Missenyi. Joto la kisiasa limepanda katika Jimbo la Missenyi baada ya wagombea wawili wa ubunge, Projestus Tegamaisho na Frolente Kyombo, kurushiana maneno hadharani wakati wa kujitambulisha kwa wajumbe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Kata ya Kashenye.
Mzozo huo ulizuka baada ya Tegamaisho, aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi, kumtuhumu Kyombo kwa kushindwa kushiriki katika ujenzi wa ofisi ya CCM ya wilaya hiyo, akidai kuwa hata mchanga wa msingi wa jengo hilo hakuweza kuchangia.
“Mpaka leo hakuna hata Mbunge aliyejitokeza kujenga ofisi ya chama ya wilaya, wote wanaingia ofisi za ajabuajabu kuchukua fomu, wanagombea ubunge wanajiondokea sisi tunabaki kupiga miayo,”amesema Tegamaisho.
Nakuongeza kuwa ameongoza harambee ya kuchangia ujenzi wa jengo la CCM lenye ukumbi wa kuingia watu 300.
“Bahati nzuri ndugu yangu Frolente Kyombo ni shahidi hata koleo moja la mchanga hajawahi kuweka,” amesema.
Kauli hiyo ilimkera Kyombo, ambaye ni Mbunge anayemaliza muda wake wa jimbo hilo, na kujibu kwa mkazo akisema, amepeleka maendeleo mengi Misenyi ikiwemo miundombinu ya barabara, umeme na kuwakilisha mkoa huo kwa kushika nyadhifa ya kuwa katibu msaidizi wa CCM Bungeni.
“Tusirudi nyuma, tuendeleze mambo tumalizie..tumefanya kazi kubwa na nyie mmeona nawaomba mfanye maamuzi sahihi msirudi nyuma,”amesema.
Tegamaisho na Kyombo ni miongoni mwa wagombea saba waliopitishwa na Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya na kupitishwa na Kamati Kuu ya CCM Taifa kuwania kiti cha ubunge Jimbo la Missenyi.
Wagombea wengine waliopitishwa ni pamoja na Assumpter Mshama, Jacklyne Rushaigo, Amina Athumani, Nasiru Byabato na Placidius Ndibalema.
Hali hiyo imetulizwa na Mkurugenzi wa uchaguzi wa CCM wilayani Missenyi, Bakari Mwacha baada ya kusimama na kuwaomba utulivu, huku akizuia watia nia hao kupigiwa makofi na wajumbe.
“Niombe wagombea wote mfuate taratibu za kujinadi sihitaji kusikia mtu anamtaja kwa jina mwenzake kila mtu awaeleze wajumbe endapo akipewa ridhaa kitu gani atafanya kwa maendeleo ya jimbo,” ameelekeza.