Moshi. Aliyekuwa mbunge wa Viti Maalumu Shally Raymond, ameibua shangwe kutoka kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalumu wa Umoja Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT) Mkoa wa Kilimanjaro, licha ya jina lake kutojumuishwa katika orodha ya walioteuliwa kugombea nafasi hiyo.
Mkutano huo unafanyika leo Jumatano Julai 30, 2025 katika Uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi chini ya usimamizi wa Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk Batilda Burian.
Shally alikuwa miongoni mwa makada waliochukua fomu kuomba kuteuliwa na chama hicho kugombea nafasi hiyo, lakini jina lake halikurudi.
Walioteuliwa na chama hicho kugombea ubunge viti maalumu kwa Mkoa wa Kilimanjaro ni Esther Malleko, Zuena Bushiri, Regina Chonjo, Caroline Lyimo, Pamela Mallya, Never Zekeya, Mary Nashanda na Aika Ngowi.
Akiingia katika eneo hilo la mkutano, Shally alishangiliwa na wajumbe, hali iliyomfanya Katibu wa UWT Mkoa wa Kilimanjaro, Jane Chatanda kuwataka wajumbe kutulia.
Alipoingia alianza kuwapungia mkono wagombea kisha wajumbe, hali iliyoibua kelele za shangwe na Chatanda akamuomba akakae huku akiwasihi wajumbe watulie.
“Wajumbe naomba utulivu, mama Shally naomba uende ukakae,” amesema Katibu wa UWT Mkoa.
Hata hivyo, wajumbe waliendelea kushangilia hadi alipokwenda kukaa kwenye nafasi yake.
Akizungumza katika mkutano huo wa uchaguzi, Dk Burian amewaomba wajumbe kumpa ushirikiano ili uchaguzi huo ufanyike kwa amani, haki na utulivu na kila mmoja atakapotoka hapo awe ameridhika na kusiwepo na lawama wala malalamiko.
Katika mkutano huo, wajumbe 1,329, wanatarajiwa kupiga kura kuamua wabunge wa viti maalumu.