Udanganyifu ujazaji fomu za afya tishio

Dar es Salaam. Wakati fomu za taarifa za afya kwa wafanyakazi na wanafunzi wanaojiunga na shule, vyuo au taasisi zikilenga kuhakikisha usalama wa kiafya na mazingira salama ya kujifunzia na kufanya kazi, imebainika baadhi ya zinazowasilishwa siyo sahihi.

Sababu za kuwasilisha taarifa zisizo za kweli zinatajwa kuwa ni wananchi kuepuka mzunguko wa vipimo, gharama na muda wa kusubiri majibu, hali inayosababisha wachague njia za mkato zinazoweza kuhatarisha afya za wahusika.

Kwa upande wa shule, fomu hizo hutolewa kwa zile za bweni za umma na binafsi, huku zile za kutwa wazazi hutakiwa kuwajulisha walimu kuhusu changamoto za kiafya za mwanafunzi husika.

“Kwenye shule zetu za msingi za Serikali hatuna hizo fomu ila inatakiwa mzazi kumueleza mwalimu changamoto aliyonayo mtoto wake na wengine wanawekewa alama kuashiria kuwa ana changamoto,” amesema mwalimu katika Shule ya Msingi Ubungo, Dar es Salaam, hivi karibuni.

Fatuma Mkwawa, mkazi wa mkoani Iringa amesema changamoto iliyopo ni baadhi ya watu kutotunza siri, hivyo wengine kuamua kupeleka majibu ya uongo.

“Mtu anapopima au kueleza maradhi yake kwa mwajiri au mwalimu wapo wanaokiuka maadili ya kazi kwa kutoa siri za maradhi ya mtu na kufanya utendaji wake wa kazi au kusoma kunashuka kwa sababu ya maneno wanayoambiwa na jamii inayowazunguka,” amesema.

Mwanasaikolojia, Clara Mwambungu amesema sababu ya kutoa taarifa zisizo sahihi ni hofu inayotokana na mazingira yasiyo rafiki ya utoaji wa huduma na kutokuwepo kwa ulinzi wa taarifa binafsi.

“Hofu ya kujua hali halisi ya kiafya ni jambo linaloathiri watu wengi, hasa vijana waliopo katika hatua muhimu za maisha kama vile kujiunga na chuo au kuomba kazi. Wengi huamini kuwa taarifa za kiafya, hasa zikiwa na ugonjwa wa muda mrefu au wa kuzaliwa nao, zinaweza kuwa kama hukumu ya maisha yao,” amesema Clara.

Amesema hofu hiyo inachochewa zaidi na kutokuwepo usiri wa kutosha kwenye taasisi zinazopokea fomu hizo, ikiwamo shaka juu ya walimu, maofisa rasilimaliwatu na viongozi wa taasisi kutumia vibaya au kufichua taarifa hizo.

“Wapo wanafunzi na waajiriwa watarajiwa wanaoogopa kuwa wakijaza ukweli kwenye fomu za afya, taarifa hizo zinaweza kutumiwa dhidi yao aidha kunyimwa nafasi, kubaguliwa au kusemwa hadharani. Kuna hali ya kutoaminiana kwamba walimu au viongozi hawataheshimu usiri wa taarifa hizo,” amesema.

Amesema vitendo vya baadhi ya watendaji kujadili afya za watu bila idhini yao au kutoa dokezo kwa wenzao, huzua hofu kubwa ya unyanyapaa, jambo ambalo huwaathiri kisaikolojia na kuwafanya watu wachague kuficha ukweli.

“Taarifa za kiafya ni siri ya mtu binafsi zinapovuja au kushughulikiwa bila weledi, si tu kwamba zinadhalilisha, bali huathiri kabisa hali ya mtu kujitambua na kujiamini. Tukiwa na mfumo unaolinda kwa dhati faragha za kiafya, watu wengi watajitokeza kwa uwazi bila woga,” amesema.

Ameshauri ni muhimu kwa taasisi zote za elimu, ajira na afya kuweka mifumo madhubuti kulinda taarifa za watu na kutoa elimu kuhusu umuhimu wa kujua hali ya afya mapema kwa ajili ya msaada wa haraka na uokoaji wa maisha.

Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) kimesema suala la usiri wa taarifa binafsi za wafanyakazi si hiari ya mwajiri au mtu binafsi bali ni wajibu wa kisheria, huku kikitoa wito kwa waajiri wote nchini kuhakikisha wanazingatia Sheria ya Utunzaji wa Taarifa Binafsi ya mwaka 2023.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa ATE, Suzanne Ndomba amesema wanashauri waajiri kuwapatia mafunzo wafanyakazi wao juu ya athari zinazoweza kujitokeza endapo mfanyakazi atatoa taarifa zisizo sahihi, hasa kuhusu afya, jambo linaloweza kuchukuliwa kama kosa la kinidhamu.

“ATE imekuwa ikiendesha mafunzo mbalimbali, likiwamo somo maalumu la utunzaji wa taarifa binafsi kwa wanachama wake,” amesema.

Amesema waajiri wanashauriwa kuhakikisha mikataba inazingatia kuwa na vifungu vinavyosimamia utunzaji wa siri kati ya pande zote mbili.

Hii ni pamoja na utengenezaji wa sera za ndani za mwajiri: Sera za usiri, sera za kutunza taarifa binafsi kwa wanachama wake, ambazo huainisha aina za taarifa zinazokusanywa, namna ya kutunza taarifa hizo, kuweka miongozo ya namna gani taarifa zitatakiwa kutolewa na nani atahusika na kwa utaratibu gani, pia hutoa jukumu kwa kila pande kutunza siri.

Pia, ametoa wito kwa waajiiri kujisajili kwenye Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi kama inavyotakiwa na sheria ili kuhakikisha zoezi zima la utunzaji wa taarifa linasimamiwa ipasavyo.

Wapo wazazi na waomba ajira wanaosema changamoto ya mazingira na gharama huwasababisha kutumia njia za mkato kujaza fomu hizo licha ya kutambua zina madhara.

“Nilipopewa barua ya kujiunga na ajira pamoja na fomu hiyo nilikwenda hospitali nikamtafuta mtu akanipeleka kwa daktari ili kuijaza kwa gharama ya Sh5,000. Hii ni kwa sababu kila kipimo nilichouliza kinalipiwa jumla ilifika Sh100,000 na sikuwa na kiasi hicho cha pesa,” amesema Benson Isack mkazi wa jijini Dar es Salaam.

Kwa upande wake, Judith Kileo amesema kutokana na baadhi ya vipimo majibu yake hutolewa kwa kuchelewa, alimuomba daktari amjazie pasipo mtoto wake kupimwa.

“Tunajua kuwa si sawa kufanya hivyo, tatizo ni muda pia wakati mwingine ni uelewa tu kwa wazazi hakuna, kwa kuona siyo muhimu kufanya vipimo halali,” amesema.

Dk Faraja Kristomus wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) amesema udanganyifu unaofanyika unatokana na kutokuwa na mazingira rafiki ya utoaji huduma ya vipimo.

“Bima zetu zimekuwa na changamoto kwa kudai baadhi ya magonjwa hayalipii, hii inatengeneza mwanya wa kupita njia fupi,” amesema.

Vilevile amesema baadhi ya madaktari hawafuati maadili ya kazi, hivyo kuandika pasipo vipimo kufanyika.

Athari kwa watoto, taasisi

Dk Kristomus amesema udanganyifu huo umekuwa chanzo cha baadhi ya wanafunzi kukumbwa na magonjwa ambayo baadhi ya wazazi huyahusisha na imani za kishirikina baada ya mtoto kufika elimu ya chuo.

“Wakati mwingine kuna magonjwa yanajitokeza ukubwani, unakuta mwanafunzi kaanza chuo jambo hilo linajitokeza, badala ya kuhangaika naye wazazi wanalalamika mtoto wao amefanywa vibaya baada ya kuingia chuo kwa kuonewa wivu,” amesema Dk Kristomus.

Amesema athari kubwa hujitokeza badala ya kusoma, mtoto hutumia muda mwingi kwenye matibabu na wakati mwingine kuacha masomo au hufeli.

Mkuu wa shule iliyopo mkoani Kilimanjaro, Jackson Shayo amesema ujazaji fomu usio sahihi huwanyima watoto haki ya kupata msaada wa haraka wanapopata changamoto za kiafya.

Amesema hilo hutokana na shule au taasisi husika kukosa taarifa sahihi kuhusu historia ya afya ya mwanafunzi.

“Wazazi wengine hujaza majina na umri pekee, lakini sehemu ya historia ya magonjwa kama vile pumu, kifafa au mzio (allergy) wanaacha tupu au kuandika uongo kwa kuficha siri. Siku mtoto akizimia au kupata shambulio shuleni hakuna anayejua aanze wapi,” amesema.

Shayo amesema mzazi anapojaza fomu ya afya ni lazima atambue hiyo si karatasi tu ya kukamilisha usajili, bali ni nyenzo ya kuokoa maisha ya mtoto.

Daktari kutoka Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya, Ernest Winchislaus amesema kinachofanyika siyo tu ni hatari kiafya, bali pia ni kinyume cha sheria na maadili ya taaluma ya kitabibu.

“Licha ya kuwa ni kinyume cha maadili, madhara yake ni kwamba mtoto akipatwa na changamoto walimu hawajui cha kufanya kwa sababu historia yake halisi haipo,” amesema.

Dk Winchislaus amesema hatua hiyo humfanya mtoto ashindwe kupata msaada wa haraka anapohitaji huduma ya afya ya dharura kwa kuwa hakuna taarifa sahihi ya awali inayoweza kusaidia wahudumu wa afya kutoa tiba inayofaa.

“Mfano, kama mtoto ana mzio au hali ya kiafya inayoathiri kinga ya mwili wake na haya hayajaandikwa kwenye fomu, inaweza kuhatarisha maisha yake au ya wenzake. Hii si tu kudanganya, bali ni kuchezea uhai,” amesema.

 “Kwa mujibu wa sheria, madaktari hatuwezi kuandika kwa kusema tu mtu anahitaji cheti, lazima tufanye tathmini sahihi. Kutoa cheti bila kufanya hivyo ni kuvunja sheria na maadili ya kitabibu.”

Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Mugisha Nkoronko amesema kinasimamia misingi ya maadili ya taaluma na kufanya kazi kwa weledi, hivyo wanaojaza fomu hizo pasipo vipimo kufanyika wakibainika watashtakiwa kwa kosa la kutoa taarifa za uongo na hukumu yake ni faini, kifungo au vyote kwa pamoja.

“Ikumbukwe kuwa vipimo hivyo vina malengo ya kubaini utimamu wa mwili na mahitaji ya kiafya yanayohitajika ili ama mtumishi, mwanafunzi au waajiri watimize wajibu wao kikamlilifu,” amesema  Dk Nkoronko.

Amesema anayetakiwa kufanya vipimo ni daktari aliyesajiliwa na anatakiwa kujiepusha na ushawishi wa aina yoyote, ikiwamo vitendo vya udanganyifu na mashinikizo ya kupindisha ukweli.

“Kila anayehitaji kupata huduma ya medical examination (uchunguzi wa kitabibu) anatakiwa kupimwa kama inavyotakiwa kwenye fomu ya maombi na si kuandikiana tu,” amesema.