Wakulima wasio na ‘Kadi Janja’ Songwe kukosa fursa

Songwe. Wakulima wa kahawa mkoani Songwe wametakiwa kujisajili katika mfumo wa kidigitali na kupewa kadi janja ili kukunufaika na fursa mbalimbali ikiwamo mbolea za ruzuku, huduma za kifedha na bima.

Akizungumza leo Julai 29, 2025 kwenye uzinduzi wa mfumo huo unaotekelezwa na kampuni ya Byz Tech kwa kushirikiana na bodi ya kahawa nchini (TCB), Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Hamad Mbega amesema shughuli hiyo itaenda kuwanufaisha wakulima kiuchumi.

Amesema Serikali inaendelea kufanya juhudi mbalimbali kuhakikisha kilimo cha kahawa kinakuwa na soko kwa kuboresha mazingira ya wakulima na kwamba Mbozi inategemea zaidi kilimo.

“Kwa kushirikiana na wadau wengine, serikali inaendelea kuweka miundombinu mizuri kwa wakulima hasa wa zao la kahawa ili kufanya vizuri kama uchimbaji mabwawa na barabara,” amesema Mbega.

Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea nchini (TFRA) Nyanda za Juu Kusini, Joshua Ng’ondya amesema hatua hiyo ni utekelezaji katika mkakati wa kuwahudumia kwa ufasaha wakulima.

Amesema kadi janja zitakazotolewa kwa wakulima si tu kuwatambua, bali wataweza kupata huduma mbalimbali ikiwamo mbolea za ruzuku na kwamba kwa hatua za awali wameanza na wakulima wa kahawa.

“Tutatambua mashamba yao na kujua kiwango cha pembejeo zinazohitajika kwa kiwango gani, mbolea za ruzuku na kutambuliwa na kwa hatua za awali tumeanza na wakulima wa zao la kahawa.

“Wakulima wote waliosajiliwa kwenye mpango wa ruzuku watafikiwa na kupewa kadi janja, shughuli hii ni endelevu na hadi sasa tumewafikia wakulima 176,747 japo tunahitaji wakulima milioni 1.8 kwa ukanda wetu,” amesema Ng’ondya.

Mkurugenzi wa Byz Tech, Mahmoud Shoo amesema matarajio yao kwa wakulima ni kuzalisha kahawa yenye ubora kuweza kushindana kwenye soko la kimataifa huku wakitunza mazingira.

Amesema mafunzo waliyotoa kwa washiriki 160 mkoani humo wanaamini yanaenda kubadili maisha ya wakulima na kuongeza tija kwenye uzalishaji na kupunguza changamoto ya maafisa ugani.

“Tumekutana na wakulima 160, hatuishii kuzungumza nao bali kufika hadi mashambani kuona shughuli za kilimo chenye tija na uzalishaji ambao utaleta soko shindani bila kukata miti” amesema Shoo.

Meneja wa Bodi ya Kahawa Kanda ya Mbeya, Ezekiel Mwakajoma amesema hatua hiyo inaenda kufungua fursa nyingi kwa wakulima kwa kupata uhakika wa soko ndani na nje ya nchi kupitia mradi wa European Union Deforestation Regulation (EU-DR).

“Bodi ya kahawa inafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na wadau mbalimbali ikiwamo vyama vya ushirika, hivyo hii ni fursa kubwa kwa wakulima kuweza kupata uhakika wa soko kupitia mradi na mfumo huu,” amesema Mwakajoma.

Mmoja wa wakulima, Aron Kasabela amesema pamoja na mfumo huo kwenda kuwasaidia, ameiomba serikali kutofuta majina ya wakulima kwenye vyama vya ushirika (Amcos) kwa ajili ya ruzuku.

“Ni mfumo mzuri unaoenda kututambua na kutupa fursa nyingine, lakini nitoe angalizo na ombi kwa serikali kutofuta majina ya wakulima wa ruzuku kwenye Amcos, hali hii itaathiri watu haswa wale wa chini na vijijini, lakini tunaomba huu mfumo wa kadi janja usiishie mjini,” amesema Kasabela.