fabianus Lyamuya kutoka kampuni hiyo ya ujenzi amesema watahakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati na kwa muda uliopangwa.